Walioghushi kadi za benki kuiba Sh147 bilioni wakamatwa

Dar es Salaam. Mamlaka zimeanza uchunguzi wa tuhuma za utapeli wa Sh147.5 bilioni, zilizotolewa katika akaunti za benki za wateja mbalimbali, bila ridhaa zao.

Fedha hizo, zilitolewa katika akaunti za wateja hao, baada ya kadi zao za benki kughushiwa na yakafanywa malipo ya kodi, huduma, usafirishaji na bima ya afya, bila wenyewe kujua.

Tuhuma hizo, ziliibuliwa Machi 30, 2026 katika taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ya mwaka wa fedha 2024/25, Chrispin Chalamila aliyoiwasilishwa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika taarifa yake hiyo, Chalamila alisema Sh147.5 bilioni zilitolewa katika akaunti za benki za wateja mbalimbali nchini pasi na ridhaa yao.

Uchunguzi huo, alisema umebaini fedha ilitolewa kupitia malipo ya huduma na bidhaa kwa kutumia kadi 1,551 za wateja wa mataifa 11 kupitia kampuni 162 na benki tano za Tanzania.

“Kadi zilizoghushiwa zilitumika kufanya malipo mbalimbali ya huduma za utalii, usafirishaji, malipo ya kodi na bima ya afya. Watuhumiwa walifanya utakatishaji wa fedha na kusababisha hasara ya Sh2.6 bilioni kwa baadhi ya benki,” alisema.

Alisema kampuni 82 za utalii zilizopo Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza, zilitumia kadi hizo zilizogushiwa kinyume na Sheria ya Kanuni za Adhabu.

Katika uchunguzi huo, alisema hadi kufikia Juni 2025, Sh678 milioni ziliokolewa na kurejeshwa benki.

Ukubwa wa tukio hilo umeibua wasiwasi wa wadau kuhusu udhaifu wa mifumo ya usalama wa kadi za benki na udhibiti wa ndani katika taasisi hizo.

Akizungumzia ripoti hiyo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema mamlaka zimeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo na kwamba hatua za udhibiti zimeimarishwa katika sekta ya fedha ili kuzuia matukio kama hayo kujirudia.

Amesema watuhumiwa wanaoaminika kuwa raia wa kigeni walitumia teknolojia ya kisasa kunakili kadi za benki na kuiba fedha kutoka kwa wateja bila wao kujua.

Kwa mujibu wa Tutuba, Takukuru tayari imewakamata watuhumiwa kadhaa na kesi zimeanza kusikilizwa mahakamani, huku watuhumiwa hao wakiamriwa kurejesha fedha zilizoibwa.

“Watu hawa walitumia teknolojia ya hali ya juu kunakili kadi za benki na kuiba fedha kutoka kwa wamiliki halali wa akaunti. Uchunguzi unaendelea, mifumo ya udhibiti imeimarishwa, na tayari baadhi ya watuhumiwa wamekamatwa, kesi ziko mahakamani na juhudi za kurejesha fedha zinaendelea,” amesema Tutuba.

Hata hivyo, hakubainisha kiasi halisi cha fedha kinachotarajiwa kurejeshwa wala idadi ya watuhumiwa waliokamatwa na kufikishwa mahakamani hadi sasa.

Wakati uchunguzi ukiendelea, Mhadhiri Mwandamizi wa Fedha na Benki katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Tobias Swai, amesema tukio hilo linaonesha umuhimu wa kuimarisha elimu ya fedha kwa watumiaji, hasa katika kufuatilia miamala ya akaunti na kubaini shughuli zisizo za kawaida.

“Wateja wengi bado hawana uelewa wa kutosha wa kubaini miamala isiyo ya kawaida au kuchukua hatua kwa haraka pale wanapogundua tofauti,” amesema.

Amesisitiza wateja wana haki ya kuhoji makato yasiyoeleweka, pia wanapaswa kukagua taarifa za akaunti zao mara kwa mara na kulinda taarifa zao za kifedha.

Dk Swai pia, ameitaka BoT kuimarisha usimamizi wake kwa kuhakikisha benki zinazingatia viwango vya juu vya kiutendaji na usalama na kuwawajibisha viongozi wa taasisi husika pale udhaifu unapobainika.

Aidha, amewahimiza wateja kutumia mifumo ya kushughulikia malalamiko na mifumo ya ulinzi wa mlaji, huku akiwashauri kuepuka taasisi zisizokidhi viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka, amesema matukio ya wizi na udanganyifu yanaathiri taswira ya taasisi za kifedha, hasa katika sekta inayotegemea sana imani ya wateja.

Amebainisha wateja wengi hushindwa kufuatilia akaunti zao mara kwa mara, jambo linalowaweka katika hatari ya kupoteza fedha.

“Hili ni muhimu zaidi kwa wateja wenye fedha nyingi, ambao wanaweza kupata hasara kubwa endapo mifumo haitakuwa salama,” amesema.

Dk Mwinuka amesisitiza umuhimu wa matumizi mapana ya mifumo imara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kuboresha usalama na kubaini vitendo vya udanganyifu kwa ufanisi zaidi.

Ameitaka BoT kuongeza usimamizi na kuhakikisha taasisi zote zinazingatia masharti ya kisheria.

Ameongeza baadhi ya taasisi bado zinategemea mifumo ya ndani ambayo inaweza isiwe imara kukabiliana na hatari mpya, hivyo kuna haja ya kuboresha mifumo na udhibiti wa ndani.

“Imani katika sekta ya benki lazima ianze ndani ya taasisi zenyewe kwa kuhakikisha taratibu na mifumo inalinda haki za wateja,” amesema.