Mapya yaibuka Uchaguzi Tunduru Kusini, serikali yapewa siku tatu

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songea,imetoa muda wa siku tatu kwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tunduru Kusini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kuwasilisha maombi ya mapitio nje ya muda katika shauri la uchaguzi linalohusu matokeo ya Uchaguzi wa Ubunge (jimbo la Tunduru Kusini).

Maombi hayo yaliwasilishwa na Msimamizi huyo wa Jimbo hilo na AG dhidi ya Mohamed Rais, Odax John na Fadhili Chilombe.

Katika maombi hayo,waombaji waliiomba mahakama iwape ruhusa ya kuwasilisha maombi ya mapitio nje ya muda uliowekwa kisheria ili kupitia uamuzi uliotolewa Desemba 29, 2025 katika kesi ya uchaguzi iliyohusisha pande zote.

Uamuzi huo uliotoa muda wa nyongeza ulitolewa na Aprili 8, 2026 na Jaji Emmanuel Kawishe na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Upande wa mwombaji, uliwakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Stanley Kalokola huku wajibu maombi wakiwakilishwa na Mawakili John Seka na Gilbert Sawe.

Upande wa mwombaji walieleza sababu ya kuchelewesha maombi hayo kulitokana na kugundua ushahidi mpya ambao haukuwepo wakati wa kesi ya awali kusikilizwa.

Alidai kuwa baada ya uamuzi wa mahakama kubatilisha pingamizi lao la awali, walifanya juhudi za kufuatilia uhalali wa msaada wa kisheria uliotolewa na upande wa wajibu maombi na kuwa katika mchakato huo walipata taarifa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwamba Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) haikuwa na leseni halali ya kutoa msaada wa kisheria tangu Aprili 28,2022.

Chini ya aya ya 10 ya hati ya kiapo iliyoungwa mkono, imeelezwa kuwa leseni ya TLS kutoa msaada wa kisheria iliisha tangu tarehe tajwa juu.

Kwa mujibu wa waombaji, taarifa hiyo ni muhimu kwa sababu mahakama awali ilifikia uamuzi wake kwa kuamini wajibu maombi hao walikuwa wanapata msaada wa kisheria kihalali,jambo linaonekana kuwa na utata mkubwa.

Mawakili hao walisisitiza kama Mahakama ingekuwa na taarifa hiyo wakati wa kusikiliza pingamizi la awali, ingeweza kutoa uamuzi tofauti na kuwa hawakuwa wazembe kufuatilia haki yao kwani baada ya uamuzi walichukua hatua za kukata rufaa,lakini baadaye waliondoa notisi ya rufaa baada ya kubaini uwepo wa msingi wa kuomba mapitio.

Kwa upande wao wajibu maombaji walipinga ombi hilo wakidai waombaji walikuwa wanajaribu kutumia mbinu zisizo halali kisheria na kuwa kiapo kilichowasilishwa na waombaji kilikuwa na taarifa zisizo sahihi hususani madai kwamba hakukuwa na rufaa inayosubiriwa mahakamani.

Kuhusu madai ya leseni ya TLS walidai halikuwahi kujadiliwa katika kesi ya awali hivyo haliwezi kuwa msingi wa mapitio bali lingeweza kuwasilishwa katika rufaa.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kupitia nyaraka zilizowasilishwa, Mahakama Kuu ilibaini kuwa suala kuu lililohitaji kuamuliwa ni kama waombaji walikuwa na sababu nzuri na za kutosha za kuongezewa muda.

Jaji Kawishe alieleza kuwa ni kanuni kwamba mahakama ina mamlaka ya kuongeza muda wa kuwasilisha maombi au rufaa nje ya muda, lakini mamlaka hayo lazima yatumike kwa busara na kwa kuzingatia haki.

Katika uamuzi wake, jaji alikubaliana na hoja za waombaji kuwa hawakuwa wazembe katika kufuatilia haki yao, akibainisha kuwa walichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwasilisha notisi ya rufaa na kufanya uchunguzi kuhusu uhalali wa msaada wa kisheria uliotolewa.

Jaji Kawishe amesema sababu kuu ya waombaji ni kutokana na kutupiliwa mbali pingamizi lao Desemba 29, 2025.

Mahakama pia ilikubaliana kwamba notisi ya rufaa si rufaa yenyewe, hivyo uwepo wake haukumaanisha kuwa waombaji walikuwa wanatumia njia mbili za kisheria kwa wakati mmoja.

Kuhusu madai ya uongo kwenye kiapo, mahakama ilibaini kuwa hayakuwa na msingi kwani nyaraka zinaonyesha wazi kuwa notisi ya rufaa iliondolewa kabla ya kuendelea na hatua nyingine.

Aidha, mahakama iliona kuwa suala la leseni ya TLS linaweza kuwa na uzito wa kisheria na linaweza kuathiri uhalali wa uamuzi wa awali hivyo kutoa muda wa siku tatu kuanzia tarehe ya uamuzi huo ili wawasilishe maombi hayo ya mapitio nje ya muda.

“Ni wazi kwamba ushahidi mpya hukuwafikia waombaji wakati wa kusikilizwa kesi kama walivyosema.Kwa kuwa suala la leseni halali katika kutoa msaada wa kisheria ni suala la kisheria,kama halitafuatwa na kusababisha uvunjifu wa sheria.Ni busara kwa mahakama kupata fursa ya kuzingatia ushahidi upya,”amehitimisha

Awali Desemba 29,2025 Mahakama hiyo ilitupilia mbali pingamizi shauri la uchaguzi Tunduru Kusini,baada ya kusikiiza hoja za pande zote mbili imeeleza kuwa walalamikaji wanaopata msaada wa kisheria hawalazimiki kulipa dhamana ya gharama, hivyo shauri la ubunge kuendelea kusikilizwa.

Pingamizi hilo la awali liliwasilishwa na Msimamizi huyo wa uchaguzi katika jimbo hilo na AG, katika shauri la uchaguzi linalohusu matokeo ya uchaguzi wa Ubunge.

Uamuzi huo ulitolewa Desemba 29, 2025, na Jaji James Karayemaha anayesikiliza shauri hilo lililofunguliwa Novemba 26, 2025.

Shauri hilo limetokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 wa Rais, Wabunge na Madiwani ambapo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilimtangaza Fadhili (mlalamikiwa wa pili) kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa mshindi.

Mahakama hiyo baada ya kusikiliza na kuchambua kwa kina hoja za kisheria zilizotolewa na mawakili wa pande zote,imejiridhisha kuwa walalamikaji hawakupaswa kuwasilisha maombi ya dhamana ya gharama.

Kutokana na sababu hiyo Mahakama hiyo ilitupilia mbali pingamizi hilo lililoibuliwa na mlalamikiwa wa kwanza na wa tatu kwani halina mashiko na kuamuru kila upande utabeba gharama zake.

Walalamikaji hawakuridhika na matokeo hayo na wakaamua kuyapinga Mahakamani wakidai kuwa uchaguzi haukuwa huru na wa haki ambapo kupitia shauri hilo hilo wanaomba Mahakama itoe nafuu nne.

Nafuu hizo ni kutamka kuwa uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Tunduru Kusini ni batili, uteuzi wa Fadhili kama mbunge haukuwa halali,kufanyika kwa uchaguzi wa kura ili kuthibitisha Fadhili hakuwa mgombea aliyepata kura nyingi katika jimbo hilo hivyo hakustahili kutangazwa na nafuu nyingine Mahakama itakayoona inafaa.