Mshery majanga Yanga, awekwa chini ya uangalizi

KAMA uliangalia mechi ya Pamba Jiji dhidi ya Yanga juzi Jumatano, najua utajiuliza maswali kwa sababu hukumuona kipa Aboutwalib Mshery, taarifa zinasema ameumia goti, hivyo yupo katika uangalizi wa madaktari kufahamu majeraha hayo yana ukubwa kiasi gani.

Kuumia kwa Mshery, kulimpa nafasi Hussein Masalanga kudaka mechi hiyo iliyomalizika kwa Yanga kushinda 3-0, huku kipa wa akiba akiwa Joseph Semsey kutoka timu ya vijana.Taarifa kutoka Yanga zinabainisha, Mshery aliumia goti wakati wa maandalizi ya mechi dhidi ya Pamba Jiji, hivyo ikatoa nafasi kwa Masalanga kudaka kwa mara ya kwanza kwenye ligi tangu ajiunge na kikosi hicho kipindi cha usajili wa dirisha dogo la Januari 2026 akitokea Singida Black Stars.

“Mshery hakuonekana kwenye mchezo dhidi ya Pamba baada ya kuumia goti kwenye mazoezi yetu ya mwisho, ndiyo maana alidaka Masalanga.

“Tunarudi naye Dar es Salaam wakati madaktari wakifuatilia maendeleo yake na atafanyiwa vipimo zaidi ili kujua ukubwa wa jeraha lake, kwa hiyo tutawajulisha majibu ya madaktari,” amesema bosi mmoja wa Yanga.

Yanga kesho Jumamosi itacheza mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya TMA ikiwa ni hatua ya 16 bora na Masalanga anatarajiwa kuendelea kukaa langoni, huku mbadala wake akiwa Semsey.

Ikumbukwe, kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra ataukosa mchezo huo akiwa anamalizia adhabu yake ya kusimamishwa mechi tatu aliyopewa na Kamati ya Usimamizi ya Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kufuatia kumfanyia vurugu mwamuzi. Tayari amekosa mechi mbili dhidi ya Tanzania Prisons na Pamba Jiji na zote Yanga imeshinda mabao 3-0.

Kwa upande wa makipa, Mshery anaungana na Khomein Abubakar ambaye ni majeruhi wa muda mrefu anayetarajiwa kurudi uwanjani msimu ujao.