TAARIFA zinasema Simba hivi sasa inajiandaa kuyaanza maisha ya msimu ujao wa 2026-2027 bila ya kipa wake wa sasa, Djibrilla Kassali, huku ikienda Nigeria kuzungumza na nyanda mmoja wa maana.
Kama mazungumzo yatakwenda sawa kati ya Simba na kipa namba moja wa timu ya taifa ya Nigeria, Stanley Nwabali, huenda msimu ujao wa 2026-2027 akatua viunga vya Msimbazi.
Ishu kubwa iliyopo hadi sasa ni suala la gharama, baada ya vigogo wa Simba kukaa na kipa huyo aliyezaliwa Juni 10, 1996 huko Lagos nchini Nigeria kuwaambia mambo anayohitaji ili ajiunge nao.
Baada ya Nwabali kuachana na Chippa United ya Afrika Kusini, hana timu tangu Februari 1, 2026 jambo ambalo vigogo wa Msimbazi kuona kama kungekuwa na urahisi wa kumpata, lakini wakakutana na ongezeko la gharama.
Mwanaspoti liliwasiliana na mtu wa karibu na kipa huyo ambapo amesema baada ya Simba kuhitaji huduma yake, mahitaji aliyoyataka Nwabali ni mshahara wa Dola 15,000 (Sh38.9 milioni) kwa mwezi ambao ni ongezeko la asilimia 25 ya aliokuwa anaupata akiwa na Chippa United.
“Akiwa Chippa United alikuwa anapokea mshahara wa Dola 12,000 (Sh31.1 milioni), lakini anahitaji pesa ndefu zaidi kutoka klabu ya Simba ambayo imewahi kumfuata mwanzo, hii ni mara ya pili,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Simba baada ya kuambiwa hilo, iliomba kupewa muda wa kujadiliana, hivyo endapo kama kila kitu kitakwenda sawa huenda akajiunga nao, ikishindikana basi ifahamike ni suala la gharama kuwa kubwa.”
Kabla ya kuachana na Chippa United, kipa huyo msimu huu alicheza jumla ya mechi 12, ambapo 11 za Ligi Kuu ya Afrika Kusini akiruhusu mabao 16, huku akiambulia clean sheet tatu. Pia mechi moja ya Kombe la Carling Knockout.
Akiwa na timu ya taifa la Nigeria, Nwabali, ameonyesha uzoefu mkubwa katika mechi za kimataifa akicheza jumla ya mechi 34, hajaruhusu bao katika mechi sita huku akiruhusu mabao 29 katika dakika 3,125.
Wastani wa mabao anayoruhusu uko chini ya bao moja kwa kila mechi (takriban 0.85), hali inayomweka katika kiwango kizuri ukilinganisha na makipa wengi wa kimataifa. Clean sheets ni sita kati ya mechi 34.
Makipa waliopo Simba ni Yakoub Suleiman anayeuguza majeraha na sasa anafanya mazoezi ya gym chini ya daktari akitarajiwa kurudi uwanjani.
Wakati Yakouba akiwa anauguza majeraha, Hussein Abel hana nafasi kubwa ya kucheza mbele ya Djibrilla Kassali aliyechukua mikoba ya Moussa Camara aliyewekwa nje ya mfumo wa usajili baada ya kupata mejeraha mwanzoni mwa msimu huu.
Chanzo kutoka Simba kilisema: “Simba inahitaji kipa wa viwango vya juu zaidi, kutokana na mchakato wa kurejesha ushindani wa kufanya vizuri kimataifa na ligi ya ndani kuchukua mataji pamoja na hilo kunaangaliwa uwezekano wa hao wanaozungumza nao.”
Kassali ametua Simba dirisha dogo la usajili Januari 2026 ambapo kwa mujibu wa taarifa za ndani ya klabu hiyo, alipewa mkataba mfupi hadi mwisho wa msimu huu ikiwa ni sehemu ya kumuangalia kiwango chake.
Kipa huyo kwa sasa ndiye namba moja kikosini hapo huku akionekana kuwa na makosa kadhaa ya kiuchezaji uwanjani ikitajwa hayupo vizuri katika kutumia miguu yake kulinganisha na aliyemrithi, Moussa Camara.
Wakati huohuo, taarifa zinasema muda wowote Simba itatoa taarifa za kuvunjika mkataba wa mshambuliaji Jonathan Sowah aliyebakisha takribani miezi miwili kumalizika mwisho wa msimu huu.
Kulikuwa na tetesi za Simba kutaka kuachana na Sowah mwishoni mwa msimu huu, sababu kubwa ikitajwa ni utovu wa nidhamu na kabla ya kufanya hivyo, mshambuliaji huyo alisimamishwa na kutakiwa ajibu mambo kadhaa ya utovu wa nidhamu na hata alipofanya hivyo, bado hakurudishwa kikosini.
Mwanaspoti limepenyezewa Sowah ndiye amefikia uamuzi wa kuvunja mkataba na Simba kutokana na kuchoka kukaa muda mrefu bila kucheza mechi.
Kigogo mmoja (jina linahifadhiwa) alipoulizwa kuhusu hilo amesema: “Ndiyo mkataba umevunjika, lakini sikutakiwa hata kukujibu na siwezi kwenda mbali zaidi ya hilo, maana mkataba ni siri ya klabu na mchezaji.”
Sowah aliyezaliwa Januari Mosi, 1999 Ghana, alijiunga na Simba dirisha kubwa la usajili mwanzoni mwa msimu huu 2025-2026 akitokea Singida Black Stars aliyoitumikia kwa takribani miezi sita msimu uliopita.
Mghana huyo akiwa Singida BS alipoingia dirisha dogo msimu uliopita akicheza nusu msimu, alimaliza na mabao 13 katika Ligi Kuu Bara.
Kabla ya Sowah kusimamishwa na Simba, mshambuliaji huyo Desemba 16, 2025 alikumbana na adhabu kutoka Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) alipofungiwa mechi tano kutokana na makosa ya nidhamu yaliyofanyika Desemba 7, 2025 katika mechi ya Ligi dhidi ya Azam.
Wakati adhabu hiyo ya mechi tano ikimalizika, ndipo akasimamishwa na Simba, hivyo hajacheza mechi ya ligi tangu Desemba 7, 2025 dhidi ya Azam. Hata hivyo, alishiriki Kombe la Mapinduzi 2026 na Simba iliishia nusu fainali.
