Dodoma. Mbunge wa Kisarawe (CCM), Dk Seleman Jafo ameapa kupeleka hoja binafsi bungeni kwa ajili ya kusaidia ajira za muda kwa vijana.
Hata hivyo, Dk Jafo ametaja kuwa ajira hizo zinapaswa kwenda moja kwa moja kwa madereva bodaboda na bajaji ambao ni wasomi wa viwango vya kuanzia stashahada.
Waziri huyo wa zamani katika wizara kadhaa, ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 9,2026 wakati akichangia kwenye Hotuba ya Makadirio ya Mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2026/27.
Jafo amesema hali ilivyo hakuna namna ni lazima apeleke hoja binafsi bungeni ili kusaidia ajira za vijana nchini ambako amesema kumekuwa na changamoto kubwa.
“Nitaomba wabunge mniunge mkono katika jambo hili, lazima tuje na mkakati wa kuwapa walau ajira za mkataba wa miaka mitatu, watu wa diploma (stashahada) tuwalipe Sh500,000 kwa mwezi lakini kwenye digrii (shahada) walipwe Sh700,000,” amesema Jafo.
Amefafanua kuwa jambo hilo linawezekana kwa kuwa uwezo wa kiuchumi kwa Taifa upo isipokuwa nia pekee ndiyo inatakiwa.
Amesema Mpango huo hautakiwi hata kuwa katika utaratibu wa Wizara ya Utumishi ambako kunakuwa na masharti magumu ya upatikanaji wa ajira.
Kuhusu sababu za kwa nini wapate ajira waendesha bodaboda na bajaji, amesema hao ni vijana ambao tayari wameonyesha uthubutu kwenye kazi hivyo wakipatiwa ajira watafanya kazi kwa moyo na uzalendo wa hali ya juu.
Juzi Mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafuwe alitaka Serikali kusajili makundi ya bodaboda na bajaji kwa viwango vya elimu zao ili zinapotokea fursa za ajira wapewe kipaumbele.
Hoja ya Mafuwe inalingana na Jafo kwani wote wanadai walio kwenye uendeshaji wa vyombo hivyo ni watu ambao tayari wameonyesha nia ya kujitegemea na uwezo wa kazi kama watapatiwa nafasi.
