ASKARI ALIYETOA TAARIFA KWA WAZIRI MKUU YUPO NA ANAENDELEA NA KAZI.

*****

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limekanusha taarifa zilizokuwa zikisambaa kwenye Mitandao mbalimbali ya Kijamii nchini zikieleza kuwa Mkaguzi msaidizi wa Polisi Nassoro Mana, aliyetoa kero yake mbele ya Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ametekwa na kupotea baada tu ya kueleza kero yake kwa Waziri Mkuu wakati wa ziara yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Salim Morcase katika taarifa yake kwa Vyombo vya habari leo Ijumaa Aprili 10, 2026 amesema taarifa hiyo ilionekana kwa mara ya kwanza ikionesha watangazaji wa Kituo cha redio cha Kyela Fm wakitangaza jambo hilo ambalo si la kweli na Askari huyo yupo kazini na anaendelea kutekeleza wajibu wake.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani lingependa kueleza kuwa taarifa hiyo si ya kweli na ufafanuzi wake ni kwamba askari huyo alikuwa Mkoa wa Tanga akihudhuria mashtaka ya Kijeshi kuanzia Februari 15, 2026 mpaka yalipokamilika na kutumwa kwenye Mamlaka yenye maamuzi juu yake. Taarifa inayosambazwa kwenye Mitandao haina uthibitisho kutoka Jeshi la Polisi.” Amenukuliwa Kamanda Morcase.

Polisi pia imebainisha kuwa familia ya Mkaguzi huyo wa Polisi inafahamu suala hilo kwani Mke wake alifika Mkoani Tanga na kuonana na mumewe Aprili 08, 2026, Askari huyo pia alipewa kibali cha kutoka Mkoani Tanga kwenda Pwani kwenye Kituo chake cha kazi na Aprili 10, 2026 Askari huyo pia alirejea kwa Kamanda wa Polisi Pwani ambaye alimuelekeza kurejea Chalinze, Kuendelea kutekeleza majukumu yake.

Katika taarifa hiyo, Polisi pia imetoa rai kwa wananchi na waandishi wa habari kutotumia vibaya mitandao ya kijamii na Vyombo vyao vya habari kwa kutoa taarifa za uongo na kuleta taharuki kwa wananchi na Viongozi, Polisi ikisisitiza kuchukua hatua kali za kisheria kwa wanaokiuka sheria, kanuni na taratibu zilizopo nchini.