Wizi waongoza sababu watu kuingia magerezani

Dar es Salaam. Wakati makosa matano yakitajwa kuongoza kwa kuwa na wahalifu wengi waliopelekwa gerezani mwaka 2025, wizi umebeba asilimia 72.89 ya wahalifu hao.

Mbali na mwaka 2025, wizi umetajwa kinara katika kipindi cha miaka miwili mfululizo kwa kuwa na watuhumiwa wengi, ripoti ya Takwimu za Wafungwa na Mahabusu Tanzania Bara 2025 iliyotolewa na Jeshi la Magereza inaeleza.

Ripoti hiyo iliyotolewa mwishoni mwa Machi 2026 inaonyesha makosa hayo matano yalikuwa na jumla ya wafungwa na mahabusu 87,618 mwaka 2025, kati ya hao 63,866 walikuwa na makosa ya wizi, kuvunja na kuiba pamoja na unyang’anyi.

Hali hii inaelezwa na wadau kuwa inachangiwa na kukosekana kwa ajira ambazo zinaweza kuwaingizia watu kipato, hali inayofanya watafute njia mbadala ya kukabiliana na changamoto za maisha.

Wadau wanasema hayo wakati ambao Jeshi la Magereza limeanzisha programu za mafunzo ya ufundi stadi, wafungwa hupewa ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa kitaifa na kimataifa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, makosa yaliyokuwa na wahalifu wapya walioingia magerezani kwa upande wa wafungwa, wizi walikuwa 8, 648, kujeruhi 3, 249, kuvunja na kuiba 1, 594, kubaka 1, 241 na unyang’anyi 570.

Kwa upande wa mahabusu watuhumiwa walioshtakiwa kwa makosa ya wizi walikuwa 25,616, kujeruhi 8,321, unyang’anyi 9,459, kupatikana na nyara za Serikali 6,905, kuvunja na kuiba 12,328.

Kwa upande wahalifu waliokuwepo magerezani kwa mwaka huo, wa wizi walikuwa 3,583, kujeruhi 1,083, kuvunja na kuiba 728, kubaka 1,462 na mauaji ni mauaji 894.

Kwa upande wa mahabusu waliokuwa na makosa ya wizi walikuwa 1,271, kujeruhi 159, kuvunja na kuiba 69, kubaka 183, mauaji 247.

Ingawa ripoti ya Magereza haijaeleza sababu za mgawanyiko huo, Profesa wa Uchumi Abel Kinyondo amesema hali hii inachochewa na mambo mawili ambayo ni uchumi duni na malezi.

Anasema mtu hawezi kuwa na kila kitu akaiba na kuwa malezi mabaya yanaweza kumfanya hata aliyekuwa nacho akaiba.

Amesema ili kutoka huko lazima hayo yafanyiwe kazi kwa pamoja kwanza kwa kuhakikisha uchumi unakuwa shirikishi ili watu wote wapate kipato badala ya uchumi kuendelea kusemwa unakua lakini watu wengi hawauoni mifukoni mwao.

“Wengi wamekuwa watazamaji, wanaona watu wengine wanafanikiwa wakati kwao haipo hivyo. Hili ni tatizo la kiuchumi na lisipofuatiliwa litaongeza idadi ya wezi, kwani vijana wakikosa fedha na chakula wanazo nguvu wanazoweza kuzitumia katika kuiba,” amesema.

Amesema ujenzi wa uchumi uende sambamba na maadili yatakayomfundisha mtu na kumkataza kuiba kwa sababu ana njaa, lakini akikosa mafunzo hayo anaweza kuwa na hela nyingi lakini akiona nyingine akaiba kwa tamaa.

“Serikali inaweza kuweka mchango kidogo kwa kufundisha maadili katika mfumo wa elimu na kuweka sheria kali za kimaadili, lakini hawawezi kufanikiwa peke yao bali wengine wanaoweza kubadili hali hii ni wakuu wa dini na familia,” amesema.

Amesema ili somo hilo lipate nguvu inapaswa mtu alisikie kila anapokwenda kama ni kanisani, msikitini na nyumbani akumbushwe ili mwisho wa siku mtu akatae kufanya baya kwa sababu anahitaji kitu fulani na kuridhika na chochote ulichonacho.

“Serikali peke yake haiwezi kusimamia hili, watu tofauti wakiungana wanaweza kusaidia kutokomeza suala hili,” anasema.

Mtaalamu wa saikolojia, Charles Kalungu amesema malezi yana mchango mkubwa katika kujenga na kubomoa tabia ya mtu.

“Mtoto anapokua anazoeshwa kupewa vitu, siku akikosa lazima agombane na wazazi kwa kudhani ni haki yake kupewa kila anachokihitaji. Jambo ambalo humfanya aingiwe na tamaa ya kuiba na hivyo kuanza kutengeneza tabia ya tamaa, ambayo hupelekea kuiba vitu au pesa kama asipopewa,” amesema Kalungu.

Amesema ili kuhakikisha suala hilo haliathiri tabia na ukuaji wa watu ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha kwamba, anamfundisha mtoto maisha ya kupata na kukosa, kwani ndiyo msingi bora wa uvumilivu na utoshelevu.

Akizungumzia suala hili, Zaujiati Marwa, mkazi wa Dar es Salaam amesema malezi na kukosa uangalizi mzuri wa wazazi yanaweza kuwa moja ya sababu ya kuendelea kuwapo kwa matukio hayo katika jamii.

“Baadhi ya wazazi hawajui watoto wao wanavyoishi huko mitaani, wanachojua tu wanatoka na kurudi, hawajui tabia zao zikoje kwa kisingizio cha kufanya kazi kupita kiasi ili kujenga maisha ya baadaye, wasijue kizazi chao kinaangamia,” anasema.

Maneneno yake yaliungwa mkono na Zuberi Hassan mkazi wa Tabata anayesema wakati mwingine kupata idadi kubwa ya watoto kuliko uwezo wa kuwahudumia inaweza kuwa chanzo cha uhalifu.

“Watoto wanakosa uangalizi kwa sababu chakula hakuna, hawapati mahitaji muhimu kwa ajili ya kufanikisha kile wanachohitaji mwisho wa siku wanaingia katika makundi mabaya, kwa sababu mzazi huwezi kufuatilia anachofanya mtoto, anahisi jukumu lake ni kuzaa tu,” amesema.

Amesema umefika wakati sasa wazazi kuhakikisha wanapata watoto kulingana na uwezo wao wa kuwalea ili kupunguza utegemezi au kukosa huduma za muhimu wanapohitaji.

Wakati haya yakifanyika, Jeshi la Magereza kutokana na kutambua uhalifu kwa kiasi kikubwa unachochewa na umaskini, ukosefu wa ajira na ujuzi walilazimika kuja na programu za mafunzo ya ufundi stadi.

Kupitia programu hizo wafungwa hupewa ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa kitaifa na kimataifa.

“Mafunzo haya hutolewa katika fani mbalimbali kama vile ufundi umeme, useremala, ushonaji, uchomeleaji, kilimo cha kisasa na ufugaji. Kwa kuzingatia mitaala inayotambuliwa na mamlaka husika kama Veta na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) wafungwa hupata vyeti vinavyotambulika kitaifa, jambo linalowawezesha kuajiriwa au kujiajiri baada ya kuachiwa,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Mkakati huo unalenga kugeuza magereza kuwa vituo vya uzalishaji, maarifa na ujuzi badala ya kuwa maeneo ya kutumikia adhabu pekee na tayari katika mwaka 2025 wafungwa 239 walipatiwa vyeti vya kuhitimu mafunzo ya ujuzi mbalimbali.

Katika kipindi husika pia wafungwa 129 walipatiwa mafunzo ya ufundi stadi na kutunukiwa vyeti na (Veta) katika mikoa mbalimbali nchini ambapo kati wanaume walikuwa 124 na wanawake walikuwa watano.

Mkoa wa Dar es Salaam uliongoza kwa kuwa na wafungwa 56, Kilimanjaro 22, Manyara 18 na Mbeya 11.

Mikoa iliyokuwa na wafungwa wachache waliopata elimu ya ujasiriamali ni Tabora mmoja, Katavi wawili na Lindi wawili.

Pia mwaka 2025, wafungwa 45 walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali ambapo kati yao wanaume 35 na wanawake 10 huku ambapo Kilimanjaro walikuwa 26, Dodoma 16 na Tanga watatu.