Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeelezea mafanikio yake katika maendeleo ya miji na sekta ya makazi wakati wa Kongamano la Pili la Miji Africa (2nd African Urban Forum) linalofanyika jijini Nairobi, huku ikitoa wito kwa wawekezaji wa ndani na kimataifa kuchangamkia fursa zilizopo nchini humo.
Amesema, Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Africa, hasa katika maeneo ya miundombinu, upatikanaji wa nishati, utoaji wa huduma za kijamii na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
‘’Juhudi hizo zinaendana na mkakati wa Bara la Africa wa kuimarisha muunganiko, biashara na maendeleo jumuishi’’. amesema
Aidha, Mhe. Dkt Akwilapo alielezea pia mikakati ya serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto za ukuaji wa kasi wa miji pamoja na upungufu wa makazi, ambapo kwa sasa makazi yasiyo rasmi yanakadiriwa kufikia asilimia 67.3.
Amesema, katika kukabiliana na hali hiyo, serikali ya Tanzania inaendelea kutekeleza mageuzi ya sera, kuanzisha mifumo bunifu ya fedha, kuboresha umiliki wa ardhi pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika makazi nafuu kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.
Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesisitiza kuwa, serikali ya Tanzania itaendelea kutumia rasilimali zake za asili pamoja na kudumisha amani na usalama ili kuharakisha utekelezaji wa Ajenda 2063.
Kupitia Kongamano hilo, Dkt Akwilapo alieleza salamu za dhati kutoka kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyempongeza Mhe. William Ruto pamoja na wananchi wa Jamhuri ya Kenya kwa kuandaa Kongamano hilo muhimu.
Kongamano la Pili la Miji Africa limezinduliwa rasmi April 9, 2026 na Rais wa Kenya Mhe. William Ruto na linaongozwa na kauli mbiu isemayo “Adequate Housing for All: Advancing Socio-Economic and Environmental Transformation Towards the Realization of Agenda 2063,” ikilenga kuhamasisha mijadala inayotoa fursa kwa washiriki kutoka nchi mbalimbali za Africa kubadilishana uzoefu na suluhisho bunifu katika kukabiliana na changamoto za maendeleo ya miji na makazi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akisoma tamko la Tanzania katika Kongamano la Pili la Miji Africa (2nd African Urban Forum) linalofanyika jijini Nairobi nchini Kenya.

Ujumbe wa Tanzania ukiwa katika Kongamano la Pili la Miji Africa (2nd African Urban Forum) linalofanyika jijini Nairobi nchini Kenya.

Sehemu ya washiriki wa Kongamano la Pili la Miji Africa (2nd African Urban Forum) wakiwa katika kongamano hilo linalofanyika jijini Nairobi nchini Kenya. ( PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)