WAWAKILISHI wa Championship, TMA FC ya jijini, Arusha, itakuwa na kibarua kigumu leo kuisaka rekodi mpya ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la CRDB, itakapocheza dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Yanga.
Katika mechi hiyo ya hatua ya 16 bora itakayopigwa Kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, jijini, Dar es Salaam, kuanzia saa 12:30 jioni, inazikutanisha timu hizo zikiwa na mwenendo mzuri, tangu mashindano hayo yalipoanza msimu wa 2025-2026.
TMA ilianza kampeni za michuano hiyo kwa ushindi mnono baada ya kuichapa Newala FC ya Mtwara mabao 7-0, katika hatua ya 64 na kufuzu kibabe, huku hatua iliyofuata ya 32, bora ikaishangaza maafande wa Tanzania Prisons kwa kuichapa bao 1-0.
Ushindi wa mabao 7-0, ulimfanya, Fredy Masota wa TMA, kuweka rekodi ya kufunga ‘Hat-Trick’, sawa na Yassin Mgaza (Dodoma Jiji), Omary Ramadhan (Transit Camp), Paul Peter (JKT TZ), Jacob Masawe (Namungo FC) na Laurindo Dilson Maria ‘Depu’ wa Yanga.
Kwa upande wa Yanga ambao ni wenyeji, ilianza kampeni za michuano hiyo kwa kuichapa Cosmopolitan mabao 2-0, katika hatua ya 64 bora, huku hatua ya 32 bora, ikaitembezea kichapo cha fedheha cha mabao 7-1, maafande wa Polisi Tanzania ya Moshi. Licha ya mwenendo mzuri wa TMA katika michuano hii msimu huu, ila timu hiyo itakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na Yanga, ambayo hadi sasa haijawahi kupoteza mechi ya Kombe la CRDB, tangu mara ya mwisho ilipochapwa na watano zao Simba.
Mara ya mwisho Yanga kupoteza mechi ya Kombe la CRDB, ilichapwa bao 1-0, dhidi ya Simba, lililofungwa na, Mganda Taddeo Lwanga, katika fainali ya msimu wa 2020-2021, iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma, Julai 25, 2021.
Tangu, Julai 25, 2021, hadi leo hii Aprili 11, 2026, Yanga imefikisha siku 1,721, bila ya kupoteza, sawa na miaka minne, miezi nane na siku zake 17, ikitumia sekunde milioni 148,694,400, dakika 2,478,240, saa 41,304 au wiki 245 na siku sita.
Kwa maana hiyo, TMA inaingia na kibarua cha kuivunja rekodi ya Yanga iliyoiweka kwa miaka minne na tangu Julai 25, 2021, kimecheza jumla ya mechi 26, za Kombe la CRDB na kushinda zote, ikiwa ni mtego mkubwa kwa wapinzani.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Mkuu wa TMA FC, Haji Ali Nuhu, amesema anatambua anaenda kukutana na timu kubwa na yenye wachezaji bora na wenye uzoefu, ingawa, malengo yao ni kucheza kwa nidhamu ya kuwaheshimu, hususan eneo la kujilinda.
“Hakuna asiyejua ubora wa mpinzani tunayeenda kukutana naye, tutacheza kwa kuwaheshimu kwa maana ya kujilinda vizuri na wakati huohuo tunawashambulia kwa kuwashtukiza, malengo ni kufuzu, japo, hata hapa tulipo ni heshima pia,” amesema Nuhu.
