Mradi wa Sh92 bilioni kuwawezesha walimu tarajali wakamilika baada ya miaka minane

Dodoma. Baada ya kudumu kwa takribani miaka minane ukilenga kuboresha ubora wa walimu wanaotarajiwa kuingia darasani, mradi wa kuwawezesha walimu tarajali wanaosoma katika vyuo vya ualimu nchini (TESP) wenye thamani ya Sh92 bilioni umekamilika, huku ukitajwa kuleta mabadiliko katika mafunzo ya ualimu na matumizi ya teknolojia katika vyuo hivyo.

Mradi huo ulioanza mwaka 2017 na kukamilika mwaka 2026, umetekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Global Affairs Canada, ukiwa na lengo la kuwajengea uwezo walimu tarajali ili waweze kumudu changamoto za ufundishaji wanapoingia kazini.

Akizungumza jana Alhamisi Aprili 9, 2026 jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Ndombo alisema mradi huo umejikita katika kuimarisha mafunzo katika vyuo vya ualimu pamoja na kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia.

Amesema teknolojia ilikuwa moja ya maeneo yaliyopewa kipaumbele katika utekelezaji wa mradi huo, ambapo baadhi ya vyuo vya ualimu viliunganishwa na mkongo wa taifa wa mawasiliano ili kurahisisha matumizi ya mafunzo ya kidijitali.

“Masuala ya teknolojia yalikuwa muhimu katika mradi huu. Baadhi ya vyuo viliunganishwa na mkongo wa taifa, huku vifaa vya kidijitali, maabara na maktaba vikiboreshwa ili kuwasaidia walimu tarajali katika maandalizi ya masomo yao,” amesema Profesa Ndombo.

Ameeleza kuwa pamoja na uboreshaji wa miundombinu, mradi huo pia ulizingatia masuala ya kijinsia kwa kuhakikisha kunakuwa na usawa katika nafasi za uongozi ndani ya vyuo vya ualimu pamoja na kutoa mafunzo kwa wakuu wa vyuo na watumishi wengine.

Profesa Ndombo amesema pia mradi huo uliangazia masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwa kujenga majengo mapya katika baadhi ya vyuo kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati mbadala.

Baadhi ya wakufunzi wa vyuo vya ualimu nchini na walimu tarajali wakiwa kwenye mkutano wa kukamilisha mradi wa kuwawezesha walimu wanafunzi (Tesp) Jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, Serikali ya Tanzania ilichangia katika maeneo mbalimbali ikiwemo kugharamia chakula cha wanafunzi pamoja na kuwezesha mafunzo kwa vitendo, huku Shirika la Global Affairs Canada likichangia fedha kiasi cha Sh92 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi huo, Cosmas Mahenge amesema mradi umefanikiwa kuimarisha matumizi ya Tehama katika vyuo 25 vya ualimu nchini kwa kuviunganisha na mkongo wa taifa wa mawasiliano.

Hata hivyo amesema bado kuna maeneo yanayohitaji kuboreshwa zaidi ili kuhakikisha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji yanaendelea kuimarika.

“Mradi umewezesha wakufunzi waliopo kazini kupata mafunzo ili kuendana na mabadiliko ya mitaala mipya iliyoanza kutumika kufuatia mageuzi ya elimu yaliyofanyika mwaka 2023,” amesema Mahenge.

Mkuu wa Chuo cha Ualimu Tabora, Balbina Joseph amesema mradi huo umeleta maboresho katika maeneo mbalimbali ikiwemo utoaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, utunzaji wa mazingira pamoja na kuimarisha usawa wa kijinsia katika vyuo vya ualimu.

Amesema kupitia mradi huo vyuo vilipatiwa vifaa vya Tehama ikiwemo kompyuta mpakato na za mezani, hatua ambayo imechangia kuboresha ujifunzaji na ufundishaji.

Mwalimu mwanafunzi kutoka Chuo cha Ualimu Mpwapwa, Gileadi Mgaya amesema mradi huo umewasaidia kupata mbinu bora za kujifunza na kufundishia kwa kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa.

Amesema hatua hiyo itawasaidia wanapoingia kazini kuwa na uwezo wa kufundisha kwa ufanisi zaidi na kukabiliana na changamoto za elimu katika mazingira ya sasa.