SIMBA imeshindwa kupunguza gepu la pointi dhidi ya vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga, baada ya kubanwa mbavu leo Alhamisi Aprili 9, 2026 na TRA United, mechi ikipigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Sare ambayo Simba imeipata leo, imeifanya Yanga kuzidi kukaa mkao wa kula kileleni ikiwa na pointi 44, ikiwaacha wekundu hao wa Msimbazi kwa tofauti ya pointi nane kwani inazo 36 ikikamata nafasi ya pili. Hii ni sare ya sita kwa Simba katika Ligi Kuu Bara msimu huu, wakati Yanga inazo tano.
Leo Simba ilianza dakika 45 za kipindi cha kwanza ikijaribu kusaka bao la mapema, lakini TRA United ilionekana kuwa bora katika kulinda ikiongozwa na nahodha, Nassry Kombo huku ikitumia idadi kubwa ya viungo, akiwemo Jamali Dulazi, Chanda Chewe na Ally Ng’anzi kudhibiti presha ya mshambulizi ya wekundu hao wa Msimbazi.
Kocha wa TRA United, Etienne Ndayiragije, alionekana kuingia na mpango mzuri ambapo wachezaji wake waliongeza presha ya kutafuta mpira mara tu wanaposogea katika nusu ya pili ya uwanja kwa kutumia muundo ya pembe tatu.
Tofauti na ilivyokuwa katika mechi tano zilizopita za Simba dhidi ya TRA, mechi ya leo vijana wa Steve Barker walishindwa kupata bao katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, TRA United ilikuwa ikiwasubiri na baada ya kunasa mpira ilitumia kasi ya wachezaji wake wa pembeni akiwemo Ramadhan Chobwedo katika mashambulizi ya kustukiza.
Simba ilirejea kipindi cha pili na kujaribu kuifungua ngome za TRA, huku baada ya dakika 14 za kipindi cha pili ikifanya mabadiliko mawili kwa mpigo, ilimtoa kiungo wa kati, Alassane Kante na winga Libasse Guaye huku wakiingia Clatous Chama na Morice Abraham ili kuongeza nguvu katika eneo la mwisho.
Hata hivyo, TRA United iliendelea kucheza kwa nidhamu ya kujilinda huku katika kipindi hicho cha pili ikionekana kuwa na idadi kubwa zaidi ya wachezaji nyuma tofauti na kipindi cha kwanza ambapo ilikuwa na ukuta wa wachezaji wanne, akiwemo Kombo na Mganda, Christopher Tebandeke ambaye alimpa wakati mgumu, Seleman Mwalimu.
Katika maeneo ya pembeni wakifanya vizuri, Issac Mtengwa na Valentino Nouma, tofauti na ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza ambapo viungo wao walisaidia pia katika kushambulia, walionekana kuwa nyuma zaidi na kuifanya Simba kuwa na wakati mgumu zaidi katika utengenezaji wa nafasi.
Dakika ya 77, Simba ilifanya mabadiliko ya tatu katika mchezo huo kwa kumtoa Neo Maema na kuingia Inno Loemba, kisha dakika ya 84 ikafanya mabadiliko mengine kwa kuwatoa Shomary Kapombe na Mwalimu, wakaingia David Kameta ‘Duchu’ na Hussein Mbegu.
TRA United ilijikuta ikimaliza pungufu katika mchezo huo kufuatia Nouma kuonyesha kadi ya pili ya njano dakika ya 88 iliyozaa nyekundu. Kadi ya kwanza alionyeshwa dakika ya 82.
Simba iliingia katika mechi hiyo ikiwa na rekodi ya kuvutia dhidi ya TRA United, maarufu kama wakusanya kodi, baada ya kushinda michezo mitano mfululizo bila kuruhusu bao lolote tangu Februari 6, 2024.
Katika historia ya michezo yao, Simba ilianza kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya wapinzani wao hao ambao wakati huo walijulikana kama Tabora United.
Walipokutana tena katika mchezo wa marudiano Mei 6, 2024 jijini Dar es Salaam, Simba iliendeleza ubabe wake kwa kushinda mabao 2-0.
Mfululizo huo uliendelea ambapo katika michezo mitatu iliyofuata, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 ambapo ni Agosti 18, 2024, Februari 2, 2025 na Machi 22, 2026.
Kwa ujumla, Simba imekuwa na rekodi ya kutokosa pointi tatu katika michezo hiyo yote mitano huku ikifunga jumla ya mabao 15 bila ya kuruhusu bao, sawa na wastani wa mabao matatu kwa kila mechi. Cha kuvutia zaidi ni kwamba katika kila ushindi wa mechi hizo, Simba ilipata bao kipindi cha kwanza, tofauti na ilivyokuwa katika mchezo wa leo ambapo walienda mapumziko ubao ukisoma 0-0.