Na Oscar
Assenga, TANGA
Chama cha
Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kimetoa maelekezo kwa Halmashauri ya Jiji la
Tanga kuhakikisha maeneo ya kukusanyia taka katika soko la Mgandini
yanaboreshwa kwa kujazwa kifusi ikiwemo kurekebisha barabara za ndani ili
kuimarisha usafi.
Agizo
hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajab Abdurhaman wakati wa
ziara yake ambapo alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha maji ya mvua yanaelekezwa
ipasavyo kwenye mifereji ili kuepusha mafuriko na uharibifu wa miundombinu.
Ziara hiyo
ilikuwa ni kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa awali kuhusu kuboresha
usafi wa soko hilo ambapo viongozi wa Jiji hilo walianza kuyafanyia kazi
ikiwemo kuondosha uchafuzi uliokuwepo awali.
Awali,
wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya usafi, Mwenyekiti huyo hakuridhishwa na
mazingira ya soko hilo na kutoa muda wa mwezi mmoja kwa uongozi wa Jiji
kuhakikisha hali ya usafi inaboreshwa.
Akizungumza
baada ya kufanya ziara ya ufuatiliaji, Rajab aliwapongeza Mstahiki Meya pamoja
na viongozi wa Jiji kwa kuchukua hatua na kuanza kutekeleza maelekezo hayo ya
CCM.
“Hatuhitaji
viongozi wa kulalamika, tunahitaji viongozi wanaochukua hatua kutatua changamoto
za wananchi. Mlichokifanya ni kutimiza wajibu wenu,” alisema.
Alisema kuwa
hali ya uchafu iliyokuwepo awali haikuwafurahisha viongozi wala wafanyabiashara,
hivyo hatua zilizochukuliwa zinaonesha uwajibikaji wa uongozi.
Hata
hivyo Mwenyekiti Rajab alisisitiza kuwa atarejea kukagua maendeleo hayo baada
ya wiki mbili na kuonya kuwa hataki kusikia visingizio badala ya utekelezaji.
“Ndani ya
mwezi mmoja kuanzia Aprili 9 hadi Mei 9, tunatarajia kuona kazi imeanza. Hatutaki
hadithi, tunataka vitendo,” alisisitiza.
Aidha,
alieleza kuwa Jiji la Tanga ni taswira ya mkoa huo, hivyo linapaswa kuwa safi
na lenye mpangilio mzuri.
Alikumbusha
kuwa zamani Tanga ilikuwa mji unaojulikana kwa usafi na ustaarabu, hivyo ipo
haja ya kurejesha hali hiyo.
Kuhusu
huduma za vyoo katika soko hilo, Mwenyekiti alieleza kutoridhishwa na hali
iliyopo, akibainisha kuwa choo kilichopo hakitoshelezi mahitaji kutokana na
idadi kubwa ya watumiaji.
Alisema
kuwa hali hiyo inasababisha baadhi ya watu kulazimika kujisaidia katika maeneo
yasiyofaa, jambo linalohatarisha afya za wananchi na wafanyabiashara.
Alisisitiza
umuhimu wa Jiji kutafuta suluhisho la kudumu, ikiwemo kuboresha mfumo wa maji
taka ili kuendana na ongezeko la watumiaji.
Hata
hivyo, aliwapongeza viongozi kwa kuanza mpango wa kujenga choo kipya chenye
matundu 12 kitakachosaidia kupunguza changamoto hiyo, hasa katika kipindi hiki
ambacho soko linatarajiwa kujengwa upya.
Pia
alizungumzia changamoto ya msongamano wa magari yanayoleta bidhaa sokoni hapo,
akielekeza kuwepo kwa utaratibu maalum wa magari kuingia na kushusha mizigo kwa
mpangilio ili kupunguza msongamano na kuboresha usafi.
Alipendekeza
magari yapaki katika maeneo maalum yaliyo nje ya soko, kisha yaingie kwa zamu
kushusha bidhaa.
Katika
hatua nyengine alisisitiza umuhimu wa kujenga mifereji ya maji ili kuzuia maji
ya mvua kutuama au kuingia sokoni, hali inayochangia uchafu na uharibifu wa
mazingira.
Alimalizia
kwa kuwataka viongozi wa Jiji kuwa karibu na wananchi na kushughulikia
changamoto zao kwa vitendo, akibainisha kuwa wananchi hao ndio chanzo cha
mapato ya Jiji kupitia kodi.
Kwa
upande wake, Naibu Meya Khalid Rashid alisema kuwa Jiji lina mpango wa
kuboresha miundombinu ya ndani ya soko, ikiwemo njia za kupita ili kuondoa
changamoto ya matope wakati wa mvua. Alibainisha kuwa kazi hiyo inatarajiwa
kuanza ndani ya wiki moja.
Mwisho.