Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Charles Kichere amebaini utendaji usioridhisha wa viwanda vya dawa nchini, ikiwemo kutotumika kwa mitambo ya uzalishaji dawa katika kiwanda cha dawa Idofi kilichopo mkoani Njombe, yenye thamani ya Sh7.96 bilioni.
Pamoja na hayo amebaini mapungufu katika sekta ya dawa nchini, ukiwemo uwekezaji wa mabilioni ya shilingi uliokosa tija, pamoja na changamoto katika Bohari ya Dawa (MSD) na kwenye vituo vya afya nchini.
Hayo ameyabainishwa katika Ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha 2024/2025 iliyokabidhiwa katika Bunge la Tanzania leo Ijumaa, Aprili 10, 2026.
Katika Ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma uliofanyika Oktoba 12, 2025 katika kiwanda cha dawa cha Idofi kinachomilikiwa na Kampuni ya Medipharm, CAG anasema alibaini kuwa mitambo ya uzalishaji iliyonunuliwa zaidi ya miaka minne iliyopita bado haijaanza kutumika.
Mitambo hiyo, yenye thamani ya Sh7.96 bilioni, imesalia bila kazi kutokana na kuchelewa kukamilika kwa majengo yanayotakiwa kuendana na viwango vya Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Tanzania (TMDA) pamoja na uhaba wa fedha.
Ripoti inaeleza kuwa majengo yenye thamani ya Sh3.85 bilioni hayajakamilika tangu Mei 15, 2023, kutokana na changamoto za kifedha na marekebisho ya kiufundi.
Medipharm, ambayo inategemea Bohari ya Dawa (MSD) kama mmiliki wake, imeathiriwa pia na changamoto za kifedha za taasisi mama kutokana na madeni ya muda mrefu kutoka serikalini.
“Kutokana na hali hiyo, mitambo hiyo inakabiliwa na hatari ya kupoteza thamani, kuharibika au kushindwa kutumika ndani ya muda wa dhamana. Hata hivyo, hatua mbadala zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kusimika kiwanda cha uzalishaji wa dawa za maji na kuanza mazungumzo na wadau kwa ajili ya matumizi ya mitambo hiyo,” ameeleza CAG.
Katika kiwanda kingine cha Mabibo, kilicho chini ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Dawa, CAG alibaini kushuka kwa kasi kwa uzalishaji, ambapo kilifanya kazi kwa asilimia 5 tu ya uwezo wake katika mwaka wa fedha 2024/25.
Ripoti inaeleza kuwa mapato halisi ya kiwanda hicho yalifikia Sh82.03 milioni pekee, tofauti kubwa na makadirio ya Sh2.04 bilioni. Mwaka uliotangulia, anasema kiwanda hicho kilifanya kazi kwa asilimia 8, hali inayoonyesha kushuka kwa ufanisi.
CAG anabainisha sababu ya kushuka kwa uzalishaji ni mipango duni ya upatikanaji wa malighafi, jambo linaloathiri uendelevu na ukuaji wa kiwanda hicho.
Katika mapendekezo yake, CAG ameitaka Medipharm na MSD kuharakisha upatikanaji wa fedha na kukamilisha miundombinu ili mitambo iweze kufanya kazi. Aidha, ameshauri kuwepo kwa mikakati madhubuti ya matumizi ya mitambo hiyo kabla ya kuharibika au kupitwa na wakati.
Kwa upande wa Kiwanda cha Mabibo, amependekeza Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Dawa kuhakikisha mpango thabiti wa upatikanaji wa malighafi unaandaliwa ili kiwanda kiweze kufanya kazi kulkingana na uwezo wake na kuongeza tija ya uzalishaji.
CAG amesema deni la Serikali kwa MSD limeongezeka hadi Sh321.31 bilioni likihusiana na bidhaa za afya za miradi misonge, kati ya deni lote la Sh476.11 bilioni hadi Juni 2025.
“Kuongezeka kwa deni hili kunatokana na bajeti kutokidhi mahitaji halisi ya malipo ya dawa na vifaatiba vinavyosambazwa kupitia MSD,” amesema CAG katika ripoti yake.
Ameeleza kuwa hali hiyo ni kinyume na kanuni ya fedha ya mwaka 2024 inayotaka malipo ya huduma za dawa kufanyika kwa wakati, isipokuwa kwa mikopo ya muda mfupi yenye kibali maalumu.
CAG ameonya kuwa deni hilo linaweza kuathiri uaminifu wa wasambazaji na kuleta changamoto za ukata katika mnyororo wa usambazaji wa dawa nchini.
Hata hivyo, amebainisha hatua zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo kutoa Sh50 bilioni, Agosti 2025 kwa ajili ya kulipa deni lililothibitishwa, pamoja na kuongeza bajeti ya dawa kutoka Sh200 bilioni hadi Sh350 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26.
“Ni muhimu kuhakikisha ongezeko hili la bajeti linaendana na ulipaji wa madeni ili kuimarisha huduma za afya na uaminifu kwa wasambazaji,” aliongeza.
Aidha, CAG anasema katika mwaka wa fedha 2024/25, MSD ilipokea oda za zaidi ya Sh638.73 bilioni kutoka vituo vya afya, ambapo asilimia 99.6 zilitimizwa ndani ya muda, jambo linaloonyesha maboresho ukilinganisha na miaka iliyopita.
Hata hivyo, oda zenye thamani ya Sh2.77 bilioni hazikutekelezwa, hali inayohitaji uboreshaji zaidi wa mifumo ya usambazaji ili kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi kwa wakati.
CAG ametoa wito kwa Wizara ya Afya na Wizara ya Fedha kuimarisha usimamizi wa bajeti na malipo ya dawa ili kuhakikisha huduma endelevu na kupunguza deni linaloongezeka.
Katika ripoti hiyo, CAG Kichere anasema MSD ilipokea dawa na vifaatiba vyenye thamani ya Sh20.28 bilioni vikiwa vimebakiza muda mfupi wa matumizi, kinyume na miongozo ya usimamizi wa ghala.
“Kwa mujibu wa muongozo wa mwaka 2018, bidhaa zinapaswa kuwa na angalau asilimia 80 ya muda wa matumizi au miaka miwili. Hata hivyo, tulibaini dawa 4,389,681 zilikubaliwa zikiwa na muda mfupi zaidi,” amesema CAG bila kutaja muda huo.
Ameongeza kuwa hali hiyo inachangiwa na uhaba wa dawa ghalani na udhaifu wa mfumo wa ununuzi na ufuatiliaji wa mikataba na wasambazaji.
“Matokeo yake ni kuharibika kwa dawa zenye thamani ya mabilioni ya shilingi na nyingine kubaki na muda mfupi wa matumizi, jambo linalohatarisha upotevu wa rasilimali,” anaongeza.
CAG anasisitiza umuhimu wa kuboresha usimamizi wa mnyororo wa usambazaji na utekelezaji wa mikataba ili kuzuia upotevu wa dawa na kuongeza ufanisi wa huduma za afya.
Pia, amebaini MSD ilihifadhi dawa na vifaatiba vyenye thamani ya Sh21.5 bilioni kwa muda wa miezi 11 hadi 69, kinyume na kikomo cha miezi 10 kilichowekwa na mwongozo wa mwaka 2018.
“Dawa kukaa muda mrefu ghalani kunasababisha mtaji kukwama na kuongeza hatari ya kuisha muda wa matumizi na hasara kwa Serikali,” anasema CAG.
Anaongeza kuwa changamoto hiyo inachangiwa na makadirio yasiyo sahihi ya mahitaji na mabadiliko ya magonjwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuboresha mfumo wa makadirio na usimamizi wa dawa.
CAG pia ameshauri kuwepo kwa mfumo wa kiotomatiki wa kufuatilia muda wa dawa ghalani ili kuchukua hatua mapema kabla ya kuharibika.
Katika hatua nyingine, amesema MSD ilichelewa kutekeleza oda 8,055,135 zenye thamani ya Sh36.39 bilioni, kinyume na muda wa siku 14 uliowekwa katika mkataba wa huduma kwa wateja.
“Ucheleweshaji huu unatokana na changamoto za kukadiria mahitaji, upungufu wa bidhaa ghalani, na kuchelewa kwa uthibitisho wa malipo kutoka kwa wateja,” anasema CAG.
Anaongeza kuwa hali hiyo inadhoofisha utoaji wa huduma za afya na kupunguza imani ya wananchi kwa MSD.
CAG ameshauri kuboreshwa kwa usimamizi wa dawa ghalani na kuanzishwa kwa utaratibu wa malipo kabla ya utoaji wa oda ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji.
Katika ripoti hiyo, CAG anasema alibaini vifaa tiba vyenye thamani ya Sh5.17 bilioni katika vituo 28 vya afya vimesalia bila kutumika kutokana na changamoto za rasilimali watu na miundombinu.
“Vifaa hivi havitumiki kutokana na ukosefu wa watumishi wenye utaalamu, majengo yasiyokamilika, upungufu wa vitendanishi na miundombinu isiyotosheleza. Hii inapunguza ubora wa huduma na kuhatarisha uchakavu wa vifaa,” anasema CAG katika ripoti yake.
Ameongeza kuwa vituo 15 vya huduma za afya vilihamisha Sh3.56 bilioni kutoka kwenye mifuko ya kuchangia gharama za dawa na vifaa tiba kwenda matumizi mengine, kinyume na miongozo ya usimamizi.
“Hii inaonyesha udhaifu wa ufuatiliaji na kushindwa kuzingatia miongozo ya mwaka 2017,” anaongeza.
CAG anasisitiza haja ya kuboresha usimamizi ili kuhakikisha vifaa vinatumika kikamilifu na huduma za afya zinaboreka.
