Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa maagizo kwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kuhakikisha vijana wa Kitanzania wananufaika kikamilifu na fursa zinazotokana na ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Akizungumza leo Aprili 10, 2026, Jijini Dodoma mara baada ya kuzindua minara 758 ya mawasiliano pamoja na kuimarishwa kwa mkongo wa taifa katika wilaya 85, Rais Samia alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuchochea ajira na ubunifu kwa vijana.
Alisisitiza kuwa miundombinu hiyo inapaswa kutumika kikamilifu kuwawezesha vijana kujenga ujuzi wa kidijitali na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
“Ni muhimu kuhakikisha vijana wetu wanapata fursa za kunufaika na uchumi wa kidijitali kupitia ubunifu, ajira na matumizi sahihi ya teknolojia,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais alielekeza kuwepo kwa mazingira rafiki kwa kampuni changa (start-ups) zinazomilikiwa na vijana, ikiwemo upatikanaji wa mitaji ili ziweze kukua na kushindana katika soko la ajira na biashara.
Katika kuimarisha juhudi hizo, aliwataka wadau wa sekta binafsi kushirikiana na serikali katika kukuza uwekezaji na ubunifu kwenye sekta ya TEHAMA, akibainisha kuwa vijana ndio nguvu kazi kuu ya uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa na teknolojia.
Sambamba na hilo, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu ya mkongo wa taifa ili kuhakikisha inaendelea kutoa huduma bora na kuchangia maendeleo ya taifa.
Aidha Rais amesisitiza kuwa utekelezaji wa maagizo hayo utahakikisha hakuna kijana anayebaki nyuma katika safari ya kuelekea uchumi wa kidijitali jumuishi nchini.



