Dawa ya kuepuka miguu yako kunuka

Russia.Tatizo la harufu mbaya ya miguu kitaalamu huitwa Bromodosis. Ni hali inayoweza kumletea mwathirika usumbufu mkubwa na hata kusababisha ajitenge au kutengwa na watu wanaomzunguka kutokana na kero ya harufu.

Kwa kawaida, chanzo kikuu cha tatizo hili ni kutokwa na jasho jingi miguuni pamoja na kuvaa viatu vilivyofungwa muda mrefu, hususan wakati wa joto kali.

Tatizo huongezeka zaidi endapo mhusika atakuwa na maambukizi ya bakteria au fangasi kwenye ngozi ya miguu.

Kwa nini miguu hutokwa na jasho kwa wingi? Jasho lina kazi muhimu mwilini. Husaidia kulainisha ngozi, kupunguza msuguano na kudhibiti joto la mwili, hasa wakati wa joto au mazoezi.

Hata hivyo, eneo la chini ya kifundo cha mguu lina tezi nyingi za jasho kuliko sehemu nyingine za mwili, zinazokadiriwa kufikia takribani 250,000 kwa miguu yote miwili.

Tofauti na sehemu nyingine, tezi za jasho za miguuni hutoa jasho karibu wakati wote, hata bila kufanya mazoezi au kuwa kwenye joto kali.

Harufu mbaya ya miguu haitokani moja kwa moja na jasho, bali hutokana na bakteria waliopo juu ya ngozi. Bakteria hawa huvunja jasho na kuzalisha kemikali zenye harufu kali, mara nyingi inayofanana na harufu ya jibini.

Tatizo la harufu mbaya ya miguu linaweza kusababishwa au kuongezeka kutokana na mambo yafuatayo kama kutumia jozi moja ya viatu kwa muda mrefu bila kubadilisha na kutovikausha viatu baada ya kutumika, hivyo jasho kubaki ndani na kuvaliwa tena kabla havijakauka.

Pia kutofuata kanuni za usafi wa mwili, hasa kwa watu wanaoishi maeneo yenye joto na mabadiliko ya homoni yanayoongeza utoaji wa jasho, hasa kwa vijana au watu wenye msongo wa mawazo na hofu.

Sababu nyingine ni kuwa na tatizo la kiafya linaloitwa Hyperhidrosis (kutokwa jasho kupita kiasi) na maambukizi ya fangasi kwenye ngozi ya miguu.

Ili kuepuka au kupunguza harufu mbaya ya miguu, zingatia kudumisha usafi wa mwili kwa kuosha miguu kwa maji safi na sabuni kila siku, kisha kausha vizuri kwa kitambaa safi, hasa katikati ya vidole.

Badili viatu mara kwa mara kwa kuepuka kuvaa viatu vilevile zaidi ya siku mbili mfululizo bila kuvikausha au kuviosha.Badili soksi kila siku ukitumia soksi za pamba zinazonyonya jasho kwa urahisi kuliko za nailoni.

Pia tumia poda au dawa maalum. Kuna poda na manukato maalum yenye viambato vya kuua bakteria na kupunguza harufu.

Chagua viatu vinavyopitisha hewa kama viatu vya ngozi halisi au turubai, pamoja na vile vyenye matundu, kwani husaidia kupunguza unyevunyevu.

Tumia soli zinazobadilika huku vikanyagio vya ndani (insoles) vikibadilishwa pindi vinapolowa na jasho.

Tibu fangasi mapema ikiwa una dalili za fangasi, tafuta matibabu katika kituo cha afya au tumia dawa za kupaka zilizoidhinishwa.