Serikali yatuma wataalamu wa jiolojia kuchunguza ardhi kupasuka Same

Same. Ikiwa zimepita siku tisa tangu gazeti hili kuripoti hali ya taharuki, hofu na sintofahamu iliyotokana na ardhi kuanza kutitia na kujipasua katika Kijiji cha Marieni, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, hali hiyo imeanza kupata ufumbuzi baada ya Serikali kuchukua hatua.

Kutokana na hali hiyo, serikali tayari imetuma wataalamu wake kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Nchini (GST) kufika katika eneo hilo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha tatizo hilo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Mpaka sasa, kaya 10 zimeyakimbia makazi yake katika kijiji hicho huku moja ya nyumba za ibada ikishindwa kutumika, baada ya kutengeneza nyufa zilizosababishwa na hali hiyo.

Kufuatia hali hiyo, baadhi ya wananchi ambao maeneo yao yameathiriwa wamehamisha familia zao pamoja na mali zao na kwenda kuhifadhi kwenye maeneo ambayo wamepata hifadhi ya muda wakisubiri muafaka wa serikali.

Hata hivyo, Mwananchi lilipotembelea eneo hilo, Aprili Mosi, 2026, lilishuhudia moja ya makanisa likiwa limeachwa wazi baada ya kuta zake kupasuka kwa nyufa kubwa, huku sakafu yake ikionyesha dalili za kutitia

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 10, 2026, Mtaalamu wa Jiologia kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Nchini, Gabriel Mbogoni amesema tayari serikali imetuma wataalamu wake katika Kijiji hicho kufanya uchunguzi wa kitaalamu zaidi katika eneo hilo.

“Tayari serikali imeanza kuchukua hatua na imetuma wataalamu wake kufika eneo la tukio kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Nchini kuchunguza tukio hilo,”amesema Mbogoni

Aidha, amesema kwasasa hawawezi kutoa taarifa yoyote kuhusiana na tukio hilo licha ya kufika eneo la tukio mpaka hapo watakapofanya utafiti kuchunguza changamoto hiyo inasababishwa na kitu gani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji hicho, wameishukuru serikali kwa kuchukua hatua za haraka kufika katika eneo. hilo.

Akizungumza mmoja wa wanachi wa Kijiji hicho, Msafiri Mkodo, ameishukuru serikali kwa kuchukua hatua hizo za haraka na kusema hatua hiyo inaleta matumaini makubwa kwa wananchi ambao wameathiriwa na nyufa hizo.

“Kwa kweli haya ni matumaini makubwa sana kwetu sisi wananchi, kitendo cha serikali kuchukua hatua za haraka mumetufariki sana maana usiku tulikuwa hatulali licha ya kwamba tumehama makazi yetu na kuyaacha,”amesema Mkodo

Mwananchi mwingine, Cathbert Wilfred ameipongeza serikali kwa kufika katika eneo hilo na kuiomba kuangalia namna ya kuwapa msaada wa haraka walioathiriwa katika eneo hilo.

“Tunaishukuru sana serikali kuwa kuchukua hatua za haraka, tunaomba aiangalie namna nzuri ya kuwasaidia waathirika wa tukio hili, ambao baadhi wameyahama makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao,”amesema Mwananchi huyo

Marry Godfrey ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho, amelishukuru Gazeti la Mwananchi kwa kufika katika eneo hilo na kuibua tukio hilo ambalo sasa serikali imeanza kuchukua hatua.

“Tunawashukuru sana Waandishi wa Gazeti la Mwananchi kwa kufika hapa Kijiji kwetu na kutoa taarifa hii ambayo sasa tunaona serikali imeanza kuchukua hatua kutokana na uzito wao wake,”amesema mwananchi huyo.