Kigali. Alipokea taarifa ile kama ndoto, na ni ndoto ambayo hakuwahi kufikiria ingeweza kuwa kweli.
Hiyo ni baada ya miaka 13 ya majonzi, hofu na sintofahamu, Mchungaji Biramahire Jean Damascene, ambaye ni mchungaji wa Kanisa la Kilokole, anasema alijulishwa kuwa mke wake aliyepotezana naye wakati wa mapigano yaliyosababisha mauaji ya kimbari yaliyochukua maisha ya watu zaidi ya milioni moja Aprili 7, 1994, alikuwa hai.
Damascene ameyasema hayo leo Ijumaa Aprili 10, 2026 alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Kigali nchini Rwanda, ambako Serikali na wananchi wake wameanza maombolezo ya siku 100 ya kuwakumbuka wote waliopoteza maisha katika mauaji hayo huku bendera zote zilizoko nchini humo zikipepea nusu mlingoti.
Kwa sauti yenye hisia, mchungaji huyo anasimulia namna maisha yake yalivyogeuka ghafla wakati vita vilipozuka nchini humo. Anasema akiwa miongoni mwa wanajeshi wa kundi la waasi waliokuwa wakiipinga Serikali, alilazimika kukimbia na kukimbilia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, iliyojulikana wakati huo kama Zaire, baada ya kikundi chao cha mapigano kuzidiwa nguvu na Jeshi la Rwanda.
“Hapo ndipo maisha mapya ya uhamishoni yalipoanza. Yalikuwa ni maisha yaliyojaa hofu, upweke na kutokuwa na uhakika wa kesho yangu,” anasimulia.
Anasema kadiri miaka ilivyokuwa inazidi kusonga, matumaini ya kuja kuonana tena na mkewe sambamba na familia yake yalianza kufifia.
Mchungaji Biramahire Jean Damascene akiwa na mkewe.
Hata hivyo, Damascene anasema ndani yake bado kulikuwa na chembe ya imani kwamba huenda mke wake alikuwa hai.
“Kuna siku nilikutana na jamaa yangu mmoja huko msituni Congo. Huyu nilikuwa ninaishi naye Rwanda. Akaniambia anarudi Rwanda, nikamtuma akanitazamie kama bibi yangu bado yupo,” anasema.
Hata hivyo, anasema tangu alipomtuma huyo jamaa yake aliyemtaja kwa jina la Ndabhaya Nshaseye, muda ulipita bila ya kurudishiwa majibu, hali iliyozidi kumkatisha tamaa.
“Sababu nilimtuma akaniangalizie bibi yangu na ndugu zangu kama wapo, ila ukapita mwaka mzima sikupata jibu,” anasema.
Mwaka mmoja baadaye, anasema mjumbe wake alirejea na picha ya mke wake ikionyesha kwamba bado yupo hai, jambo ambalo lilisaidia kubadili mawazo yake.
Anasema aliambiwa kwamba mkewe amesema anaomba mumewe arejee nyumbani kwa kuwa bado anaendelea kumsubiri akiamini ipo siku atarejea Rwanda.
“Nilipoiona tu ile picha, moyo wangu ulisimama kwa mshangao, machozi yalinitoka. Kumbe bibi yangu bado yupo na ananisubiri. Ilikuwa kama ndoto. Nikauliza tena, yuko hai? Ameolewa? Nikaambiwa bado ananisubiri mimi,” anasema Damascene.
Anasema hata hivyo furaha yake ilichanganyika na hofu. Licha ya hamu kubwa ya kutaka kurejea Rwanda kumtafuta mke wake ili waonane tena, vitisho vilivyokuwa vikienezwa vilimfanya arudi nyuma.
Anasema walikuwa wakielezwa kwamba wanajeshi wote waliokimbia nchi hiyo wakirudi, wangeuawa.
Lakini hatima ilikuwa na mpango mwingine.
Anasema kulikuwa na mjomba wake (hakumtaja jina), aliyekuwa akiwasiliana naye na alikuwa akifahamu alikokuwa akiishi Congo. Aliamua kuchukua hatua ya kumsaka mke wake Rwanda na kumpeleka Congo.
“Hii ni baada ya miaka 13 ya kusubiri, hatimaye tukaonana tena na mke wangu. Yeye alinivumilia kwa miaka 13 na mimi nikamvumilia kwa miaka 13. Sasa tukakutana tena. Sikuamini, ila ikawa kweli,” anasema Damascene.
Damascene anasema furaha ya kukutana tena na mkewe ilifuatiwa na uamuzi mgumu uliotoka kwa mkewe.
Alimpa sharti kwamba kama anampenda kweli, warudi pamoja Rwanda wakaendelee na maisha yao kama zamani, kwa sababu alipoondoka alimuacha akiwa na mtoto mmoja (sasa wana watoto watatu).
Na asipokubali, basi kila mmoja aendelee na maisha yake, na kama angerudi Rwanda na akapata mtu wa kumuoa, angeolewa na asingeendelea kumsubiri.
“Kauli ile iliniumiza sana kwa sababu tumekutana wote tukiwa hai, wote tumevumiliana kwa miaka 13 tukisubiri siku hii. Sikuweza kukubali kumpoteza tena.”
Damascene anasema mwaka 2012 alichukua uamuzi mgumu wa kurejea Rwanda akiwa ameambatana na mkewe.
Anasema kinyume na matarajio yake, hakukutana na madhara kama waliokuwa wakielezwa awali kwamba waasi wote wanaorejea nchini humo Serikali ya Rwanda inawaua au kuwashitaki.
Anasema badala yake alipokelewa vizuri na kupewa nafasi ya kujifunza na kujijenga upya.
Leo hii, Damascene anasema maisha yake ni ushuhuda wa mabadiliko. Anahudumu katika Mamlaka ya Mapato na wakati huo huo anaendelea na wito wake wa uchungaji.
Kinachovutia zaidi ni kwamba wale waliokuwa maadui wake vitani sasa ni marafiki zake wa karibu, anasimulia Damascene.
Anatoa wito kwa Wanyarwanda waliokimbia nchi yao kurejea kwa sababu nchi yao imetulia na wananchi wanaishi kwa umoja na amani na hakuna tena mikwaruzano.
“Saa hii bibi yangu, wakati tunakuja, tulikuwa tunaishi kwenye nyumba iliyobomoka, lakini sasa tumejenga nyumba nzuri. Mimi nina kazi na yeye anafanya biashara ya kuchukua nguo China na kuja kuuza. Maisha yanasonga,” anasema Damascene.
Anasema tangu amerejea Rwanda kutoka mafichoni Congo, ameshatimiza miaka 10 na hakuna mtu anayembugudhi.
“Wakuje tujenge nyumba yetu, nchi yetu, kwa sababu nchi iko na amani kubwa sana.”