Wakulima wa kahawa watakiwa kuachana na kilimo cha mazoea

Moshi. Serikali imewataka wakulima wa kahawa nchini kuachana na kilimo cha mazoea na badala yake kuzingatia kilimo cha kisasa chenye tija ili kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa kahawa na kuwapa uwezo wa kushindana katika soko la kimataifa.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa zao hilo muhimu la biashara na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Profesa Peter Msofe, wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa miche 12,000 ya kahawa kwa wakulima katika Kata ya Uru Mashariki, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Msofe amesema wakulima wanapaswa kutumia mbinu bora za kilimo pamoja na miche bora ili kuongeza tija na ubora wa kahawa inayozalishwa nchini.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo, ikiwemo sekta ndogo ya kahawa, ili kuhakikisha zao hilo linakuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa wananchi.

“Miche bora ya kahawa ni nyenzo muhimu katika kuongeza tija ya uzalishaji. Uzalishaji wenye tija utamsaidia mkulima kupata faida na kuongeza ari ya kuwekeza zaidi katika kilimo,” amesema Profesa Msofe.

Ameeleza kuwa Wizara ya Kilimo inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya kahawa kwa kushughulikia changamoto zinazowakabili wakulima na kuboresha mazingira ya biashara ya zao hilo.

“Serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazozorotesha sekta hii, ikiwemo kuondoa kero zilizopo na kuhakikisha mkulima anapata bei inayoridhisha ya mazao yake,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo amesema wakulima wanapaswa kutumia vizuri ardhi waliyonayo kwa kuwekeza katika kilimo cha kahawa ili kupata manufaa zaidi kiuchumi.

Amesema licha ya kahawa kuwa sehemu ya urithi wa kihistoria kwa wakazi wa Kilimanjaro, ni muhimu sasa zao hilo litazamwe zaidi kama biashara yenye tija.

“Zao la kahawa kwetu hapa Kilimanjaro ni urithi tuliourithi kutoka kwa mababu zetu. Lakini sasa tunataka lichukuliwe kama kilimo cha kibiashara kitakachosaidia kuondoa umaskini,” amesema Kimaryo.

Ameongeza kuwa ardhi ya Kilimanjaro imebarikiwa kwa kilimo cha kahawa na kama wakulima wataitumia ipasavyo wanaweza kurejesha mafanikio yaliyowahi kupatikana hapo awali kupitia zao hilo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, John Meela amesema juhudi zinaendelea kufanywa kuhakikisha vijana wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika kilimo cha kahawa ili kulifanya zao hilo kuwa tegemeo la uchumi wa wananchi.

“Zao la kahawa lilikuwa na mchango mkubwa katika maisha ya watu wa Kilimanjaro. Wazazi wetu waliuza kahawa na fedha zake zilitumika kuwasomesha watoto. Tunaamini kama tutaliendeleza vizuri linaweza kurejesha ustawi wa kiuchumi kwa familia nyingi,” amesema Meela.