WAKATI Fountain Gate ikithibitisha kuachana na Kocha wake Mohamed Laizer, uongozi wa timu hiyo umetangaza kumvuta kikosini Fredi Felix ‘Minziro’ kuiongoza timu hiyo kwa mechi zilizobaki Ligi Kuu.
Hivi karibuni kumekuwapo na taarifa zisizo rasmi za Laizer kuachana na timu hiyo na leo Aprili 10, imethibitishwa rasmi pande zote kukubaliana kuachana.
Minziro ambaye alikuwa Big Man ya Championship, anajiunga na timu hiyo akitarajia kusaidiana na Mathias Wandiba aliyekuwa akiiongoza Gunners nayo ya Championship kwa ajili ya kuiweka salama timu hiyo ya Ligi Kuu.
Wawili hao wanakutana kwa mara nyingine baada ya kuachana kwa takribani msimu mmoja tangu walipofanya kazi pamoja katika kikosi cha Pamba Jiji ya jijini Mwanza kabla ya kila mmoja kutafuta ‘chaka’ lake.
Pia makocha hao walishafanya kazi katika kikosi cha Mbeya City kabla ya Wandiba kutimkia Geita Gold kisha kufufukia Pamba Jiji katika kikosi cha timu ya vijana (U20) ambapo Gunners waliamua kumvuta na sasa wanakutana tena.
Taarifa iliyotolewa na uongozi wa timu hiyo, umesema Minziro atakuwa Kocha Mkuu akisaidiana na Wandiba, huku Aboubakari Francis akibaki na majukumu yake ya kocha msaidizi na Hnery Joseph kocha wa viungo kikosini humo.
Taarifa hiyo imeeleza uongozi unaamini kupitia uzoefu wa kocha huyo na staa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, weledi na kujitolea kwa benchi hilo, timu itaimarika zaidi na kufikia malengo yake kwenye mashindano.
“Wakati huohuo tunathibitisha kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Laizer, Fountain Gate inamtakia kila la heri katika majukumu yake, tunaendelea kujidhatiti katika kujenga timu kuwa imara, ushidani na kuleta mafanikio kwa mashabiki na wadau wake,” imesema taarifa hiyo.
Minziro anatua kikosini humo akiwa ameiacha Bigman nafasi ya saba kwa pointi 27, huku msaidizi wake akiiacha Gunners nafasi ya 10 kwa pointi 23 baada ya michezo 21 kwa timu hizo kwenye Championship.
Mwisho………..
