MASHABIKI wa Simba wanalia na timu hiyo kuendelea kuangusha pointi Ligi Kuu Bara, baada ya juzi kutoka suluhu na TRA United, mjini Arusha, huku ikimtegemea mshambuliaji mmoja, Selemani Mwalimu.
Ni kutokana na hilo, mastraika ndio wanaoweza kuinyima ubingwa timu hiyo endapo itaendelea kupoteza ubora wa kuamua mechi kupitia eneo hilo la mwisho ambalo ndilo mahususi kwa ajili ya kupata mabao, japo yanaweza pia kupatikana kwa wachezaji wa maeneo mengine.
Iko hivi, Simba imejitibulia na licha ya kupoteza mechi moja na kuangusha pointi tatu, timu hiyo imeangusha zingine 12 kwa kupata sare sita, nne ni zile walizoshindwa kufunga hata bao moja.
Simba imepata sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar na Pamba Jiji, pia sare tasa ni zile dhidi ya Dodoma Jiji, Yanga, Azam FC na ya juzi dhidi ya TRA United ambazo zimezidi kutibua matumaini ya ubingwa kwenye timu hiyo.
Kinara wa ufungaji Simba ni mshambuliaji Seleman Mwalimu ‘Gomez’ mwenye mabao sita hadi sasa lakini ukiondoa nguvu yake, wekundu hao wamekosa mtu mwingine bora kwenye ufungaji na jukumu likihamishiwa kwa viungo na mabeki kutafuta mabao.
Kando ya Mwalimu, wafungaji wengine kwenye mechi za Simba ni Jonathan Sowah mwenye mabao matatu lakini akiwa nje ya kikosi hicho kutokana na uamuzi wa mabosi wa klabu hiyo kumsimamisha akilingana na beki wa kati, Rushine De Reuck huku viungo wapya, Anicet Oura na Libasse Gueye wakiwa na mabao mawili kila mmoja.
Simba kutokufunga hakuna lawama kwa benchi la ufundi kutokana na kikosi hicho kinatengeneza nafasi, lakini ubora wa umaliziaji ndiyo unainyima timu hiyo mabao ikitegemea nguvu kubwa ya Mwalimu pekee.
Wakati Simba ikipambana na kuboresha kikosi hicho, mabosi wa Simba watajilaumu wenyewe kwa kushindwa kutafuta mshambuliaji bora kwenye timu hiyo wakati wa dirisha la usajili wa Januari, ikimuongeza kinda Baraka Mwangosi pekee ambaye ameshindwa kuwa na nguvu stahiki ya kuhimili presha ya mechi za wekundu hao.
Kwenye usajili wa Januari licha ya Simba kufanya vizuri lakini hadi sasa nyota walioongezwa wamefunga mabao matano pekee yakiwemo ya Oura, Gueye ambao kila mmoja amefunga mawili huku moja likifungwa na beki wa kati, Ismael Toure.
Kuonyesha benchi la ufundi la Simba linapata shida na ubora wa safu ya ushambuliaji, kocha wa timu hiyo Steve Barker mara mbili tofauti amekuwa na mahesabu yaliyoshtua, akitangulia kumpanga Inno Loemba kucheza kama mshambuliaji wa kati.
Mbali na hilo, wakati Simba ikicheza ugenini dhidi ya TRA, kocha huyo alifanya uamuzi mgumu akimtoa Mwalimu kisha nafasi yake akamuingiza beki kinda, Hussein Mbegu dakika ya 85 wakati wekundu hao wakitafuta bao la kuamua mechi.
Wakati ligi inaendelea Mwanaspoti linafahamu Simba ipo sokoni ikitafuta washambuliaji wa maana kwa hesabu za msimu ujao ikielezwa tayari kuna wawili ambao inapambana nao kutafuta saini zao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori, alithibitisha kazi ya kuunda kikosi hicho inaendelea na harakati za usajili zimeshaanza kutafuta watu bora zaidi kulingana na mahitaji ya timu hiyo.
“Usajili tulishaanza na tunaendelea kutafuta wachezaji wazuri ambao tunaamini watakuja kukipa thamani zaidi kikosi chetu. Hadi sasa tuna timu nzuri, lakini kuna maeneo lazima tuyaongezee nguvu,” amesema Magori
