Asilimia 59 fedha za mikopo ya halmashauri hazijafika kwa wahusika

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikijizatiti kuwawezesha wananchi kiuchumi, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini dosari katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kutoka halmashauri, ikibainisha asilimia 59 ya fedha hizo hazikufika kwa walengwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya ukaguzi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka wa fedha 2024/25, jumla ya Sh1.82 bilioni ziliidhinishwa na kuhamishwa kwenye benki na halmashauri saba kwa ajili ya kukopeshwa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Hata hivyo, ripoti hiyo imebainisha katika fedha zote hizo, ni asilimia 41 pekee ndizo zilizotolewa kwa vikundi vilivyokidhi vigezo, huku zaidi ya Sh1.07 bilioni zikiwa hazijatumika na hivyo kutowafikia walengwa.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni leo Ijumaa, Aprili 10, 2026, imeeleza kuwa sababu kuu ya fedha hizo kutotolewa ni baadhi ya vikundi vilivyopendekezwa kutokidhi vigezo vya ukopeshwaji vilivyowekwa na benki zilizohusika katika mchakato huo.

Hali hiyo, kwa mujibu wa CAG, imeibua hoja kuhusu uwiano na ubora wa tathmini zinazofanywa katika ngazi ya halmashauri kabla ya kuwasilisha majina ya vikundi kwenye taasisi za kifedha.

Imeelezwa kuwa, halmashauri ndizo zilizopewa jukumu la awali la kupendekeza vikundi vinavyostahili kunufaika na mikopo hiyo, lakini sehemu kubwa ya vikundi hivyo havikupitishwa na benki kutokana na kutokidhi masharti ya kifedha.

Jambo hilo, ripoti hiyo inaeleza linaashiria kuwepo kwa pengo kati ya tathmini ya halmashauri na vigezo halisi vinavyotumika katika utoaji wa mikopo.

Katika muktadha huo, ripoti imeeleza Aprili 2023 Serikali ilisimamisha utoaji wa mikopo hiyo ili kutoa nafasi ya kufanya maboresho ya mfumo wa usimamizi wa mfuko huo, ikilenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi.

Baada ya maboresho hayo, CAG amesema utoaji wa mikopo ulianza tena Julai 2024 kwa mfumo wa majaribio katika halmashauri 10 zilizochaguliwa.

Licha ya hatua hiyo, changamoto zimeendelea kujitokeza. Ripoti inaeleza kuwa halmashauri tano kati ya hizo 10 hazikutoa mikopo yoyote kupitia mfumo wa kibenki katika kipindi cha ukaguzi, kutokana na kuchelewa kusainiwa kwa mikataba ya ushirikiano kati ya halmashauri na benki pamoja na michakato mirefu ya tathmini kabla ya kuwasilisha vikundi.

CAG ameonya kuwa, ucheleweshaji huo na kiwango kidogo cha matumizi ya fedha zilizohamishwa vinaweza kudhoofisha ufanisi wa mfuko huo, kuchelewesha upatikanaji wa mikopo kwa walengwa na hatimaye kupunguza imani ya wadau.

“Aidha, hali hiyo inaathiri uwezo wa mfuko kujiendesha na kudumisha mzunguko wake wa kifedha kutokana na fedha kutokutumika kwa wakati,” imeeleza ripoti hiyo.

Kutokana na changamoto hizo, ripoti imependekeza Tamisemi kuimarisha mfumo wa usimamizi wa mikopo ya kibenki kwa kuhakikisha miongozo ya utoaji mikopo inaidhinishwa kwa wakati na kuwepo kwa uwiano kati ya tathmini za halmashauri na vigezo vya benki.

Pia, imesisitiza umuhimu wa kurasimisha mikataba kati ya halmashauri na taasisi za kifedha kwa wakati ili kuepuka ucheleweshaji usio wa lazima.

Mbali na hilo, ripoti imebaini uwepo wa vikundi vinavyotiliwa shaka, maarufu kama vikundi hewa.

“Katika Jiji la Dodoma, vikundi vyenye thamani ya Sh188 milioni vilibainika kutopatikana, kuwa na mawasiliano yasiyo sahihi au kukosa ushahidi wa kuendelea na shughuli zao,” imesema.

Pia, katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, kulikuwa na limbikizo la Sh29.5 milioni kutoka kwa vikundi vinne ambavyo havipo tena.

Kutokana na hali hiyo, CAG amependekeza Tamisemi kufanya uchunguzi wa kina kubaini uhalali wa vikundi vyote vinavyohisiwa kuwa hewa, kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wazembe na kutoa notisi za madai ya siku 30 kwa wadaiwa sugu.

Hatua hizo, kwa mujibu wa ripoti, ni muhimu katika kurejesha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha malengo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi yanafikiwa kikamilifu.