Mafuta yaanza kupaisha bei za bidhaa, vikao vyapishana bungeni

Dar/mikoani. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwataka wafanyabiashara kuzingatia uhalisia wa gharama na kuepuka kupandisha bei holela, hali halisi miongoni mwa wananchi imeonekana kuwa tofauti, wakieleza kuanza kuhisi makali ya ongezeko la bei za bidhaa na huduma.

Licha ya wito huo wa Serikali, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika mikoa mbalimbali ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Pwani, Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro, Njombe na Iringa, unaonyesha kuwa bei za bidhaa muhimu zimeendelea kupanda.

Bidhaa zilizobainika kuathirika ni pamoja na nyanya, ndizi, viazi mviringo, vitunguu, maji ya chupa, sukari, mafuta ya kula, mchele na unga.

Akizungumza jijini Dodoma Aprili 8, 2026 baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, Rais Samia alisisitiza kuwa wafanyabiashara wanapaswa kuzingatia uhalisia wa gharama kabla ya kuongeza bei kwa wananchi kwa kutumia kupanda kwa bei ya mafuta kama kigezo.

Mmoja Wa wafanyabishara wa bidhaa za sokoni ndani ya Manispaa ya Kibaha Kisandu Ernest akipanga bidhaa zake ambazo kwa sasa bei imepanda huku chanzo kikiezwa kuwa ni kupanda kwa bei ya mafuta. Picha na Sanjito Msafiri

“Kuna bidhaa ambazo zimeingia sokoni katika kipindi hiki na zimeathiriwa na msukosuko huu, hivyo kupanda kwa bei kunaweza kueleweka, lakini si zote,” alisema.

Hata hivyo, mchambuzi wa uchumi, Elihuruma Mushi, amesema endapo hali ya kupanda kwa bei ya mafuta itaendelea, kuna uwezekano mkubwa wa bei za bidhaa nyingi kuendelea kupanda kutokana na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji.

Mbali na bidhaa, nauli za usafiri wa umma ikiwemo bajaji na daladala katika baadhi ya maeneo zimeanza kupanda, licha ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kukutana na wadau wa sekta hiyo Aprili 8, 2026 na kuwataka kusubiri siku 14 kabla ya kutoa uamuzi.

Wafanyabiashara waliozungumza na Mwananchi wameeleza kuwa ongezeko hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na kupanda kwa gharama za usafirishaji.

Aprili 1, 2026 Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), ilitangaza ongezeko la bei za mafuta kwa zaidi ya Sh900 kwa lita.

Kupanda kwa bei hizo kunahusishwa na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, baina ya Marekani na Israel kwa upande mmoja, na Iran kwa upande mwingine, hali iliyoathiri uzalishaji na usafirishaji wa nishati hiyo duniani.

Hata hivyo, kuna dalili za matumaini ya kupungua kwa bei ya mafuta kufuatia taarifa za uwezekano wa kufunguliwa tena kwa njia hiyo muhimu, baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda wa wiki mbili.

Jijini Dar es Salaam wananchi waliozungumza na Mwananchi wamesema tayari wameanza kushuhudia kupanda kwa bei kwa bidhaa kadhaa na kuanza kuwaathiri wananchi, hasa wa kipato cha chini.

Viazi mviringo vikiwa kwenye ujazo tofautitofauti soko kuu Manispaa ya Iringa tayari kwa kuuzwa. Picha na Christina Thobias

Mkazi wa Magomeni, Yusuph Abdallah amesema: “Jana nilikuwa sehemu, nikanunua soda ya chupa. Baada ya kumaliza nikampa muuzaji Sh1,000 akanirudishia Sh200. Nikamuuliza kulikoni mbona hii badala ya Sh300? Akanijibu mambo yamebadilika.”

Amesema muuzaji alimweleza kuwa hata kwa wauzaji wa jumla gharama zimeongezeka kutokana na kupanda kwa gharama za usafirishaji, hivyo analazimika kuongeza bei ili kuendelea kupata faida ya kuendesha biashara.

Mkazi wa Mwananyamala, Aloyce Frank yeye amesema alikuwa ananunua maji ya kunywa kwa Sh700 lakini sasa analipa Sh800: “Ukiangalia yale yaliyokuwa Sh500 sasa ni Sh600. Hii inaonyesha wameongeza takribani Sh100 kwa kila bidhaa na hali inazidi kuwa ngumu kila siku.”

Mkoani Morogoro, mfanyabiashara Joshua Mugabo amesema bidhaa kadhaa zimepanda bei ndani ya muda mfupi. Ametaja viazi mviringo vilivyokuwa vinauzwa Sh55, 000 kwa gunia sasa vinauzwa Sh68, 000, huku dagaa wa Mwanza waliokuwa Sh10, 000 kwa kilo wakifikia Sh12,000.

Aidha, pilipili hoho ambazo awali zilikuwa Sh800 kwa kilo sasa zinauzwa hadi Sh2,000.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa vinywaji baridi, Aziz Msuya amesema hata soda zimepanda bei.

“Chupa ya soda sasa inauzwa Sh800 wakati ilikuwa Sh600 na soda za kopo zilizokuwa Sh1, 000 sasa zimefika Sh1,200,” amesema.

Tangawizi zikiwa soko kuu Manispaa ya Iringa tayari kwa kuuzwa. Picha na Christina Thobias

Katika soko la Sabasaba jijini Dodoma, mfanyabiashara Agnes Nicolaus amesema ongezeko la bei linaanzia mashambani hadi sokoni kutokana na kupanda kwa gharama za usafiri.

Amesema awali alikuwa akinunua tenga la nyanya kwa Sh30, 000 lakini sasa linauzwa kati ya Sh58,000 hadi Sh60,000 huku gharama ya usafirishaji zikiongezeka kutoka Sh3,000 hadi Sh6,000.

“Hapa sokoni hakuna bidhaa ambayo haijapanda bei. Sado ya vitunguu imepanda kutoka Sh7,000 hadi Sh9,000, viazi mviringo kutoka Sh3,000 hadi Sh5,000 na nyanya kutoka Sh3,000 hadi Sh6,000,” amesema Agnes.

Amesema hata mkungu wa ndizi umeongezeka kutoka Sh25,000 hadi Sh30,000, wakati kiroba cha viazi kimepanda kutoka Sh65,000 hadi Sh75,000 huku tikiti maji likipanda kutoka Sh2,000 hadi Sh4,000.

Vivyo hivyo katika Soko la Loliondo mkoani Pwani, Mfanyabiashara Jerson Segesela amesema tenga la nyanya limepanda kutoka  Sh45,000 hadi Sh60,000 huku gunia la viazi likiongezeka kutoka Sh55,000 hadi Sh70,000.

“Hata mafuta ya kupikia ya lita 20 ambayo tulikuwa tunauza Sh80, 000 sasa yamefika Sh100,000, hali inayosababisha wateja wengi kushindwa kumudu bei,” amesema.

Kwa upande wa mchele, Mfanyabiashara Aloyce Mgaya wa Iringa amesema bei ya mchele aina ya supa imeongezeka na sasa inauzwa kati ya Sh3,500 kwa kilo moja, huku mchele wa kawaida ukifikia Sh2,500 kutoka Sh2,200.

Karoti mkoani humo zimepanda kutoka Sh2,000 hadi Sh3,000 kwa kilo moja, huku tangawizi nayo ikiongezeka kutoka Sh3,000 hadi Sh6,000 kwa kilo.

Mbali na viungo, bei ya sukari nayo imepanda katika baadhi ya maeneo ya Iringa ambapo kilo moja imeongezeka kutoka Sh2,800 hadi Sh3,000.

Taus Emmanuel, mfanyabiashara wa Mbeya amesema maji madogo yamepanda kutoka Sh500 hadi Sh700, soda ndogo kutoka Sh500 hadi Sh700 huku kubwa kutoka Sh1,000 hadi Sh1,200.

Bei ya mchele imeendelea kubaki vilevile mabapo kwa ndoo ya kilo 20 inauzwa kati ya Sh58,000 hadi Sh70,000 kulingana na ubora.

Huko Moshi mkoani Kilimanjaro ongezeko hilo la bei nako limeshuhudiwa ambapo mchele uliokuwa ukiuzwa kwa Sh3,000 kwa kilo unauzwa kati ya Sh3,200 hadi Sh3,300.

Aidha, mafuta ya kula ya lita moja yamepanda kutoka Sh5,000 hadi Sh6,000 huku mahindi yakipanda kutoka Sh3,500 hadi Sh4,000 kwa sado moja.

Mkazi wa Majengo mjini Moshi, Aidan James amesema kupanda kwa bei za vyakula kunazidi kuwaongezea ugumu wa maisha ya kila siku.

“Kila kukicha imekuwa afadhali ya jana, sasa hivi ukienda sokoni kila kitu kimepanda bei, mchele, mafuta havishikiki, tunaomba Serikali iangalie namna ya kupunguza haya makali ya maisha, maana hali ni mbaya huku mtaani,” amesema James.

Wakati hali ikiwa hivyo, jana Jumatano, Aprili 8, 2026, Kamati ya Nishati na Madini chini ya uenyekiti wa Subira Mgalu ilikutana na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa ya Serikali kuhusu hali ya upatikanaji na bei za bidhaa za mafuta nchini.

Kikao hicho, kilihudhuriwa pia na Watendaji kutoka Wizara ya Fedha akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Elijah Mwandumbya.

Kama haitoshi, leo Alhamisi, Aprili 9, 2026 baada ya kipicha cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu, Spika wa Bunge Mussa  Zungu ameliambia Bunge kuwa anakabidhi kiti kwa Mwenyekiti Najma Giga kwani yeye anakwenda kwenye kikao.

“Waheshimiwa wabunge, naomba nimuachie kiti Mwenyekiti Najma Giga kwani mimi nakwenda kwenye kikao muda huu,” amesema Zungu.

Baada ya kuondoka kwenye kiti, Zungu alikwenda moja kwa moja eneo la Ofisi ndogo ya Spika iliyopo ndani ya ukumbi wa Bunge kwenye kikao kuhusu sakata la mafuta.

Wengine walioingia ndani ya ukumbi huo ni Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, Katibu wa Bunge, Baraka Leonard, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati, Subira Mgalu na wengine wachache walionekana kwenda huko.

Baadhi ya bidhaa zikiwa zimewekwa kwenye maduka ya rejareja katika Manispaa ya Moshi.

Kikao hicho kilidumu kwa muda wa dakika 50 ndipo viongozi hao wakatoka akianza Mgalu kisha Spika Zungu, Katibu wa Bunge na Waziri Ndejembi.

Mwananchi limemtafuta Mgalu kujua matokeo ya kikao cha Jumatano na cha Alhamisi kinaendelea ambapo amejibu kuwa, “Taarifa tumeiwasilisha kwa Spika, tunasubiri aipangie ratiba.”

Hata hivyo, Mgalu ambaye ni Mbunge wa Bagamoyo (CCM) aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini amesema vikao hivyo bado vinaendelea kikiwemo kitakachofanyika mchana wa Alhamisi.

Spika Zungu Aprili 1, 2026 aliiagiza Kamati ya Nishati na Madini kukutana na Waziri Ndejembi kupata taarifa ya nini kimetokea.

Zungu alitoa maagizo hayo dakika chache baada ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kusema Serikali itaketi ili kuangalia uwezekano wa kuleta unafuu kwa Watanzania.

“Tumeona bei zimeshaanza kupanda, tutakaa ndani ya Serikali kuhakikisha tunakabiliana nalo vipi suala hili ili wananchi waendelee kupata mafuta kwa bei nzuri na kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha.”

Imeandikwa na Christina Thobias (Iringa), Hawa Mathias, Sadam Sadick (Mbeya), Jesse Mikofu (Zanzibar), Sanjito Msafiri (Pwani), Rachel Chibwete (Dodoma), Hamida Sharif (Morogoro), Herrieth Makweta, Bakari Kiango na Elizabeth Edward (Dar).