Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Uwekezaji, Dk Fred Msemwa amewataka watumishi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (Tiseza), kuondoa hulka ya kufanya kazi kwa mazoea kutokana na jukumu kubwa walilonalo katika kuchangia pato la Taifa kupitia uwekezaji.
Dk Msemwa amesema hayo leo Ijumaa, Aprili 10, 2026 wakati anafungua Baraza la kwanza la Wafanyakazi wa Tiseza, lililoundwa baada ya kuunganisha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA).
“Tiseza mna jukumu kubwa sana la kuhakikisha Tanzania inakuwa kimbilio la uwekezaji wa ndani na nje; na ninyi kama Baraza la Wafanyakazi mna mchango mkubwa wa kuifanya Tiseza ifanikiwe,” amesema.
Alisema Dira ya Taifa 2050 imeelekeza asilimia 70 ya pato la Taifa lichangiwe na sekta binafsi, ambayo uwekezaji upo ndani yake.
Hivyo, amewakata wafanyakazi hao kuwa wakarimu kwa wawekezaji ili waione Tanzania ni mahali sahihi pa uwekezaji.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Uwekezaji, Dk Fred Msemwa (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (Tiseza), baada ya kufungua baraza lao jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa Aprili 10, 2026.
Awali, akimkaribisha Dk Msemwa, Mkurugenzi Mkuu wa Tiseza, Gilead Teri amezungumzia matokeo ya utendaji wa wafanyakazi hao, kuwa katika kipindi cha Januari hadi Machi 2026 miradi 177 yenye thamani ya dola za Marekani 1.2 bilioni (Sh3.11 trilioni) imesajiliwa ikitarajiwa kutoa ajira 19,750.
Terry ameshukuru kwa ushirikiano anaoupata kutoka Ofisi ya Rais, Uwekezaji ambao unakuwa ni chachu ya kufanya maendeleo endelevu katika uwekezaji.
Amesema katika kutoa kipaumbele kwenye mradi wa Bagamoyo, Tiseza imeamua kuuundia kurugenzi maalumu ili kuhakikisha unakuwa na tija.
