Polisi yathibitisha kumkamata Pauline Pallangyo

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limesema baadhi ya taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu kukamatwa kwa Pauline Pallangyo zimekuwa za kupotosha umma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, Aprili 9, 2026, Polisi imeeleza Pallangyo, mkazi wa Dar es Salaam, alikamatwa jana Jumatano saa moja usiku na anaendelea kushikiliwa kutokana na tuhuma za jinai zinazomkabili.

Taarifa hiyo imefafanua hatua ya kumkamata ilifuatia kukamilika kwa ushahidi uliokuwa unakusanywa kabla ya kukamatwa kwake, na kwamba kwa sasa anashikiliwa kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

“Kupitia mitandao ya kijamii kuna taarifa za kutaka kuupotosha umma zinazoaambazwa kumhusu Pauline Pallangyo, Mkazi wa Dar es Salaam.

Taarifa sahihi ni kwamba, Aprili 8, 2026 saa moja usiku, alikamatwa na askari polisi kutokana na tuhuma za jinai zinazomkabili na anaendelea kushikiliwa ili kukamilisha ushahidi uliokwishaanza kukusanywa kabla ya kukamatwa kwake,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Polisi imeonya kuwa kuna watu wanaoendelea kuandaa na kusambaza taarifa za kupotosha kuhusu tukio hilo, na kusisitiza hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhusika.

Sambamba na hilo, Jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi kuendelea kuzipuuza taarifa za uzushi, upotoshaji na zile zinazolenga kuchochea taharuki, zikielezwa hazina uthibitisho.

“Jeshi la Polisi la Mkoa wa Dodoma linatoa onyo kwa baadhi ya watu wanaoendekeza tabia ya kuandaa na kusambaza taarifa za kupotosha wananchi, kwani halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.”

Hata hivyo, wakati Polisi ikitoa ufafanuzi huo, familia ya Pallangyo imeeleza mazingira ya tukio hilo kwa mtazamo wao, ikidai kuwa watu waliojitambulisha kama askari polisi walifika nyumbani kwake wakiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser na kumchukua bila kutoa maelezo ya kina kuhusu kosa lake.

Wameeleza licha ya kufika Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma (Central) jitihada za kumuona hazikufanikiwa mara moja, hali iliyozua maswali zaidi juu ya mchakato wa kukamatwa kwake na mawasiliano kati ya mamlaka na familia.

Pia, wameeleza kuwa wakati wa tukio hilo, kulikuwa na shinikizo la kutaka atoe neno la siri la simu yake, jambo ambalo alikataa kufanya.

Tukio hilo limeibua mjadala mpana mitandaoni, hasa kutokana na historia ya Pallangyo kutajwa miongoni mwa vijana waliowahi kukamatwa Oktoba 29 kwa tuhuma za uhaini kabla ya baadaye kuachiwa huru baada ya mashtaka kufutwa.