Kimoto kutua na wawili Singida Black Stars

SINGIDA Black Stars imemtangaza kocha mpya wa kikosi hicho, Papy Kimoto, akiwa na msaidizi wake Kapiten Ngoyi Dora ambao wote wamesaini mkataba wa mwaka mmoja na miezi mitatu.

Kimoto, raia wa DR Congo, anatua Singida BS baada ya kuachana na klabu yake ya Union Maniema iliyoishia hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika. Pia Kimoto atakuwa na msaidizi mwingine hivyo kuwa wasaidizi wawili.

Awali, Singida BS ilitangaza kutimua benchi lote la ufundi kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo katika kipindi cha hivi karibuni ukichagizwa na kupoteza dhidi ya TRA United mabao 2-0.

Baada ya hapo ilitua DR Congo kusaka kocha na majina mawili yalitua mezani akiwemo Guy Busaka wa FC Lupopo na Kimoto na mazungumzo ya awali yalionekana kuwa magumu kutokana na matakwa kuwashinda mabosi wa timu.

Awali Singida ilikuwa imchukue kocha Guy Bukasa anayeifundisha timu ya taifa ya vijana ya DR Congo, lakini inadaiwa aligoma kuachana na majukumu yake mpaka mkataba wake utakapomalizika.

Taarifa za ndani zimelidokeza Mwanaspoti, “Singida ilikuwa inataka kocha sasa hivi baada ya kufuta benchi lake, Bukasa ilikuwa ngumu hakutaka kuondoka vibaya pale Congo ndiyo maana wakaweka nguvu kwa Kimoto.”

Kimoto amekubali ajira hiyo akija na wasaidizi wawili kwenye benchi jipya ambapo wakati wowote wiki hii atatua nchini kuanza kazi kuchukua nafasi ya Othman Najjar ‘Otna’, raia wa Tunisia.

Taarifa kutoka Singida BS zinadai Kimoto anakwenda kuwa meneja mkuu na Kapiten Ngoyi Dora kuwa kocha msaidizi wote wakisaini mkataba wa mwaka mmoja na miezi mitatu.

Pia, Muhibu Kanu ataendelea kukaimu nafasi ya kocha mkuu hadi mwisho wa msimu huu akisimamia kikamilifu jukumu la kushirikiana na safu mpya ya benchi la ufundi.

Makocha wapya wa Singida BS wanakwenda kuongeza idadi ya wakufunzi wa Kikongomani ambao wanafundisha Ligi Kuu Bara ambapo wanafikia watatu msimu huu wakiongozwa na Florent Ibenge.

KANU AENDELEA KUPIGA MZIGO

Katika hatua nyingine, kaimu kocha mkuu wa Singida BS, Muhibu Kanu amesema hakupata shida kuendeleza pale walipoishia makocha wengine kutokana na kujua jinsi ya kuendana na wachezaji, kuhakikisha hawatoki katika mstari wa mapambano.

Uongozi wa Singida BS ulivunja benchi la ufundi lililokuwa chini ya kocha mkuu David Ouma baada ya kufungwa mabao 2-0 dhidi ya TRA, hivyo timu ikakabidhiwa kwa Kanu kwa muda akisaidiana na Amissi Tambwe nyota wa zamani wa Simba na Yanga.

Kanu ana leseni A ya CAF amesema: “Nafurahia kufanya kazi ya taaluma niliyoisomea, hakuna changamoto ya kibinafsi ninayoipata, najua jinsi ya kuendana na wachezaji na siyo mara ya kwanza kufundisha timu, nimewahi kuifundisha Pamba kabla hajapanda Ligi Kuu.”

Amesema kwa sasa anaelekeza nguvu kufanya vizuri mechi zilizopo mbele yao, akiwaacha viongozi kuendelea na majukumu yao, ikifika wakati wa kupewa maelekezo mengine atayafuata. “Kuhusu kocha nani anakuja hilo ni jukumu la viongozi, ikitokea kaja basi nitafanya majukumu mengine nitakayopangiwa, kikubwa ni kuona timu ikifanya vizuri na kufikia malengo,” amesema Kanu aliyewahi kuitumikia Stand United ‘Chama la Wana’ ya Shinyanga ambayo kwa sasa inacheza Ligi ya Championship.