Lucas Sendama aweka msimamo Mbeya Kwanza

MSHAMBULIAJI wa Mbeya Kwanza, Lucas Sendama, amesema kwa sasa anafurahia maisha mapya na timu hiyo tangu ajiunge katika dirisha dogo la Januari 2026, akitokea Tanzania Prisons, ingawa, hatima ya mkataba wake ataijua mwishoni mwa msimu huu.

Nyota huyo amejiunga na Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship msimu huu katika dirisha dogo la Januari 2026, baada ya kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha maafande wa Prisons kutokea jijini, Mbeya.

“Mkataba wangu na Mbeya Kwanza ni wa mkopo, lakini baada ya msimu huu kuisha nitakuwa nimemalizana na Prisons na kuanzia hapo ninaweza kuangalia mambo mengine, malengo yangu kwa sasa ni kufanya vizuri na kuisaidia timu hii,” amesema Sendama.

Aidha, Sendama, amesema tangu amejiunga na timu hiyo amekuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara tofauti na Prisons, ingawa, kama mchezaji alikuwa hajakataa tamaa, kwa sababu aliwaheshimu waliokuwa wanacheza na kujifunza pia mambo mengi.

Mshambuliaji huyo aliyezichezea pia KenGold, Geita Gold, Biashara United na DTB iliyobadilishwa jina baadaye na kuitwa Singida Big Stars baada ya kupanda Ligi Kuu Bara, alijiunga na Prisons Agosti 14, 2025, baada ya kuondoka Stand United.

Msimu wa 2024-2025, Sendama aliifungia Stand mabao manne Ligi ya Championship na kuiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu na pointi 61, jambo lililosababisha kucheza mechi za (Play-Off) kusaka tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara na kukwama.

Stand ilicheza mtoano na Geita Gold iliyomaliza ya nne na pointi 56 na kuiondosha kwa kuichapa jumla ya mabao 4-2, kisha hatua iliyofuata ikakutana na Fountain Gate iliyotolewa na Tanzania Prisons na kikosi hicho kuchapwa jumla ya mabao 5-1.