Dar es Salaam. Jamhuri imefanya mabadiliko katika hati ya mashtaka kwenye kesi ya kughushi vibali/leseni za kumiliki silaha, kwa kuongeza mashtaka 16 mapya, yakiwemo ya kukutwa na mihuri ya kughushi ya Jeshi la Polisi Tanzania.
Kesi hiyo inawakabili watu tisa, akiwemo maofisa sita wa jeshi hilo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mkaguzi wa Polisi mwenye namba PF. 19931 Fredrick Malekela (45) mkazi wa Kilwaroad; E. 4627 Sajenti Kalemwa Kaunga (54), mkazi wa Chanika; E.7855 Sajenti Edger Mlogo (54), mkazi wa Kibamba; F.1126 Sajenti Robert Titus (47), mkazi wa Kisarawe na F.5092 Sajenti John Kaposwe (46) mkazi wa Kurasini na WP 10050 Julieth Moshi (30), mkazi wa Kisarawe.
Wengine ambao sio maofisa wa jeshi hilo ni Damson Mnyilenga (59), mkulima na mkazi wa Chanika; Simon Aloyce (60), mfanyabiashara na mkazi wa Mwanza pamoja na Venrand Liberio (29), mfanyabiashara na mkazi wa Tataba, Dar es Salaam.
Kwa sasa washtakiwa hao, ambao wanakabiliwa na kesi ya kesi ya jinai namba 18451 ya mwaka 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, watakuwa jumla ya mashtaka 32, badala ya 16 yaliyokuwepo awali.
Wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi ameeleza hayo mahakama leo Ijumaa Aprili 10, 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuanza usikilizwaji.
Kati ya mashtaka 32 yakayowakabili washtakiwa hao, mashtaka 15 ni ya kughushi kitabu cha leseni za umiliki wa silaha, 15 ni kutoa nyaraka za uongo, ambazo ni kitabu cha leseni za umiliki wa silaha na mawili ni ya kukutwa na mihuri ya kughushi ya Jeshi la Polisi nchini Tanzania, kinyume cha sheria.
Akiwasomea upya mashtaka yao, Wakili Mbilingi amedai washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo, kinyume na kifungu namba 333 na 335A na kifungu 337 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Inadaiwa katika mashtaka hayo, wanadaiwa kuwa vibali au leseni hizo, vimetolea kati ya Desemba 5, 2024 hadi Aprili 4, 2025.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa katika kipindi cha mwaka 2024, ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ni kitabu cha leseni ya kumiliki silaha chenye jina la Ahmed Ally, wakati wakijua kuwa sio kweli.
Vile vile mashtaka mengine kuanzia shtaka la pili hadi la 13, wanadaiwa katika kipiundi cha mwaka 2024 na mwaka 2025 ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, walighushi na kutengeneza vitabu vya leseni za kumiliki silaha vyenye majina ya Ahmed Ahmed Sandrudin, Omary Abdallah, Robert Koka, Fathi Ally, Mohamed Salim, Suleman Mbewa, Mickdad Chakindo, Irfan Nafari, Gulam Abbas Najafi, Ismail Ismail na Salim Salim.
Katika shtaka la 14 hadi 30, washtakiwa kwanadaiwa mwaka 2025 katika mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai walitengeneza nyaraka za uongo ambazo ni kitabu cha leseni ya kumiliki silaha chenye jina la Marwaan Habretsh, Maurice Kitiwe na Said Mohamed na wengine,wakati wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Mbilingi alidai katika shtaka la 31 na 32, washtakiwa kwa pamoja na kwa nia ya makusudi na kinyume cha sheria walikutwa na mihuri ya kughushi ya Jeshi la Polisi Tanzania.
Washtakiwa baada ya kusomewa mnashtaka yao, walikana kutenda kosa hilo na upande wa mashtaka waliieleza mahakama hiyo tayati wamesajili nyaraka mtandaoni kwa ajili ya upande wa utetezi wawezi kuzisoma kabla ya kuanza usikilizwaji.
“Mheshima hakimu, kutokana na kuwaongezea mashtaka washtakiwa hawa, kuna nyaraka ambazo awali hazikuwepo wakati tulipowasomea hoja za awali, hivyo kwa sababu hiyo tayari tumeshasajili nyaraka hizo ambazo zinatokana na ongezeko la mashtaka tuliyowasomea leo. Nyaraka hizo ni vitabu 19 vya leseni za sihaha wanazodaiwa kughushi washtakiwa hawa,” alidai na kuongeza
“Kutokana na sheria kueleza kuwa kabla ya kesi kuanza kusikilizwa, washtakiwa wanatakiwa wapewe maelezo ya mashahidi pamoja na nyaraka zinazohuka katika kesi husika, tunaomba kuahirisha kesi hii kwa leo ili tuwape nafasi washtakiwa na mawakiliwa waweze kupitia nyaraka hizo,” amesema
Mawakili wa utetezi hawakuwa na pingamizi na hakimu Mhini aliahirisha kesi huyo hadi Mei 11, 2026 itakapoanza usikilizwa.
“Kesi hii itasikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Mei 11, 206 hadi Mei 13, 2026 upande wa mashtaka mjitahidi kuleta mashahidi wa kutosha,” alisema Mhini.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani Julai 28, 2025 na kusomewa mashtaka. Kwa saasa wapo nje kwa dhamana.
