Mwekezaji mpya Bagamoyo kuanza uzalishaji magari, boti za uvuvi

Dar es Salaam. Hadi mwishoni mwa mwaka huu, Tanzania inaweza kuwa na kiwanda cha uunganishaji wa magari makubwa yanayotumia gesi, boti za uvuvi na vipuri vya magari, kufuatia uwekezaji mpya unaotarajiwa kufanyika katika eneo la Bagamoyo mkoani Pwani.

Mbali na viwanda hivyo vitatu, vingine 147 ambavyo vitahusisha utengenezaji wa pikipiki vifaa vya ujenzi navyo vitakuwa vinaendelea kujengwa.

Hiyo ni baada ya kampuni ya HWTZ SEZ Limited na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), kusaini mkataba wa upangishaji hekta 500 za ardhi katika eneo la uwekezaji Bagamoyo kwa ajili hiyo.

Uwekezaji katika magari yanayotumia gesi asilia unafanyika wakati ambao dunia inashuhudia kupanda na kushuka kwa bei za mafuta, jambo ambalo linaathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Tanzania ni miongoni mwa waathirika wa hali hiyo na tayari wasafirishaji wa abiria na mizigo wamepaza sauti kutaka mabadiliko ama ya nauli au bei za mafuta kwa kuwa vinawaathiri.

Akizungumzia suala hilo, leo Alhamisi, Aprili 9, 2026, Mkurugenzi wa Tiseza, Gilead Teri amesema kuanza kuunganishwa kwa magari hayo kutapunguza kiwango cha uagizaji mafuta na kuchochea matumizi ya gesi asilia.

“Tanzania tuna nishati ya gesi asilia, ujio wa kiwanda hiki utasaidia kuchochea matumizi yake na kupunguza uagizaji wa mafuta,” amesema Teri.

Amesema Tanzania imeendelea kuvutia uwekezaji, hasa katika huku akitolea mfano wa maombi matano ya uanzishaji viwanda hivyo yaliyopokewa kati ya Januari hadi Machi mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Gilead Teri akizungumza na wanahabari juu ya kampuni ya HWTZ SEZ Limited kuanza uzalishaji wa magari ya gesi, boti za uvuvi na vipuri vya magari unaotarajiwa kufanyika katika eneo la Bagamoyo mkoani Pwani

“Mwaka 2021 tulikuwa na kiwanda kimoja pekee cha kuunganisha magari, hadi mwaka 2025 tulikiwa navyo vinne na miezi mitatu pekee tumepata maombi matano. Hii inaonyesha namna gani Tanzania inaendelea kuvutia wawekezaji katika eneo hili,” amesema.

Kuhusu mkataba huo, amesema kampuni imepewa umiliki wa ardhi hiyo kwa muda wa miaka 33.

Amesema kupitia uwekezaji huo, Tanzania itanufaika kwa kuongeza uzalishaji wa ndani wa bidhaa muhimu za viwandani ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiagizwa kutoka nje ya nchi, hali itakayosaidia kupunguza gharama za uagizaji na kuimarisha uchumi wa taifa.

“Mbali na hilo, mradi huo unatarajiwa kuvutia zaidi ya viwanda 150, hatua itakayochochea ukuaji wa sekta ya viwanda na kuongeza thamani ya malighafi zinazopatikana nchini,” amesema.

Katika uwekezaji wake, mwekezaji atajenga miundombinu yote muhimu ndani ya kongani hiyo ikiwemo ya barabara, maji, umeme, mifumo ya maji taka, ulinzi na nishati jadidifu ya jua, jambo litakaloweka mazingira bora ya uzalishaji.

Kwa upande wa ajira, zaidi ya nafasi 5,000 za moja kwa moja zinatarajiwa kuzalishwa, sambamba na kutoa fursa za mafunzo ya vitendo kwa vijana wa Kitanzania kupitia chuo maalumu kitakachoanzishwa ndani ya mradi huo.

“Uwekezaji huu unatarajiwa kuingiza zaidi ya dola 3 bilioni  za Marekani katika uchumi wa nchi, kuongeza mapato ya Serikali na kukuza mauzo ya bidhaa nje ya nchi, hatua itakayochangia upatikanaji wa fedha za kigeni,” amesema.

Kampuni hii inasaini mkataba wakati ambao tayari Tiseza imepokea maombi 48 ya wawekezaji wanaotaka kupewa maeneo katika eneo la kimkakati la Bagamoyo Eco Maritime City (BEMC).

“Kati ya maombi hayo, Tiseza imesaini mikataba tisa ya upangishaji wa maeneo ya uwekezaji, na wawekezaji husika tayari wapo katika hatua mbalimbali za kuendeleza maeneo yao,” amesema.

Akizungumzia uwekezaji huo, David Zhou ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa HWTZ SEZ Limited, amesema wanatarajia hadi mwishoni mwa mwaka huu gari la kwanza linalotumia gesi litaanza kutumika.

“Mbali na magari pia tutaanzisha na kuendeleza viwanda vya kutengeneza miundombinu ya chuma. Mradi huu utahusisha ujenzi wa miundombinu yote muhimu kwa ajili ya viwanda,” amesema.

“Tunatarajia kwamba ifikapo mwisho wa mwaka huu, tutaanza uzalishaji wa awali, hususan kwa magari makubwa  ndani ya eneo maalum la kiuchumi,” amesema.

 “Tumeanza tafiti na maandalizi ya kina ili kujenga kongani ya kisasa ya viwanda. Kongani yetu itakuwa tofauti na nyingine kwa kuwa tutatoa miundombinu yote muhimu mapema, pamoja na huduma za Serikali ndani ya eneo hilo,” amesema.

Amesema hiyo itafanya wawekezaji watakaokuja, kuleta tu mitambo yao na kuanza uzalishaji mara moja.

“Vilevile, tutafunga mifumo ya nishati ya jua juu ya paa za viwanda vyote, ambayo itazalisha hadi megawati 45 za umeme kwa ajili ya kuhudumia viwanda vyote ndani ya kongani,” amesema.

Katika uzalishaji, wataanza na kuunganisha pikipiki, boti za uvuvi, pamoja na vifaa vingine, huku wakizingatia matumizi ya nishati safi kadri inavyowezekana.

“Pia tutazalisha malori makubwa hasa kwa matumizi ya migodini na shughuli za ujenzi,” amesema