10 mbaroni wakidai kuchukuliwa nyeti zao Zanzibar

Unguja. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, linawashikilia watu 10 wakidai kuchukuliwa nyeti zao na kusababisha madhara makubwa kwa watu waliowatuhumu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Richard Mchonvu, watu hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti kati ya Aprili 4 na 9 katika maeneo tofauti baada ya kudai wamechukuliwa nyeti zao na kusababisha kushambuliwa kwa watu waliowatuhumu kuwaibia nyeti hizo jambo ambalo amedai ni uzushi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 10, 2026 ofisini kwake Madema, Kamanda Mchonvu amesema katika matukio hayo 10, yapo ambayo yameambatana na uhalifu na wizi wa mali..

Amewataja watu hao ni Samir Mohamed Kasim (19), Abdul Amir Simkiwa (18), Khamis Hassan Jonathan (21), Aban Kasim Kasimba (26) na Mohamed Said Yakub (27).

Wengine ni Haji Salum Kasimba (55), Ali Said Ali (26), Juma Atukae Said (26), Salum Khamis Salum 48, na AbdulLatif Hassan Mohamed (29).

“Tarehe 4 tulipata tukio la kwanza maeneo ya Magomeni kijana mmoja aliibua tuhuma wakiwa ndani ya daladala kwamba kashikwa bega na nyeti zake zimeondoka,” amesema Mchonvu.

Amesema Aprili 7 majira ya jioni Forodhani kuna kijana alisema ameshikwa bega na nyeti zimeondoka na Aprili 8, maeneo ya Nyerere lilitokea tukio lingine na kusababisha watu washambuliwe.

Amesema zaidi kubwa jana yalitokea matukio mawili moja Kijangwani majira ya jioni

Kwa mujibu wa Kamanda tukio lingine lilitokea Kijichi Aprili 9 saa nne usiku kuna mfanyabiashara anayefanyia shughuli zake Masingini, muda huo alimkodi bodaboda kumpeleka nyumbani.

Amesema alipofika ndani baada ya saa moja kuna kundi la bodaboda likawa limezingira nyumba yake wakimtaka afungue.

“Alipouliza kuna shida gani wakasema umechukua nyeti za mtu kwahiyo tunataka urejeshe maumbile kama yalivyokuwa.

“Alivyoona hivyo akafunga mlango akarudi ndani, wakavunja mlango wakaingia ndani wakamshambulia wakapora Tv na kuharibu mali zake,” amesema.

Kwa mujibu wa Mchonvu amesema, “Tukaona sasa tunapoelekea sipo penyewe, kwa hiyo tunataka kuwaambia wananchi haya mambo yalivyo.”

Amesema watu wote waliokamatwa wakidai nyeti zimepotea, wamewapeleka hospitali ya serikali wamewapina na wakathibitisha kwamba hakuna mabadiliko yoyote ya maumbile yao.

“Kwa hiyo tunataka hili liwafikie wananchi kwamba watu wote hawa wamepimwa na hakuna mwemye athari lakini madhara waliyoleta ni makubwa kwasababu wamesababisha watu washambuliwe bila sababu za msingi,” amesema.

Amemea kati ya hao wanaondai wameshikwa waliposema wamechukuliwa nyeti, walipotea, mmoja kati ya hao ni mgonjwa wa akili.

“Tulipofika sasa hii hali inaleta taharuki sana tunaomba wananchi watulie haya ni uzushi na hakuna ukweli wa hayo mambo,” amesema.

Kwa mujibu wa Mchovu waliokamatwa watafunguliwa mashtaka ya kudanganya, uvunjifu wa amani na wizi.

Nao baadhi ya wananchi wamesema jambo hilo linaibua wasiwasi kwani watu wapo wanaoamini jambo hilo ni kweli na wengine kuona ni uzushi.

“Kuna kila sababu ya kutoa elimu maana hali imekuwa ngumu kuna taarifa nyingi za matukio haya hali hii ikoendelea inaweza kusababisha hata vifo vya mashambulizi,” amesema Kassimu Abdulla mkazi wa Rahaleo.