Elimu ya mabadiliko ya tabianchi yasisitizwa kwa wenye ulemavu

Dar es Salaam. Taasisi ya Furaha ya Wanawake Viziwi Tanzania (Fuwavita), imesema elimu ya mabadiliko ya tabianchi kwa wenye ulemavu ni muhimu kwani yanapotokea majanga huathiri kundi hilo moja kwa moja bila kupata msaada.

Imesema kunapotokea ukame au mafuriko huongeza mzigo wa kutafuta chakula na hatari kwa wenye ulemavu hivyo maarifa ndiyo yatawasaidia kukabiliana na hatari iliyo mbele yao.

Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 10, 2026 jijini Dar es Salaam na mwanzilishi wa Fuwavita, Aneth Isaya wakati akifua mafunzo ya uongozi na uelewa wa mabadiliko ya tabianchi kwa wanawake 50 wenye ulemavu Dar es Salaam.

Anneth amesema mabadiliko ya tabia ya nchi, hutokea wakati wotewote, hivyo ni lazima kundi la watu wenye ulemavu wapatiwe elimu sahihi ya chanzo cha mabadiliko hayo na namna ya kukabiliana nayo.

“Tutaendelea kushirikiana na Serikali ili kundi la watu wenye ulemavu wawe na nafasi ya kuwasiliaha maoni yao ndani ya Serikali kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabia ya nchi,” amesema.

Amesema katika kuimarisha ushirikishwaji wa makundi maalumu kwenye mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, tayari wamezindua programu ya Haki ya Tabianchi kwa kushirikiana na Taasisi ya African Alliance for Women with Disabilities in Climate Action (AWAC Alliance).

“Yote haya yanataribiwa na Kituo cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa Ujumuishi kwa Afrika Endelevu (ICCASA) kupitia Mradi wa STREVOW, unaolenga kukuza sauti, uongozi na vipaumbele vya wanawake wenye ulemavu katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo ya Ujasirimali Fuwavita Victoria Philemon amesema watu wenye ulemabu ni miongoni mwa wale wanaoathirika wakati wa hali ya dharura.

Amesema changamoto za mabadiliko ya tabianchi, zinahitaji suluhisho la pamoja na la muda mrefu ili kuhakikisha fursa sawa na upatikanaji wa rasilimali kwa wote, bila kumwacha mtu yeyote nyuma,

“Ni muhimu kuwa na mbinu shirikishi ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanajumuishwa kikamilifu katika juhudi za maendeleo kitaifa na kimataifa,”amesema.

Naye Faith Dikunda wa Shirika la ICASA amesema wameshirikiana Fuavita kuhamasisha ushirikishaji wa wanawake wenye ulemabvu kwenye uongozi na kazi za kila siku zinazohusu mabadiliko ya tabianchi.

 “Kuna changamoto nyingi ambazo wanawake wenye ulemavu wanapitia kutokana na hali zao, pia hawawezi kupata mawasiliano kwa urahisi kwahiyo zile changamoto wanazopitia makundi haya na suluhu wanazopendekeza tunakwenda kuzisikiliza na kuzifanyia kazi,” amesema.

Faith amesema ni muhimu mikutano yote inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi katika jamii watu wenye ulemabu wanashirikishwa katika kupanga, kudhibiti na kukabiliana na maafa. 

Kanuni za Usimamizi wa Maafa za mwaka 2022 zinaelekeza kuzingatia mahitaji yao wakati wa kufanya tathmini ya madhara na mahitaji kwa ajili ya kukabiliana na maafa na kurejesha hali.

Pia, Sheria ya Usimamizi wa Maafa Sura 242 imeweka uwakilishi wa watu wenye ulemavu kwa Jukwa la Taifa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa.

Vilevile, Kanuni za Usimamizi wa Maafa za mwaka 2022 zinaelekeza kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu wakati wa kufanya tathmini ya madhara na mahitaji kwa ajili ya kukabiliana na maafa na kurejesha hali.