ZIMEPITA takribani siku 16 tangu Yanga ilipoamua kumrudisha Abdihamid Moallin katika benchi la ufundi la timu hiyo kusaidiana na Kocha Mkuu, Pedro Goncavles huku maajabu yakionekana kwa haraka sana.
Uamuzi wa Yanga kutangaza kumrudisha Moallin ulifanyika Machi 23, 2026 baada ya kikao cha viongozi wa klabu hiyo na benchi la ufundi linaloongozwa na Pedro na taarifa ilisema uongozi umegundua kuna changamoto ya kiufundi inayofanya timu icheze aina tofauti na ile ambayo imezoeleka na kuendana na wachezaji walio ndani ya kikosi hicho.
Tangu Moallin arudishwe klabuni hapo na amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Ufundi, kisha Kocha Msaidizi msimu uliopita 2024-2025 chini ya Kocha Sead Ramovic na Miloud Hamdi, Yanga imekuwa na mabadiliko ya haraka ya kiuchezaji na kupata matokeo mazuri.
Moallin aliyekuwepo msimu uliopita wakati Yanga ikibeba Kombe la Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB na Kombe la Muungano 2025 na kuondoka mwisho wa msimu huo, uwepo wake katika benchi la ufundi la timu hiyo hivi sasa kwa namna moja ama nyingine umeleta matokeo chanya mapema zaidi na timu hiyo imeshinda mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara kwa matokeo yanayofanana mabao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons (nyumbani) na Pamba Jiji (ugenini).
Kabla ya kikao hicho cha viongozi na Pedro kufanyika, Yanga ilitoka kupata sare tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam (0-0), TRA United (0-0) na Mtibwa Sugar (1-1), matokeo yaliyohatarisha mbio zao za kuwania ubingwa, hata hivyo iliendelea kukaa kileleni mwa msimamo ikiwa haijapoteza hadi sasa.
Tathmini ya vigogo wa Yanga na Pedro baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, ilibainisha mambo makuu mawili nje ya ile ya kiufundi ambayo ni ratiba na majeruhi ikitajwa ni sehemu ya yaliyochangia kutopata matokeo mazuri kwa baadhi ya mechi.
Hata hivyo licha ya awali kuwepo majeruhi ambao ni Clement Mzize, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Chadrack Boka, Prince Dube, Laurindo Maria ‘Depu’, Khomein Aboubakar na Edmund John ikielezwa wimbi hilo la majeruhi limechangia matokeo yasiyo mazuri, hivi sasa amerejea Bacca pekee ambaye anacheza, huku timu ikishinda mechi hizo mbili.
Miongoni mwa mabadiliko ambayo yanaonekana ndani ya Yanga hivi sasa, ni kitendo cha Allan Okello kuchezeshwa namba 10 tofauti na awali alipokuwa anashambulia kutokea pembeni eneo la winga.
Okello aliyetua Yanga dirisha dogo la Januari 2026 akitokea Vipers ya Uganda, hadi sasa amehusika na mabao sita akifunga mawili na asisti nne, kati ya hizo alitoa tatu dhidi ya Pamba Jiji katika ushindi wa 3-0.
Mbali na hilo, uchezaji wa Yanga umebadilika pia ambapo hivi sasa inapowakosa washambuliaji wake wawili kinara, Depu na Dube, viungo wanafanya kazi kubwa ya kufunga mabao.
Katika mechi hizo mbili ambazo Yanga imevuna mabao sita, yote yamefungwa na viungo Mudathir Yahya aliyefunga matatu, Allan Okello, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli kila mmoja bao moja.
Siku chache baada ya kurudi Yanga, Moallin amesema: “Mimi sitaki kuongea sana, unajua hii Yanga ni timu kubwa hapa Tanzania na Afrika, uwepo wetu hapa tunatakiwa kushirikiana kusimamisha matokeo ya kuangusha pointi, hiki siyo ambacho mashabiki wanakitaka wala kukivumilia.
“Nilikuwa hapa asilimia kubwa ya wachezaji nawajua vizuri, nitakuwa msaidizi wa kocha mkuu kushauriana namna gani ya kuwaimarisha zaidi wachezaji ili waweze kurudi kwenye kushinda mechi.
“Bahati nzuri sana timu haijapoteza mchezo wowote kitu ambacho kinaleta presha ni matokeo ya sare, hili tunatakiwa kuunganisha nguvu kuliondoa na timu iweze kuwa na matokeo ambayo yatarudisha imani kwenda kutetea ubingwa wetu.”
Aidha Moalin aliongeza: “Kila mchezaji ambaye alikuwa bora msimu uliopita bado yupo hapa, tatizo ni baadhi ya wachezaji kuwa majeruhi, nadhani ni suala la muda wakipona timu itarudi njia yake ya kuendelea kushinda.”
Jumamosi hii, Yanga itaikaribisha TMA katika mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB ikiwa ni ya tatu ya mashindano tangu Moallin arejee kikosini hapo.
