Sido kuwakutanisha pamoja wajasiriamali | Mwananchi

Shinyanga. Zaidi ya Wajasiriamali 600 kutoka Tanzania bara na visiwani wanatarajia kushiriki maonesho ya kitaifa ya Shirika la maendeleo la Viwanda vidogo (Sido) ikiwa ni hatua ya kuwawezesha kuonyesha bidhaa zinazozalishwa nchini kwa kutumia teknolojia na kuinuwa viwanda vidogo.

Hayo yameelezwa leo Aprili 10, 2026 na Mkurugenzi mkuu wa Sido Profesa Silyvesta Mpanduji wakati wa mkutano na waandishi wa habari ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maonesho ya Sido kitaifa yatakayofanyika Wilayani Kahama Oktoba 21 hadi 30 na kufungua fursa za kiuchumi kwa wajasiriamali.
Amesema maonesho hayo yatakuwa ya tano kufanyika ambapo mara ya mwisho yalifanyika Mkoani Njombe mwaka 2023 ambayo yalikuwa ya nne,ambayo yamelenga kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wakati ili kuwawezesha watanzania kufahamu teknolojia ambao wanaweza kuzitumia kuanzisha viwanda vidogo.

“Mwaka huu maonesho ya tano ya Sido yatafanyika Wilaya ya Kahama viwanja vya Magufuli na yatawakutanisha wajasiriamali wadogo na wakati ,wazalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na viwanda vidogo na vya kati nchini pia sekta za serikali na binafsi na wadau wa maendeleo walioko sekta ya viwanda”amesema Mpanduji.

Kaimu Katibu tawala Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi amesema vigezo vilivyotumika maonesho hayo kupelekwa Kahama ni pamoja na mji huo kukuwa kwa kasi na kuwa kitovu cha biashara kwa kanda ya ziwa hali ambayo inachochea ukuaji wa uchumi na kuleta maendeleo.

Ametoa wito kwa wanawake na vijana kujifunza teknolojia mbalimbali kupitia Sido ili kuanzisha viwanda vidogo vitakavyowawezesha kuinuwa uchumi wao na kuchangia pato la taifa pamoja na kuendelea kuongeza ujuzi na ubunifu wa vitu mbalimbali.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, John Mwela amesema jukumu lao kubwa ni kuwaandaa vijana ili waweze kujitegemea kuanzia ngazi ya familia na pia kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali.

Mdau wa Sido, Silvia Silivery kutoka kampuni ya Given wear amesema wamejipanga kutumia maonesho ya wajasiriamali kupata teknolojia mpya na kukuza biashara zao ikiwa ni pamoja na kutumia fursa zilizopo kuanzisha viwanda.