Kigali. Wanyarwanda waliohudhuria kumbukizi ya mauaji ya Kimbari nchini Rwanda wameonyesha mitazamo yao wakitamani historia hiyo ifundishwe darasana kutokana na kubeba mafunzo mengi.
Kijana Yusufu Bhangula (25) amesema umefika wakati kwa Serikali ya Rwanda kuanza kufikiria namna ya kujumuisha historia ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 katika mitaala ya shule, kwa lengo la kuelimisha vizazi vijavyo na kuzuia kurudiwa kwa matukio kama hayo.
Bhangula ameyasema hayo alipofanya mahojiano na Mwananchi jana jioni katika viwanja vya Nyanza Kicukiro Memorial.
Maelfu ya vijana walikusanyika kwa ajili ya kumbukizi ya mauaji hayo ya kimbari yaliyotokea Aprili 7, 1994 nchini humo na kuua watu zaidi ya milioni moja.
Yusufu Bhangula (25)
Huo ni mwendelezo wa maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji hayo yaliyopewa jina la Kwibuka 32, yatakayodumu kwa siku 100.
Bhangula amesema kuwa kufanya hivyo kutasaidia vijana kuelewa historia ya nchi yao na kujifunza namna ya kuepuka migogoro badala ya kuichochea.
Pia, amesema maadhimisho ya kumbukumbu hiyo huwapatia fursa ya kutafakari yaliyopita na kujifunza kwa kina kuhusu historia ya Rwanda na mabadiliko yaliyofuata baada ya tukio hilo.
“Siku kama hii inatukumbusha mambo mengi na kutufundisha kuhusu tulipotoka kama taifa na tulipo sasa, pamoja na wajibu wetu kama vijana kuhakikisha historia kama hiyo haijirudii,” amesema kijana huyo.
Kwa mujibu wa Bhangula, historia inaonyesha vijana wengi walitumika kuchochea na kuendesha mauaji hayo, hivyo ni jukumu la kizazi cha sasa kupinga na kupambana na fikra zozote zinazoweza kurejesha mgawanyiko.
“Tunaambiwa mauaji yale yaliwekewa nguvu na vijana. Hivyo sisi kama vijana tuna wajibu wa kupambana na wanaopinga ukweli huu na kuonyesha madhara yaliyotupata kama taifa,” amesema.
Amesema juhudi zinazofanywa na Serikali ya Rwanda katika kuwawezesha vijana ni muhimu, kwa sababu zitawawezesha kuwa walinzi wa amani kwa vizazi vijavyo.
Bhangula amesema maadhimisho hayo pia hutoa taswira halisi ya ukatili uliotokea, akieleza kuwa kushuhudia mabaki ya miili ya waathirika kunawasaidia kuelewa ukubwa wa tukio hilo.
“Tunapoona hali halisi, tunapata picha kamili ya kilichotokea na inatufanya tuchukue hatua za kuhakikisha hakijirudii,” amesema.
Bhangula amesisitiza kuwa vijana wa Rwanda hawatamani kuona matukio kama hayo yakijirudia tena, iwe nchini mwao au sehemu nyingine yoyote duniani.
Aidha, amependekeza historia ya mauaji ya kimbari ifundishwe si tu Rwanda bali pia katika nchi nyingine, hususan barani Afrika, ili kuwajengea vijana uelewa wa kulinda amani na mshikamano.
“Badala ya kufundishwa mambo yasiyo na tija, vijana wanapaswa kufundishwa historia yenye mafunzo. Hii itawasaidia kulinda nchi zao na kuepuka kurubuniwa na watu wachache wasiozitakia mema,” amesema.
Wakati huohuo, manusura wanaoishi ughaibuni wameieleza Mwananchi kwamba maadhimisho ya Kwibuka 32 si tukio la kukumbuka tu, bali ni wajibu mkubwa walio nao Wanyarwanda na serikali yao wa kuhifadhi ukweli, kupinga upotoshaji wa historia unaotaka kushika kasi mitandaoni na katika nyaraka mbalimbali zinazojaribu kuhifadhi taarifa.
Kupitia simulizi zao kutoka sehemu mbalimbali duniani, manusura hao wanaakisi dhamira ya pamoja ya kukumbuka, kuelimisha na kupinga upotoshaji huo wa historia.
Akizungumza na Mwananchi katika maadhimisho hayo, manusura aliyejitambulisha kwa jina la Samson Nyagatare anayeishi Poland anasema Kwibuka hubeba maana pana zaidi ya kumbukumbu.
“Ni wakati wa kuwakumbuka tuliowapoteza na kusema ukweli kuhusu Mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi, hasa kwa wale ambao hawajawahi kukutana na manusura,” anasema.
Kwa mujibu wa Nyagatare, kuishi ughaibuni hakumwondolei wajibu wake kwa historia ya nchi yake.
“Kuishi mbali na nyumbani kunamaanisha kubaki na uhusiano na historia, utambulisho na nchi yangu, huku pia nikiwa shahidi na mwelimishaji. Ni wajibu wangu kueleza yaliyotokea na kuonyesha namna Rwanda ilivyojijenga upya,” amesema.
Manusura huyo anasisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha ukweli haulindwi tu, bali pia haupotoshwi, hususan kwa kizazi hiki cha vijana wa sasa.
Kwa upande wake, Dimitrie Mukanyiligira anayeishi Austria anasema bado kuna changamoto ya uwepo wa itikadi ya mauaji ya kimbari na ukanushaji wake katika baadhi ya maeneo, hali inayowalazimu Wanyarwanda kwa ujumla wao kusimama imara kupinga upotoshaji huo wa taarifa.
“Ni lazima kusema ukweli, kupinga taarifa potofu katika jamii zetu na mitandaoni, na kusimama dhidi ya kutovumiliana,” anasisitiza.
