Global Publishers
April 11, 2026
0 Comments
Ziara ya Rais mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, mjini Juba imeashiria hatua mpya ya kidiplomasia katika kuhuisha mchakato wa amani nchini Sudan Kusini.
Akiwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika kwa Ukanda wa Pembe ya Afrika na Bahari Nyekundu, alikutana na Rais Salva Kiir (pichani) pamoja na viongozi wengine wa serikali kujadili utekelezaji wa Mkataba wa Amani wa mwaka 2018 (R-ARCSS).

Katika mazungumzo hayo, Rais Kiir alisisitiza kuwa mchakato wa amani unaendelea, huku serikali ikiendeleza juhudi za majadiliano jumuishi yanayohusisha pande zote, ikiwemo ambazo hazijasaini makubaliano hayo.
Lengo kuu, amesema Rais Kiir, ni kufikia mwafaka wa kitaifa kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 2026, ambao utakuwa wa kwanza tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 2011.
Ziara hiyo pia ilijumuisha mashauriano na vyama vya siasa kama SPLM-IG, SPLM-IO na SSOA, pamoja na asasi za kiraia, viongozi wa dini na wanazuoni.
Ushirikishwaji huu mpana umeonekana kuwa nguzo muhimu ya kujenga maridhiano ya kudumu, na umepongezwa na wadau wote wa taifa hilo changa.
