CAG abaini utekelezaji hafifu wa mapendekezo, yapo yaliyofikisha miaka 19

Dar es Salaam. Wakati Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akibainisha upungufu na kutoa mapendekezo katika ripoti za ukaguzi za mwaka 2024/25, pia amebainisha utekelezaji hafifu wa mapendekezo aliyoyatoa miaka ya nyuma, ambapo baadhi yake yamefikisha hadi miaka 19 bila kutekelezwa.

Ripoti ya CAG iliyowasilishwa bungeni leo Aprili 10, 2026 inaonyesha kuwa kati ya mapendekezo 10,391 yaliyotolewa kwa mashirika ya umma na taasisi 225, ni asilimia 35 pekee yaliyotekelezwa kikamilifu huku asilimia 47 yakiwa bado katika hatua za utekelezaji.

“Asilimia 16 hayajatekelezwa au yamejirudia tena, na asilimia 2 yamepitwa na wakati,” imeeleza ripoti hiyo.

Amebainisha kwamba hali hiyo inaacha asilimia 63 ya mapendekezo bila kukamilika, ikionesha ucheleweshaji wa marekebisho na udhaifu wa nidhamu ya uwajibikaji katika taasisi za umma.

CAG Kichere amesema baadhi ya taasisi zimeacha mapendekezo bila kushughulikiwa kwa zaidi ya miaka 17, zikiwemo Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), Kitengo cha Usimamizi wa Hifadhi za Bahari, Bodi ya Korosho Tanzania, Kampuni ya Meli ya Tanzania (Tashico) na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta).

Katika taasisi hizo, changamoto kama umiliki wa mali, madeni yasiyolipwa, mapato yasiyokusanywa na udhaifu wa mifumo ya udhibiti wa ndani zimeendelea kujirudia bila ufumbuzi wa kudumu.

Pamoja na hayo, ripoti inaonesha kuwa kati ya hati 225 zilizotolewa, hati 221 sawa na asilimia 98 zilikuwa zinazoridhisha, hati tatu zilikuwa na shaka, na taasisi moja haikupata maoni.

Taasisi zilizopata hati zenye shaka ni Bodi ya Korosho Tanzania, Kiwanda cha Dawa cha Keko na Bodi ya Chai Tanzania, huku Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Kyela-Kasumulu ikikosa hati kabisa.

Hata hivyo, CAG ameonya kuwa hati safi za ukaguzi si kipimo cha moja kwa moja cha utendaji bora, akibainisha kuwepo kwa udhaifu katika utawala, ununuzi, usimamizi wa mapato na mifumo ya udhibiti wa ndani.

Wakati huohuo, CAG amebainisha katika ripoti ya ukaguzi wa Serikali Kuu kuwa baadhi ya hoja za ukaguzi za miaka iliyopita na mapendekezo yake husika zimeendelea bila kutatuliwa kwa muda mrefu, huku baadhi zikiendelea hadi miaka 19, jambo linaloakisi udhaifu katika mifumo ya ufuatiliaji na ucheleweshaji wa kutekeleza hatua za marekebisho.

Aidha, amebainisha kuwa pale udhaifu unapoendelea kuwepo licha ya mabadiliko ya maofisa masuuli, timu za menejimenti au uongozi wa taasisi, upungufu huo huwa wa kitaasisi badala ya kuwa wa mtu mmoja mmoja, ukionyesha vikwazo vya kimfumo katika udhibiti badala ya upungufu wa kiutawala uliojitenga.

CAG amesema katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Sh17.8 milioni zilizotokana na hundi za makusanyo ambazo hazijalipwa kwa miaka 19 (tangu 2006/07) zinasubiri idhini ya Mlipaji Mkuu wa Serikali.

Vivyo hivyo, Sh50.6 milioni zinazotokana na bidhaa zilizoingizwa nchini zinasubiri kukamilika kwa taratibu na nyaraka muhimu, na zimebakia bila kukamilishwa kwa miaka 19 (tangu 2006/07) zikisubiri idhini ya kufutwa katika kumbukumbu za taarifa za fedha.

Kwa mwaka 2008/09, amebainisha Sh7.24 bilioni za madeni ya kodi bado hazijalipwa baada ya miaka 17, wakati kwa mwaka 2010/11, Sh1.25 bilioni za madeni ya kodi na Sh281.99 milioni za kodi zilizokadiriwa bado ziko katika uhakiki au rufaa baada ya miaka 15, huku menejimenti ikitakiwa kutoa ushahidi unaounga mkono na kutatua migogoro iliyoko mbele ya Bodi ya Rufaa za Mapato ya Kodi.

Vilevile, katika Idara ya Uhamiaji (Fungu 93, 2007/08), amebaini Sh40.84 milioni za mapato ambayo hayakuingizwa kwenye akaunti yameendelea bila kutatuliwa kwa miaka 18, huku menejimenti ikisubiri idhini ya Hazina kufuta kiasi hicho kama deni baya kufuatia kifo cha mtumishi aliyewajibika mwaka 2011.

“Ninapendekeza kwamba Serikali, kupitia Mlipaji Mkuu wa Serikali na Maafisa Masuuli husika, ianzishe mfumo wa kimuundo wa utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na maagizo ya PAC ili kuimarisha ufuatiliaji wa mapendekezo ya ukaguzi na kuhakikisha utekelezaji wa wakati wa hoja za ukaguzi pamoja na maagizo ya PAC,” amebainisha CAG.