DK.DIMWA:MAFUNZO KWA MAKADA CCM NI MUHIMU KWA UJENZI WA CHAMA CHETU

Na Mwandishi Wetu,Zanzibar

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohammed Said Mohammed (Dimwa), amesema kuandaa mafunzo kwa makada wa chama hicho ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ujenzi wa chama pamoja na kuandaa viongozi wenye uwezo na maadili ya uongozi bora.

Dkt. Dimwa ameyasema hayo leo Aprili 11,2026, wakati akifungua rasmi mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, yaliyofanyika katika Ukumbi wa ofisi Kuu za Chama hicho Kisiwandui Zanzibar.

Amesisitiza kuwa falsafa ya uongozi bora inahitaji kiongozi kuwa mtendaji madhubuti anayezingatia misingi ya uwajibikaji na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yake.

Amebainisha mambo matano muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na viongozi hao ni utendaji,usimamizi, utekelezaji,ufuatiliaji na tathmini.

Aidha, Dkt. Dimwa amewataka makada hao kuepuka kufanya kazi kwa mazoea, badala yake wazingatie taratibu, kanuni na miongozo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuongeza ufanisi na kuleta matokeo chanya ndani ya chama.

Katika hatua nyingine, ameeleza mafunzo hayo yamelenga kuwaimarisha makada katika maeneo mbalimbali muhimu ikiwemo utunzaji wa siri za chama, kuzingatia itifaki na maadili ya viongozi, pamoja na kuelewa vyema wajibu wao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa chama mwaka 2027.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa makada na kuimarisha mshikamano ndani ya chama, hatua ambayo ni muhimu katika kukiandaa chama hicho kwa mafanikio ya chaguzi zijazo.