Biashara ya EAC yapaa hadi kufikia Dola bilioni 42.4

Arusha. Biashara ya kimataifa ya bidhaa ya nchi za jumuiya ya Afrika mashariki (EAC) imefikia dola za Marekani bilioni 42.4 katika robo ya nne ya mwaka 2025, (Oktoba – Desemba) kutoka dola bilioni 40.3 zilizokuwa katika robo ya tatu ya mwaka huo katika kipindi cha Julai -Septemba.

Kwa mujibu wa taarifa ya takwimu ya robo mwaka iliyotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki Jana Aprili 9, 2026 inaonyesha kuwa ukuaji wa mauzo ya nje ndio chanzo cha mafanikio hayo.

Katika taarifa hiyo inaonyesha kuwa uagizaji wa bidhaa uliongezeka kwa asilimia 15.4 na kufikia dola bilioni 79.6, huku mauzo ya nje yakipanda kwa kasi ya asilimia 37.7 na kufikia dola bilioni 77.0 katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025.

“Hatua hii ilisababisha kupungua kwa nakisi ya biashara hadi dola bilioni 2.5, kutoka dola bilioni 13.0 mwaka 2024,” imeeleza taarifa hiyo, ikionesha uboreshaji mkubwa wa biashara ya nje ya ukanda.

Katika biashara ya ndani ya Afrika, ukuaji uliendelea kuwa imara kwa kupanda kwa asilimia 40.1 na kufikia dola bilioni 39.0, sawa na asilimia 25.2 ya jumla ya biashara yote.

Biashara ya ndani ya EAC pia ilipanuka kwa asilimia 28.0 na kufikia dola bilioni 19.3, hali inayoonesha maendeleo endelevu katika urahisishaji wa biashara na kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama.

Bidhaa za madini ziliendelea kutawala katika mauzo ya nje, hususan shaba, pamoja na madini ya thamani na mawe ya vito.

Aidha, bidhaa za kilimo kama kahawa, chai na viungo hazijabaki nyuma Bali ziliendelea kuwa nguzo muhimu katika mapato ya fedha za kigeni na kuimarisha maisha ya wananchi vijijini katika nchi za Ukanda.

Katika soko la kimataifa, China iliendelea kuwa mshirika mkuu wa biashara wa EAC, ikifuatiwa na Falme za Kiarabu (UAE), Afrika Kusini, India, Japan na Marekani.

Kwa upande wa uagizaji, bidhaa za nishati, mitambo na bidhaa zilizotengenezwa viwandani ziliendelea kuchochea uzalishaji wa viwanda, maendeleo ya miundombinu na mahitaji ya watumiaji.

“Ukuaji mkubwa wa mauzo ya nje ukilinganishwa na uagizaji, pamoja na kupungua kwa nakisi ya biashara, unaonesha mwelekeo chanya kuelekea ukuaji endelevu wa uchumi na ushirikiano wa kina wa kikanda,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa upande wa shinikizo la mfumuko wa bei katika ukanda huu lilianza kupungua kuelekea mwisho wa mwaka 2025.

Aidha Mfumuko wa bei wa mwaka ulipungua hadi asilimia 13.3 mwezi Desemba 2025, kutoka asilimia 15.2 Novemba, na kushuka zaidi ikilinganishwa na asilimia 27.1 Desemba 2024.

Hata hivyo, wastani wa mfumuko wa bei kwa mwaka 2025 ulipanda hadi asilimia 22.9, kutoka asilimia 13.6 mwaka 2024, hali iliyochangiwa zaidi na viwango vya juu nchini Sudan Kusini na Burundi.

Mfumuko wa bei unaoondoa bei za chakula na nishati, Kwani hizo zilipungua hadi asilimia 9.6 Desemba 2025, kutoka asilimia 12.0 Novemba.

Ukuaji wa ujazo wa fedha (M3) ulipungua hadi asilimia 14.7 kwa mwaka, ukiungwa mkono na ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi lililofikia asilimia 12.6, ishara ya kuendelea kwa shughuli za biashara na uwekezaji.

Mali za kigeni ziliongezeka kwa asilimia 20.4, zikionesha kuimarika kwa uthabiti wa kifedha wa nje wa ukanda.

Mkazi wa Arusha Federdaus Mosha akitoa maoni amesema kuwa iko haja ya kuongezeka kwa uwekezaji katika miundombinu ya biashara na fursa za kiuchumi ili kuendeleza kasi ya ukuaji wa ukanda.

“Kuna haja ya kuongeza ujumuishaji wa kifedha, kupunguza vikwazo vya biashara mipakani, na kuoanisha mifumo ya kifedha na hali halisi ya uchumi wa kila nchi ili kurahisisha shughuli za wafanyabiashara, hasa wajasiriamali,” amsema

Ameongeza kuwa hatua hizo zitakuwa muhimu katika kufungua zaidi fursa za ukuaji na kuhakikisha EAC inaendelea kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi katika miaka ijayo.