NASA Yatangaza Dakika 13 za Hatari Kwa Wanaanga wa Artemis II Wakitua Duniani

Shirika la anga za juu la Marekani, NASA, limeeleza kuwa hatua ya mwisho ya ujumbe wa Artemis II ndiyo yenye hatari kubwa zaidi, huku wanaanga wakitarajiwa kurejea duniani kesho Aprili 10, 2026 baada ya safari ya siku 10 angani.

Wanaanga Reid Wiseman, Christina Koch, Victor Glover pamoja na Jeremy Hansen wanatarajiwa kutua katika Bahari ya Pasifiki, katika operesheni itakayohitimisha safari yao ya kihistoria ya kuuzunguka mwezi.

Hatua ya kurejea duniani (re-entry) inachukuliwa kuwa ngumu na hatari zaidi, ambapo chombo cha Orion spacecraft kitapenya anga ya dunia kwa kasi kubwa huku kikikumbana na joto kali linalofikia zaidi ya nyuzi joto 2,700°C.

Maafisa wa NASA wanasema kuwa ni dakika 13 ambazo kila kitu lazima kiende sawa, kwani hitilafu yoyote inaweza kuhatarisha maisha ya wanaanga wote wanne.

Hofu kubwa imejikita kwenye kifaa cha kinga ya joto (heat shield) cha Orion, ambacho kilionyesha kasoro wakati wa jaribio la Artemis I mwaka 2022.

Ingawa NASA haikubadilisha kifaa hicho kwa safari hii, imebadilisha mbinu ya kuingia angani ili kupunguza hatari. Safari hii, chombo kitashuka kwa kasi zaidi na kwa mwelekeo mkali ili kupunguza muda wa kukaa kwenye joto kali.

Wakati wa kurejea, chombo kinatarajiwa kusafiri kwa kasi ya hadi kilomita 38,000 kwa saa, huku kukiwa na kukatika kwa mawasiliano kwa takriban dakika sita kutokana na miale ya joto (plasma) inayozunguka chombo hicho.

Baada ya kufikia urefu wa takriban mita 1,800 kutoka usawa wa bahari, parachuti zitafunguka na kupunguza kasi kabla ya kutua salama baharini.

Baadhi ya wataalamu, akiwemo mwanaanga wa zamani Charlie Camarda, wameonya juu ya hatari zinazoweza kujitokeza, wakisema historia inaonyesha ajali hutokea pale tahadhari hazichukuliwi vya kutosha.

 

Hata hivyo, NASA imeeleza kuwa ina imani kubwa na maandalizi yaliyofanyika, na mifumo yote muhimu imejaribiwa kwa mafanikio katika siku zote za safari.

Baada ya mafanikio ya kuuzunguka mwezi, macho ya dunia sasa yako kwenye hatua ya mwisho ya ujumbe huu. Dakika chache zijazo ndizo zitakazoamua hatima ya wanaanga na mafanikio ya ujumbe mzima wa Artemis II.