Boresha afya kwa bustani ya nyumbani

Dar es Salaam. Kulima bustani ya nyumbani si tu mapambo ya mazingira, bali ni uwekezaji wa moja kwa moja katika afya na uchumi wa familia.

Bustani hutoa chanzo cha uhakika cha mboga na matunda mabichi, yenye virutubisho muhimu kwa ajili ya kujenga, kuimarisha na kulinda mwili.

Ofisa lishe mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Abela Twinomujuni anasema kilimo cha bustani nyumbani ni njia rahisi na endelevu ya kuzalisha mbogamboga na matunda kwa matumizi ya familia.

Anataja kuwa kupitia bustani ya nyumbani, familia inaweza kuandaa mboga za majani kama mchicha, mnavu, spinachi na figiri, pamoja na miche ya matunda kama papai, machungwa na maembe.

Pia, bustani inaweza kutumika kupanda mazao yanayotambaa kama pasheni, matango na matikiti.

Mboga na matunda ni chanzo muhimu cha vitamini na madini yanayohitajika mwilini kila siku. Uwepo wake nyumbani hurahisisha upatikanaji wa vyakula hivyo na kusaidia familia kufikia mlo kamili unaoshauriwa kitaalamu.

Chanzo cha lishe bora na kipato

Twinomujuni anasema moja ya faida kubwa ya bustani ya nyumbani ni kupunguza gharama za maisha.

“Familia inapolima mboga na matunda yenyewe, huokoa fedha ambazo zingetumika kununua vyakula hivyo sokoni,” anasema.

Mbali na matumizi ya nyumbani, ziada ya mazao inaweza kuuzwa na kusaidia kupata kipato cha kununua vyakula vingine kama dagaa, mayai au maziwa kwa ajili ya kuboresha lishe ya familia.

Anabainisha kuwa mazao yanayotoka bustani ya nyumbani mara nyingi huwa mabichi na salama zaidi kwa sababu mkulima ana udhibiti wa namna yanavyolimwa.

Hata hivyo, anasisitiza umuhimu wa kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ya dawa na kemikali, akishauri matumizi ya mbolea za asili kama samadi au mboji ambazo ni nafuu na salama kiafya.

Kwa wakazi wa mijini wanaokabiliwa na uhaba wa maeneo, anashauri matumizi ya bustani za kiroba, makopo au vichuguu, ambazo hutumia eneo dogo, maji kidogo na gharama nafuu kuanzisha.

Mbali na lishe na kipato, bustani ya nyumbani ni aina ya mazoezi ya mwili. Kazi za kupanda, kumwagilia na kupalilia husaidia kuimarisha afya na kupunguza msongo wa mawazo.

“Mtu anayejishughulisha na bustani huwa anapata utulivu wa akili kwa sababu anaushughulisha mwili na akili kwa wakati mmoja,” anasema Twinomujuni.

Faida nyingine ni uhuru wa chakula.Familia yenye bustani huwa na uhakika wa upatikanaji wa mboga na matunda wakati wowote, bila kutegemea soko au kupanda kwa bei.

Prisca Edmund, mama wa watoto wawili, anasema bustani yake ya nyumbani imemsaidia kwa zaidi ya muongo mmoja kuokoa fedha na kupata mazao mabichi kila siku.

“Sikumbuki mara ya mwisho kununua mboga za majani sokoni ni lini. Bustani imenisaidia kula mazao freshi na yenye ubora wa juu,” anasema.

Aidha, bustani huchangia kupendezesha makazi na kuboresha mandhari ya eneo la nyumbani, na kuifanya familia kuishi katika mazingira safi na yenye kuvutia.

Kwa ujumla, wataalamu wanasema kila familia inaweza kuwa na bustani, iwe kijijini au mjini, kwa kuwa faida zake ni nyingi kuanzia lishe bora, afya njema, kipato hadi ustawi wa mazingira.