Uhakika wa chakula unavyojenga ustawi wa familia

Dar es Salaam. Uhakika wa chakula na lishe ni hali ambapo familia ina uhakika wa kupata chakula cha kutosha, salama na chenye virutubisho vinavyohitajika kwa maisha yenye afya.

Wazazi wanapokuwa na uhakika wa chakula, hupunguza wasiwasi na hofu ya kushindwa kukidhi mahitaji ya familia. Hali hii huleta utulivu wa kisaikolojia na kuboresha uhusiano wa kifamilia.

Mbali na kuzuia njaa, uhakika wa chakula na lishe una mchango mkubwa katika kuboresha afya ya mwili, akili na ustawi wa familia kwa ujumla.

Ofisa mtafiti mwandamizi wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Maria Ngilisho, anasema familia yenye uhakika wa chakula na lishe huwa na uwezo wa kula milo bora yenye uwiano sahihi wa virutubishi.

Hali hii huimarisha nguvu za mwili, kusaidia ukuaji, ukarabati wa mwili na kuongeza kinga dhidi ya magonjwa.

Anafafanua kuwa lishe bora huchangia ukuaji mzuri wa watoto, uimara wa misuli na mifupa, pamoja na kuongeza nguvu na uwezo wa kufanya kazi za kila siku kwa watu wa rika zote.

Kwa mujibu wa Ngilisho, watoto wanaopata lishe bora hujifunza kwa ufanisi zaidi na kushiriki kikamilifu katika michezo, huku watu wazima wakibaki na nguvu za kufanya kazi na kushiriki shughuli za uzalishaji mali.

Anasema ukosefu wa usalama wa chakula husababisha ulaji duni, hali inayoweza kuleta matatizo kama upungufu wa damu, uoni hafifu na uzito pungufu. Iwapo hali hizi zitadumu kwa muda mrefu, zinaweza kusababisha udumavu pamoja na uzito kupita kiasi, ambavyo ni vihatarishi vya magonjwa sugu.

“Mbali na afya ya mwili, uhakika wa chakula na lishe una mchango mkubwa katika kupunguza msongo wa mawazo ndani ya familia. Wazazi wanapokuwa na uhakika wa chakula, hupunguza wasiwasi na hofu ya kutokidhi mahitaji ya familia. Hali hii huleta utulivu wa kisaikolojia na kuboresha uhusiano wa kifamilia,” anasema Ngilisho.

Anaongeza kuwa ukosefu wa uhakika wa chakula huongeza msongo wa mawazo, migogoro ya kifamilia na hata matatizo ya kisaikolojia kwa watoto na watu wazima.

Aidha, anasema milo ya pamoja huchangia kuimarisha mawasiliano na uhusiano ndani ya familia. Familia inapokaa pamoja kula, hupata fursa ya kuzungumza, kushirikiana na kujenga upendo, jambo linalosaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuimarisha afya ya akili.

“Lishe bora pia husaidia ubongo kukua na kufanya kazi vizuri, hivyo kuboresha kumbukumbu, umakini na hali ya hisia,” anabainisha.

Ngilisho anasema uhakika wa chakula na lishe huongeza uwezo wa familia kukabiliana na changamoto kama mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa bei za vyakula au matatizo ya kiafya.

Familia yenye akiba ya chakula au kipato cha uhakika huwa na uwezo mkubwa wa kustahimili misukosuko bila kuathiri afya na ustawi wao.

Ngilisho anataja mambo kadhaa yanayoonyesha namna uhakika wa chakula na lishe, unavyopunguza msongo wa mawazo katika familia:

Kwanza, huondoa hofu ya kukosa chakula. Familia inapokuwa na uhakika wa milo ya kila siku, wazazi hupunguza wasiwasi wa nini watakula leo au kesho, hali inayochangia utulivu wa akili.

Anaeleza kuwa ukosefu wa uhakika wa chakula husababisha msongo wa muda mrefu (chronic stress) unaoweza kuathiri afya ya akili.

Pili, huimarisha afya ya mwili na akili. Lishe bora husaidia mwili na ubongo kufanya kazi vizuri, huku virutubisho kama vitamini na madini vikichangia kuimarisha mfumo wa neva, kinga ya mwili na kupunguza uchovu na hasira.

Anasema upungufu wa madini ya chuma unaweza kusababisha uchovu na kuathiri hali ya hisia, hivyo uhakika wa chakula husaidia kuepuka changamoto hiyo.

Tatu, huongeza uwezo wa kufanya kazi na kipato. Familia yenye lishe bora huwa na nguvu zaidi, jambo linalowawezesha wazazi kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza kipato, hivyo kupunguza msongo wa kifedha.

Nne, hupunguza migogoro ya kifamilia. Njaa na uhaba wa chakula mara nyingi husababisha mabishano kati ya wazazi na msongo kwa watoto, lakini uwepo wa chakula cha kutosha huleta utulivu na kuimarisha uhusiano.

Tano, huchochea milo ya pamoja. Familia inapokula pamoja huimarisha mawasiliano, upendo na msaada wa kihisia, hali inayopunguza msongo wa mawazo kwa watoto na wazazi.

Sita, huongeza hali ya usalama na udhibiti wa maisha. Kuwa na uhakika wa chakula kunaleta hisia ya utulivu na kupunguza wasiwasi, hivyo kuboresha ustawi wa kisaikolojia.

Saba, hujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto. Familia yenye uhakika wa chakula inaweza kukabiliana vyema na mishtuko ya maisha kama kupanda kwa bei au magonjwa bila kupata msongo mkubwa.

Kwa ujumla, uhakika wa chakula na lishe hauhusu tu kushiba na kuwa na afya ya mwili, bali pia afya ya akili, utulivu wa kisaikolojia na uhusiano imara wa kifamilia.

Hivyo, juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa chakula bora na lishe sahihi zinapaswa kupewa kipaumbele katika ngazi ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.