Mwenge wa Uhuru kukagua miradi ya bilioni 113 Dar

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila amesema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa kwa siku tano katika mkoa huo na utakagua na kuzindua miradi ya Sh113.5 bilioni.

Amesema Mwenge wa Uhuru utapokelewa Aprili 13, 2026 kutoka Kaskazini Unguja Zanzibar na kuanza kukimbizwa wilaya ya Ilala, Aprili 14 Wilaya ya Kigamboni, Aprili 15 Wilaya ya Temeke, Aprili 16 Wilaya ya Ubungo na Aprili 17 Wilaya ya Kinondoni.

Mbali na hayo, Chalamila amezungumzia wafanyabiashara wa Soko la Simu 200 akisisitiza tayari utaratibu wa kuwapatia mikopo wafanyabiashara wenye sifa unaendelea.

Chalamila ameyasema hayo leo Jumamosi Aprili 11, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, kutangaza ratiba ya mbio za mwenge kwenye mkoa huo pamoja na miradi itakayozinduliwa.

“Mwenge huo utakagua miradi 35 yenye thamani ya Sh113.5 bilioni, ipo miradi iliyokamilika na mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji,” amesema.

“Mwenge utakapokuwa unapita, utazindua, kukagua na kuweka jiwe la msingi pamoja na kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo, upendo, amani na mshikamano,” amesema.

Chalamila ametoa rai kwa wananchi wa mkoa huo, kujitokeza kwa wingi kupoke huku akiwataka wakuu wa wilaya kuhamasisha wananchi kujitokeza kabla ya mwenge huo kukabidhiwa mkoa wa Pwani Aprili 18, 2026.

Mbio za Mwenge huo zilianza Aprili 2, 2026, visiwani Pemba ambapo zilizinduliwa kwa kuwashwa na Rais wa Zanzibar, Dk Husein Mwinyi ambapo utakimbizwa mikoa yote ya Zanzibar na Tanzania bara na kuhitimishwa mkoani Rukwa Oktoba14, 2026.

Wafanyabiashara Simu 2000

Aprili 6,2026 Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza na wafanyabiashara wa soko 2000 aliagiza  uongozi wa mkoa na wilaya kukusanya taarifa za wafanyabiashara waliopata hasara au waliokuwa na mikopo kutokana na moto uliounguza biashara zao kwenye soko la Simu 2000.

Amesema taarifa hizo ni kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara hao kushirikiana na taasisi za kifedha ili kupata suluhisho la haraka la mikopo yao.

“Pateni orodha ya wote walioathirika, mjue wamekopa wapi, tuzungumze na taasisi husika ili wapate nafuu na waweze kuendelea na biashara zao,” amesema.

Chalamila amesema maagizo yaliyotolewa na viongozi wakuu Serikalini yanatekelezwa ikiwamo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe.

Profesa Shemdoe aliagiza Serikali ya mkoa huo wafanyabiashara hao kuwekewa meza na mkandarasi wa soko hilo kukamalisha ujenzi ndani ya miezi mitatu hadi minne linatekelezwa.

Chalamila amesema: “Kuhusu mikopo wafanyabiashara wote wenye sifa wanaendelea kujaza nyaraka mbalimbali ili kukamilisha taratibu za kupata mikopo kama ambavyo Serikali imeahidi.”

James Peter, mkazi wa Dar es Salaam amesema hatua ya Serikali kutoa mikopo kwa wanyabiashara walioathirika na moto soko la Simu 2000 ni kuwajali wafanyabiashara.

“Serikali imefanya uungwana sana kuwasaidia wafanyabiashara kwasababu walikuwa na mitaji ambayo sasa imeteketea, kuwanyanyua kwa mikopo kutawaondoa kwenye umasikini,”amesema.

Pia, Chalamila amezungumzia suala la mafuta kwa mkoa wa Dar es Salaam akisema, hakuna wasiwasi ya ukosefu wa mafuta kwani yapo ya kutosha, akisisitiza mkoa huo ndio mafuta mengi hupakuliwa kutokana na uwepo wa bandari

Amesema kinacholalamikiwa sasa ni bei ya nishati hiyo iliyopanda katika soko la Dunia, akisisitiza ni muhimu Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) kusikiliza malalamiko ya wasafirishaji ndani ya mkoa huo