Sheria Mpya Marekani: Vijana Kuingizwa Jeshini Moja kwa Moja Bila Kujisajili

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth.

Serikali ya Marekani inapanga kuanza mfumo mpya wa kuwasajili moja kwa moja wanaume wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 25 kwenye orodha ya wanaoweza kuitwa jeshini, hatua inayozua mjadala mkubwa ndani na nje ya nchi hiyo.

Mpango huo umependekezwa na taasisi ya Selective Service System, ambayo inahusika na kuhifadhi taarifa za vijana wanaoweza kuitwa kwa huduma ya kijeshi endapo kutatokea dharura ya kitaifa.

Kwa sasa, wanaume wengi nchini humo wanatakiwa kujisajili wenyewe, lakini mabadiliko hayo mapya yataifanya serikali kuwajumuisha moja kwa moja kupitia mifumo ya taarifa za kitaifa. Hatua hiyo inatarajiwa kuanza kutumika mwezi Desemba mwaka huu endapo itapitishwa rasmi.

Mabadiliko haya yameidhinishwa kama sehemu ya sheria ya bajeti ya ulinzi ya mwaka 2026, yakilenga kurahisisha mchakato wa usajili na kuhakikisha hakuna anayekosa kuingizwa kwenye mfumo huo.

Hata hivyo, hatua hiyo imeibua hofu kwa baadhi ya wananchi, hasa kutokana na hali ya mvutano wa kijeshi unaoendelea kati ya Marekani na Iran. Wapo wanaohofia kuwa mpango huo unaweza kuwa ishara ya kurejea kwa mfumo wa lazima wa kujiunga na jeshi (military draft), ambao ulisitishwa mwaka 1973 baada ya vita vya Vietnam.

Kwa mujibu wa sheria za sasa, kushindwa kujisajili kwenye mfumo huo ni kosa la jinai linaloweza kupelekea faini kubwa au hata kifungo, ingawa utekelezaji wake umekuwa mdogo kwa vitendo.

Kwa upande mwingine, mjadala bado unaendelea kuhusu iwapo wanawake nao watahusishwa katika mfumo huo, jambo ambalo limekuwa likipingwa na kujadiliwa mara kadhaa bila kufikiwa kwa makubaliano.

Wakati huo huo, viongozi wa juu wa serikali, akiwemo Rais Donald Trump, hawajatoa msimamo wa moja kwa moja kuhusu uwezekano wa kurejeshwa kwa ulazima wa kujiunga na jeshi, huku wakisisitiza kuwa maamuzi ya kijeshi hayawezi kuwekwa wazi hadharani kwa sababu za kiusalama.

Mpango huu unaendelea kufuatiliwa kwa karibu, huku wachambuzi wakisema unaweza kuwa na athari kubwa kwa mustakabali wa jeshi la Marekani na usalama wa kimataifa kwa ujumla.