Minara ya Mawasiliano Yazinduliwa, Rais Samia Ahimiza Ubunifu (Picha +Video)

Global Publishers
April 10, 2026
0 Comments

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewahimiza wadau mbalimbali nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha ubunifu, kuongeza uwekezaji na kupanua miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha Watanzania wote wananufaika na maendeleo ya kidigitali.

Akizungumza Ijumaa, Aprili 10, 2026 wakati wa uzinduzi wa minara 758 ya mawasiliano pamoja na maunganisho ya Mkongo wa Taifa katika wilaya 85, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, Rais Samia amesema maendeleo ya kidigitali yanahitaji ushirikiano wa sekta zote.

Amesema Serikali inaendelea kupanua huduma za mawasiliano ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika safari ya kuelekea uchumi wa kidigitali jumuishi.

“Naomba kuwahimiza wadau wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza ubunifu, kukuza uwekezaji na kupanua miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika safari yetu kuelekea Tanzania ya uchumi wa kidigitali na jumuishi,” amesema Rais Samia.

Aidha, ameongeza kuwa upanuzi wa huduma za mawasiliano vijijini na maeneo ya pembezoni unatarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta muhimu ikiwemo elimu, afya na biashara mtandao, hatua inayolenga kuimarisha maendeleo jumuishi nchini.