Ripoti ya CAG yafichua ‘bomu’ usafiri wa umma

Dar es Salaam. Usafiri wa umma mijini nchini Tanzania unakabiliwa na majanga, baada ya magari ya huduma za jamii kupungua kwa asilimia 55, huku daladala zikipungua kwa asilimia 19, hali inayochangiwa na uratibu usioridhisha wa mamlaka husika.

Ukistaajabu kuporomoka kwa njia hizo za usafiri wa umma, utekelezaji wa malengo ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Dar es Salaam utakushangaza, kwani umeshuka hadi asilimia sifuri, kutokana na kudorora kwa uwekezaji na msaada wa kitaasisi.

Hayo ni kwa mujibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, kupitia ripoti yake ya ukaguzi wa ufanisi ya mwaka wa fedha unaoanzia Julai 2024 hadi Juni 2025. Tathmini ikifanywa katika majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya.

Ripoti hiyo, inaweka wazi kuwa hali hiyo inasababishwa na udhaifu katika upangaji na uratibu wa mamlaka zinazohusika na usafiri na kukosekana kwa mikakati madhubuti ya usafiri mijini itakayowezesha uhimilivu na uboreshaji wa huduma rasmi za umma.

“Huduma za usafiri wa mijini katika majiji makubwa, nilibaini kuwa uhakika wa huduma hizo uliathiriwa na kuenea kwa shughuli zisizo rasmi ambazo hazikuwa na ratiba maalumu wala viwango vya huduma vinavyodhibitiwa,” amesema kupitia ripoti hiyo.

Kwa sababu hiyo, amesema watumiaji wa usafiri huo mara nyingi walikumbana na muda wa kusubiri usiotabirika na hali mbaya ya vyombo vya usafiri.

Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni leo Aprili 10, 2026, CAG anasema alibaini mfumo wa utoaji leseni na udhibiti wa watoa huduma unavutia watoa huduma wasio rasmi wa usafiri wa mijini.

Aidha, alibaini Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), imekuwa ikitoa leseni kwa watoa huduma za usafiri wa mijini wanaotumia vyombo vyenye uwezo mdogo wa kubeba, abiria zikiwemo bajaji na pikipiki kinyume na Aya 5.7.2.2 ya Sera ya Taifa ya Usafirishaji ya mwaka 2003.

Aya hiyo, amesema inahimiza usafiri wa umma wa watu wengi kwa kutilia mkazo uingizaji na utoaji wa leseni kwa magari ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 30 kwa mabasi madogo hadi 90 kwa mabasi makubwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uchambuzi wa taarifa za leseni za usafirishaji kwa robo ya nne, ukijumuisha miaka ya fedha 2020/21 hadi 2024/25 ulionyesha usafiri wa umma wa watu wengi haukusajiliwa wala kupewa leseni.

“Hata hivyo, Latra imekuwa ikitoa leseni kwa watoa huduma za usafiri wa umma wenye vyombo vyenye uwezo mdogo, jambo lililosababisha ongezeko la asilimia 95 kufikia mwaka wa fedha 2024/25,” imeeleza ripoti hiyo.

Imekwenda mbali zaidi na kubainisha, kati ya mwaka wa fedha 2020/21 na 2024/25, usajili wa pikipiki uliongezeka kwa asilimia 145 kutoka 18,408 hadi 45,078, na kuzifanya kuwa aina ya usafiri wa mijini uliopewa leseni zaidi.

Kupungua daladala, mwendokasi

Ripoti hiyo inaeleza, kwa kupungua magari ya huduma za jamii kwa asilimia 55 na daladala kwa asilimia 19, huduma za usafiri wa mabasi yaendayo haraka ilishuka hadi asilimia sifuri, ikiashiria uwekezaji mdogo na usaidizi usioridhisha wa kitaasisi.

“Nilibaini kuwa hali hii ilitokana na upangaji na uratibu usiojitosheleza miongoni mwa Latra na kukosekana kwa mikakati jumuishi ya usafiri wa mijini ili kuwezesha uhimizaji na uboreshaji huduma rasmi za umma,” imeeleza ripoti hiyo.

Matokeo yake, ripoti inaeleza miji mikubwa inakabiliwa na hali mbaya ya mchanganyiko wa magari barabarani, inayosababisha msongamano, muda mrefu wa kusafiri na ongezeko la ajali za barabarani, mambo ambayo huwa yanaathiri upatikanaji wa usafiri bora na salama mijini.

“Mapitio yangu ya utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Usafiri 2020/21 hadi 2024/25 katika majiji ya Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, na Mwanza yalibaini ucheleweshaji wa mara kwa mara, usimamizi usioridhisha, ukosefu wa utengamano na utekelezaji usioridhisha wa hatua zilizopangwa.

“Juhudi muhimu, ikiwemo upanuzi wa miundombinu ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam, kuwapo kwa njia maalumu za usafiri wa umma, kuwapo kwa vituo vikuu vya usafiri vinavyounganisha njia mbalimbali, mipango ya kupunguza msongamano na uunganishaji wa mfumo wa barabara na vivuko, hazikutekelezwa kikamilifu,” imesema.

Hali hiyo, amesema ni kinyume na matakwa ya aya ya 2.3 na 2.4 ya Sera ya Taifa ya Usafirishaji ya mwaka 2003, inayotaka mipango kabambe ya usafiri wa mijini iwiane na mikakati ya kitaifa ya usafiri ili kuhakikisha mifumo jumuishi, yenye ufanisi na endelevu.

Upungufu huo pia, Kichere amesema unajumuisha miradi ambayo haijatekelezwa kama njia maalumu za usafiri wa umma, muunganisho wa mifumo ya usafiri na ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi iliyopangwa.

Ametolea mfano kuunganisha barabara na kivuko jijini Mwanza na utekelezaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka awamu ya pili jijini Dar es Salaam.

Upungufu huo, CAG anasema ulitokana na kutotafsiriwa ipasavyo kwa Sera ya Taifa ya Uchukuzi ya mwaka 2003 na mipango ya Taifa ya usafiri kuwa mipango inayotekelezeka katika ngazi ya miji na kutoingizwa kwa vipaumbele katika hatua za mipango mikuu.

“Kukosekana kwa uwiano huo kulisababisha msongamano wa kudumu, upatikanaji mdogo na kuongezeka kwa huduma zisizo rasmi za usafiri,” amesema.

Katika ripoti hiyo, CAG Kichere anasema alibaini huduma za usafiri katika miji hiyo hazikidhi mahitaji ya idadi ya watu inayoongezeka, huku kukiwa na changamoto katika upatikanaji wa usafiri wa uhakika na gharama nafuu.

Pia, amebaini miundombinu ya usafiri iliyopo haikusaidia ukuaji wa mahitaji ya kiteknolojia yanayoweza kutokea katika sekta ya usafirishaji.

Aidha, ameeleza upanuzi na uboreshaji wa miundombinu haukufanyika kikamilifu, ili kuendana na kasi ya ukuaji wa mji, ongezeko la umiliki wa vyombo vya usafiri na ongezeko la matumizi ya mifumo ya Tehama.

“Hii ilikuwa kinyume na matakwa ya Sera ya Taifa ya Uchukuzi (2003), Mpango Mkakati wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (2021–2025) na lengo la 11 la Malengo ya Maendeleo Endelevu,” amesema.

Kichere, amesema katika mapitio yake ya taarifa ya Latra kuhusu ya utendaji katika sekta ya uchukuzi ya mwaka 2023, alibaini ukuaji wa mji wa Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya haukulingana na uwekezaji katika miundombinu ya usafiri.

“Kati ya mwaka 2020 na 2023, eneo la majiji haya liliongezeka kwa asilimia 27 wakati ongezeko la miundombinu mipya ya barabara za mjini lilikuwa ni asilimia 8.5,” amesema.

Amesema wakati miji inapanuka kwa kiwango cha asilimia 21, asilimia 25.8 na asilimia 24.2, kwa miji ya Dar es Salaam, Arusha na Mbeya mtawalia, maendeleo ya miundombinu yake hayakuendana na kasi ya ukuaji wa miji hiyo.

Sababu ya tatizo hilo, amesema ni kutowapo kwa mipango jumuishi ya miji, alibaini Latra, mamlaka za serikali za mitaa, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (Tarura) hazikushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya mindombinu.

“Mgawanyiko huu unasababisha kutofanyika kikamilifu kwa uboreshaji wa miundombinu ya usafiri katika miji,” amesema.

Aidha, amesema changamoto hizo zilisababisha usafiri wa umma kuendelea kukabiliwa na msongamano na ufikiaji mdogo katika maeneo mapya ya miji.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema wanasajili pikipiki na bajaji zaidi kwa sababu ndilo eneo lenye wawekezaji wengi.

Urahisi wa gharama za kununua pikipiki na bajaji, amesema unafanya watu wengi wawekeze huko zaidi kuliko kwenye daladala, hivyo hata mahitaji ya usajili yanaongezeka katika vyombo hivyo vya usafiri.

Suluo, amesema kwa kuwa bodaboda na bajaji wana uhuru wa kutoza nauli bila kupangiwa, ndiyo maana watu wengi wanaamua kuwekeza huko.

“Watu wanautumia vibaya uhuru wa kutoza nauli kwenye bodaboda na bajaji. Wengi wanatoa huduma kama daladala na hata baadhi ya wamiliki daladala wanauza wananunua bodaboda na bajaji,” amesema.

Hata hivyo, amesema kwa kuwa CAG ameweka wazi mambo kadhaa, ni nafasi ya kwao kufanya tathmini na kujua maeneo ya kuboresha ili kuondoa changamoto zilizopo.