BAADA ya mzunguko wa 14 wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) kutamatika juzi, Alhamisi, ligi hiyo itasimama siku 11 kwa ajili ya mapumziko mafupi ya ratiba ya mechi za kimataifa.
Ligi hiyo itasimama kwa takribani siku 11 kupisha dirisha la mechi za kimataifa lililoanza Aprili 7 hadi 18. Hivyo WPL inatarajiwa kurejea Aprili 21 kwa mechi moja ya Tausi FC dhidi ya Bilo FC kabla ya michezo mingine mitano kuchezwa Aprili 22.
Baadaye, raundi ya 15 itapigwa Aprili 25 na 26, kisha ligi itasimama tena kupisha mechi za kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 20 zitakazochezwa kati ya Mei 1 hadi 10 kisha ligi itarejea tena Mei 14.
Lakini kabla ya mapumziko hayo mechi za mzunguko wa 14 zimeshtua baadhi ya wafuatiliaji wa soka la wanawake baada ya Yanga Princess kupoteza mechi muhimu dhidi ya Tausi FC kwa mabao 2-0 na mechi iliyowapa faida Simba Queens katika mbio za ubingwa.
Kabla ya mechi hiyo timu hizo zilikuwa zinatofautiana pointi moja, Simba ilikuwa kileleni huku Yanga ikiwa nafasi ya pili.
Raundi ya 14 imekuwa na matokeo ya tofauti na yameathiri kwa kiasi kikubwa mbio za ubingwa.
Simba Queens iliendeleza rekodi yake ya kutopoteza mechi msimu huu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Bunda Queens moja ya timu zilizoonyesha upinzani mkubwa.
Mabao yote matatu yalifungwa na Jentrix Shikangwa, Fasila Adhiambo na Zawadi Usananse.
Mechi nyingine ni ile kati ya Yanga Princess waliopoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Tausi FC matokeo yaliyotingisha nafasi yao. Katika mechi hiyo Yanga hawakuwa wabunifu hasa kwenye eneo la kiungo, viungo wao hawakuwa wabunifu walizidiwa na Tausi ambao walicheza kwa mpango.
Matokeo mengine ni pamoja na Mashujaa Queens kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ruangwa Queens, huku Ceasiaa Queens wakilazimishwa sare ya bila kufungana na Alliance Girls.
Fountain Gate Princess walipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Geita Queens na kuwafanya washuke hadi nafasi ya tano, wakati huo JKT Queens iliendeleza kichapo cha mabao 3-0 kwa Bilo FC.
Baada ya matokeo hayo, Simba Queens inaongoza msimamo ikiwa na pointi 37, wakifuatiwa na Yanga Princess yenye pointi 33. JKT Queens inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 32, huku Alliance ikisogea nafasi ya nne na pointi 20.
Tofauti ya pointi nne kati ya Simba Queens na Yanga Princess sasa imeanza kuonekana kuwa pengo kubwa.
Ingawa bado ligi inaendelea lakini matumaini ya Yanga kuchukua ubingwa yapo kwenye mechi saba zilizosalia timu hiyo inapaswa kuchukua pointi tatu kwa kila mechi.
Mapumziko ya kalenda ya kimataifa yanaweza kuwa na faida kwa timu mbalimbali, hususan kwa Yanga Princess na JKT Queens ambazo zinahitaji kujipanga upya.
Kwa upande wa Simba, mapumziko hayo watayatumia kuimarisha kikosi na kuendelea kulinda nafasi yao kileleni.
Kocha msaidizi wa timu hiyo, Mussa Mgosi anasema: “Tulikuwa na majeruhi baadhi lakini tulipambana na kupata pointi sita ngumu ugenini. Kwa hiyo mapumziko yanaweza kuwa na faida kwa timu kupumzika kidogo na kuangalia wapi tumekosea turekebishe.”
Kocha wa JKT, Kessy Abdallah anasema: “Ligi ya msimu huu ngumu sana hivyo timu zinapopata mapumziko kama hivi inasaidia kuangalia wapi pa kurekebisha ili tuysonge mbele.”
Ligi itakaporejea inatarajiwa kuwa na ushindani zaidi huku kila timu ikisaka pointi tatu muhimu katika mbio za ubingwa. Kwa sasa Simba Queens inaonekana kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kunyakua taji hilo, lakini soka hubeba matokeo yasiyotabirika na hilo linaifanya ligi hii kuendelea kuwa na mvuto mkubwa.
