Ripoti ya CAG yaibua madudu mengine miradi AFCON 2027

RIPOTI ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imebaini ongezeko la gharama katika ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Arusha na Benjamin Mkapa vitakavyotumika katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao unafanyiwa ukarabati, CAG amebaini makosa katika majadiliano ya bei ya mkataba ambayo yamechangia kuongezeka kwa bei ya mkataba.

Mambo matatu yametajwa kuchangia hilo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambayo ni  kujadili bei “isiyo na usawa au iliyozidi“ kwa vifaa vya mwanga, kutotoa nafasi kwa mzabuni kuthibitisha au kutoa mchanganuo wa bei kama inavyotakiwa na ongezeko la vitu ambavyo havikuidhinishwa na bodi ya zabuni.

“Timu ilijadili vitu vitatu vya ziada (pamoja na viti vya uwanja na jenereta) ambavyo havikujumuishwa katika mpango wa mazungumzo ulioidhinishwa na bodi ya zabuni. Kwa mfano, bei kwa kila kiti iliongezwa kutoka shilingi 81,000 hadi shilingi 99,114.

“Vitendo hivi vilisababisha ongezeko la bei ya mkataba ya jumla ya Sh1.98 bilioni (inayojumuisha Sh1.67 bilioni kutoka kwa vifaa vya mwanga na Sh314.04 milioni kutoka kwa vitu nje ya mpango wa mazungumzo). Ukiushi huo wa taratibu za ununuzi zilizowekwa huiweka taasisi nunuzi katika hatari ya kupata hasara ya kifedha na kudhoofisha uadilifu wa mchakato wa zabuni ya ushindani,” imefafanua ripoti hiyo.

Kwa Uwanja wa Arusha ambao ujenzi wake unaendelea, CAG amebaini ongezeko la Sh2.97 bilioni ikiwa ni gharama za ziada za uboreshaji wa uwanja huo.

“Nilibaini Sh2.97 bilioni ilizidi kwa sababu ya hesabu isiyo sahihi ya maeneo yanayohitajika kufanyiwa kazi. Wakati msimamizi wa Mradi aliidhinisha mahitaji ya mita za mraba 877.106, uthibitishaji uliofanywa wakati wa ukaguzi uligundua kuwa ni mita za mraba 442.072 tu ndizo zilizojengwa, hivyo kuacha eneo lisilohitajika la mita za mraba 435.034.

“Kwa kuzingatia mkataba huo umeundwa kama usanifu na ujenzi, kuna hatari Serikali inaweza kulipa kiasi kamili cha nyongeza ya Sh5.99 bilioni, licha ya kupunguzwa kwa nafasi iliyojengwa. Hali hii ilitokana na maandalizi duni ya nyongeza ya mradi,” imefafanua ripoti hiyo.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa, amesema hoja za CAG zitajibiwa kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria.

Kitakachofanyika, amesema ni maofisa masuuli wataitwa kueleza kila hoja iliyoibuliwa na mkaguzi huyo na zitakazojibiwa zitafutwa na zitakazokosa majibu, hatua za uwajibikaji zitafuata.

“Muda wa kutoa majibu upo kwenye utaratibu, ndiyo maana kwenye ufafanuzi wangu nasema CAG amebaini maeneo ambayo ameona kuna dosari, Serikali itapewa muda wa kujibu hoja zote hizo, kupitia maofisa masuuli,” amesema Msigwa.

Katika hatua nyingine, ripoti hiyo ya CAG imebainisha kufanywa kwa malipo ya Sh4.5 bilioni kwa kazi ambazo hazijatekelezwa kwa ajili ya ukarabati wa Uwanja wa Uhuru.

“Kifungu cha 14.3.2 cha masharti ya jumla ya mkataba (GCC) kinahitaji mkandarasi kutuma maombi ya malipo kulingana na makadirio ya thamani ya kazi zilizotekelezwa. Zaidi ya hayo, kifungu cha 14.6 cha GCC kinahitaji msimamizi wa mradi kuamua na kuthibitisha thamani ya kazi zilizotekelezwa kama ilivyowasilishwa na mkandarasi kabla ya malipo.

“Hata hivyo, mapitio ya hati ya maombi ya malipo Na. 2 na uthibitishaji wa hali halisi ya ujezni yalibaini kuwa malipo ya kiasi cha Sh4.5 bilioni yalifanywa kwa viti vya watazamaji, mitambo ya umeme, vifaa vya eneo la kukimbilia, na nyasi bandia na vifaa vyake ambavyo vilikuwa bado havijatekelezwa,” imefafanua ripoti hiyo.

Ripoti hiyo imependekeza kwamba Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ihakikishe kiasi kilicholipwa zaidi kinarejeshwa.