KICHAPO cha bao 1-0 ilichopokea Sebleni kutoka kwa Black Sailors katika Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja, bado kinamtia simanzi kocha wa timu hiyo, Yahaya Yussuf.
Kocha huyo amesema licha ya timu kucheza kwa kufuata mpango maalumu ulioelekezwa, lakini imeshindwa kupata matokeo yaliyotarajiwa.
“Matokeo hayo hayakupatikana kutokana na wachezaji kushindwa kutumia nafasi walizozipata,” amesema.
Sebleni ilipokea kipigo hicho Machi 30, 2026 kwenye Uwanja wa Mao B, Mjini Unguja ikiwa ni mechi ya kwanza kucheza tangu ligi hiyo irejee kutoka kusimama kwa takribani mwezi mmoja kupisha mtukufu wa Ramadhani.
Kocha Yussuf amesema katika mechi hiyo, kikosi chake kilitumia mbinu ya kushambulia kwa kushtukiza ambayo iliwapa nafasi nyingi za kufunga lakini wachezaji walikosa umakini wa kumalizia mashambulizi yao.
Aliongezea kuwa, licha ya kupoteza mchezo huo, bado kikosi chake kilionesha kiwango kizuri na uwezo wa kushindana, jambo ambalo linampa matumaini ya kufanya vizuri katika michezo ijayo.
Pia, amewataka wachezaji wa timu hiyo kuongeza umakini wanapopata nafasi za kufunga na kujituma zaidi uwanjani ili kuepuka makosa yanayoweza kuigharimu matokeo.
Aidha, amewataka mashabiki wa Sebleni kuendelea kuiunga mkono timu yao na kuwapa nguvu wachezaji, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika safari ya kurejesha makali ya timu hiyo kwenye ligi.
Alisisitiza watafanyia kazi upungufu uliyojitokeza ili kuhakikisha wanarejea katika ushindani kwenye mechi zijazo.
Sebleni inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja ikikusanya pointi 33 baada ya kucheza mechi 21, wakati Black Sailors ikiongoza kwa pointi 59.
