CRDB FA Cup: JKT, Mbuni, Geita Gold na Mashujaa kazini leo

KUNA mechi mbili za Kombe la Shirikisho la CRDB (FA) hatua ya 16 bora zinachezwa leo Ijumaa ambapo JKT Tanzania itaikaribisha Mbuni kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar, wakati Geita Gold ni mwenyeji wa Mashujaa, ikipigwa Uwanja wa Shule ya Wasichana Nyankumbu mkoani Geita. Zote zitaanza saa 10:00 jioni.

Kocha wa Mashujaa, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amesema mchezo dhidi ya Geita Gold utakuwa vita ya watu wazima kulingana na ushindani uliopo baina ya timu hizo pindi zinapokutana.

Julio amesema anatambua ugumu wa mchezo huo kutokana na uwezo mkubwa wa Zuberi Katwila ambaye ni kocha wa Geita Gold, huku pia akimtaja kuwa miongoni mwa walimu wa soka wenye uzoefu katika kuziongoza timu za Ligi ya Championship.

“Ukiangalia Geita Gold kwenye Championship, ukikutana nayo utakuja kufedheheka mtu mzima, kwahiyo tunaingia kucheza na watu wazima wenzetu ambao walikuwa kwenye Ligi Kuu, sio mechi ya kitoto lakini tumejipanga kupambana kama ambavyo wenzetu wamejipanga ili mwenye bahati na aliyejipanga vizuri aweze kusonga mbele,” amesema Julio.

Julio alikiri mashindano hayo kuwa magumu, hata hivyo amesema kikosi chake kimejipanga kupata ushindi kwani ndoto yao ni kucheza kimataifa msimu ujao huku upande wa Ligi Kuu wakijipanga kumaliza nafasi nne za juu wakitaka kutoka nafasi ya 11 walipo sasa na alama 20.

Kwa upande wake Kocha wa Geita Gold, Zuberi Katwila, alibainisha kuwa kulingana na uzito wa ushindani walionao kwenye Ligi ya Championship katika kupanda ligi kuu pamoja na mashindano hayo ya FA, wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi huku akitarajia kuwatumia wachezaji ambao hawapati nafasi kubwa ya kucheza.

Katwila amesema wachezaji waliokuwa hawapati nafasi anawaamini kwani ndiyo walioifikisha timu katika hatua ya 16 bora, hivyo matumaini yake ni kuona wanafika hatua ya nane bora.

“Ni ‘rotation’ ambayo tulikuwa tunaifanya toka awali, wanaocheza Championship ni wengine na watakaocheza FA ni wengine, mechi zetu zote za FA wanatumika hao ambao ni wachezaji wetu lakini katika Championship wanakuwa kidogo wanakosa nafasi, hii ni mtoano ambayo lazima utumie wachezaji ambao watakuwa na nguvu ya kutosha kupambana na mchezo,” amesema Katwila.

Mashabiki ambao watafika uwanjani kushuhudia mechi hiyo, wamepewa urahisi kwani Mlezi wa Geita Gold ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi, amelipia tiketi zote hali inayofanya kuingia bure.