Tanga. Baada ya miezi kadhaa ya malalamiko ya harufu kali na hofu ya magonjwa ya mlipuko, hatimaye dampo lililokuwa limefurika katika Soko la Mgandini jijini Tanga limeondolewa, hatua iliyorejesha matumaini kwa zaidi ya wafanyabiashara 1,500 wanaotegemea soko hilo kujipatia kipato.
Hata hivyo, licha ya hatua hiyo kuleta afueni, changamoto ya ukosefu wa vyoo katika soko hilo imeendelea kuwa kero kwa wafanyabiashara, huku baadhi yao wakilazimika kujisaidia kwenye vichaka vilivyo pembezoni mwa mfereji unaopita karibu na eneo la soko hilo.
Hatua ya kuondoa dampo hilo imechukuliwa na Halmashauri ya Jiji la Tanga ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajab Abdalah, aliyetoa muda wa wiki moja kuhakikisha adha ya dampo hilo pamoja na changamoto ya ukosefu wa choo inapatiwa ufumbuzi.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Meya wa Jiji la Tanga, Mustapher Seleboss, amesema uongozi wa jiji hilo umechukua hatua za haraka kusafisha eneo hilo kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na afya za wafanyabiashara pamoja na wananchi wanaotumia soko hilo.
Amesema zoezi la kusafisha dampo hilo lilihusisha jitihada kubwa za watumishi wa jiji, huku wakikesha kuhakikisha taka zote zinaondolewa.
“Maelekezo ya Mwenyekiti tumeyatekeleza kwa asilimia mia moja. Pia tumeongeza magari ya taka ili kuimarisha usafi katika masoko yote ya jiji. Hivi sasa magari mawili mapya ya taka yako njiani kutoka Dar es Salaam na kila moja lina uwezo wa kubeba tani 10,” amesema Seleboss.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajab Abdalah akiwa katika soko la Mgandini jijini Tanga eneo ambalo lilikuwa na dampo lililokuwa limefurika na kuhatarisha afya za wafanyabiashara zaidi ya elfu 1500 wanategemea soko hilo. Picha na Mbonea Herman.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdalah, amesema baada ya changamoto ya dampo kutatuliwa, hatua inayofuata ni kuhakikisha soko hilo linajengewa choo ili kuondoa adha inayowakabili wafanyabiashara.
“Tanga tunahitaji viongozi wanaochukua hatua kwa changamoto za wananchi. Hatuhitaji viongozi wanaolalamika huku wananchi nao wakibaki na malalamiko,” amesema Abdalah.
Amesema kama changamoto hiyo isingetatuliwa kwa wakati, alikuwa tayari kuandaa zoezi la usafi likishirikisha viongozi na wanachama wa chama hicho ili kuonyesha mfano wa uwajibikaji kwa jamii.
Mbali na suala la choo, Abdalah pia alimuelekeza Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Sebastian Danda, kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja soko hilo linaboreshwa kwa kuweka njia zinazopitika ili kuondoa adha ya matope yanayotokea wakati wa msimu wa mvua.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wamesema kuondolewa kwa dampo hilo ni hatua muhimu iliyorejesha matumaini ya kufanya biashara katika mazingira salama.
Mfanyabiashara wa nyanya katika soko hilo, Jabali Mussa, amesema hapo awali dampo hilo lilisababisha harufu kali na hata kuzuia magari yanayoleta bidhaa kuingia sokoni.
“Kwa kweli tulikuwa tunaishi kwa shida sana. Harufu ilikuwa kali na wakati mwingine magari ya kuleta nyanya yalishindwa kupita kwa sababu taka zilikuwa zimejaa mpaka barabarani,” amesema Mussa.
Hata hivyo, wafanyabiashara hao wamesema bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa choo, hali inayowalazimu kutumia maeneo yasiyo rasmi kujisaidia.
Mfanyabiashara wa viazi, Salakhe Ally amesema licha ya kufurahishwa na usafi uliorejeshwa sokoni hapo, tatizo la choo linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
“Tunajisaidia kwenye mfereji uliopo karibu na soko. Hii ni hatari, hasa kwa wanawake, na siyo mazingira salama kabisa,” amesema.
Wafanyabiashara hao wameiomba Halmashauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa haraka ili kuboresha zaidi mazingira ya biashara katika soko hilo maarufu jijini humo.