Samia atunukiwa shahada ya saba ya heshima

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameongeza orodha ya heshima anazopata kimataifa baada ya kutunukiwa shahada ya saba ya heshima, safari hii kutoka Chuo Kikuu cha Nasarawa nchini Nigeria.

Shahada hiyo ya heshima imetolewa na chuo hicho kikuu leo, Jumamosi, Aprili 11, 2026, kwa kutambua mchango wa Rais Samia katika kuimarisha uongozi barani Afrika, kukuza ushirikiano wa kimataifa na kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Rais Samia ametunukiwa shahada hiyo kwa njia ya mtandao akiwa Ikulu, jijini Dodoma, katika shughuli iliyoshuhudiwa na watendaji mbalimbali wa Serikali, wakiwemo wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Rais Samia amesema heshima aliyopewa si yake peke yake bali ni heshima kwa Watanzania wote kutokana na mchango wao katika maendeleo ya taifa na bara la Afrika.

Rais Samia amesema anaitambua heshima hiyo kama ishara ya kuthamini juhudi za Watanzania katika kujenga taifa na kuchangia maendeleo ya bara.

“Nilifurahi nilipopokea barua iliyonifahamisha kuhusu shahada hii ya heshima ambayo nimeelezwa nimeipata kutokana na mchango wangu katika maendeleo ya bara la Afrika.

“Binafsi naamini heshima hii si yangu peke yangu bali ni ya wananchi wote wa Tanzania, hivyo naitoa shahada hii kwa Watanzania wote,” amesema.

Katika hotuba yake, Rais Samia ameeleza kuwa katika kipindi chote cha uongozi wake amekuwa akitoa kipaumbele katika kuwawezesha wanawake na wasichana ili washiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

Amesema amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika uongozi, elimu na shughuli za kiuchumi, akiamini kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana iwapo wanawake wataachwa nyuma.

“Nimekuwa kinara wa kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika uongozi, elimu na shughuli za kiuchumi, nikifahamu kuwa hakuna jamii inayoweza kufanikiwa kama wanawake wako nyuma,” amesema.

Amesema kupokea heshima hiyo kunamletea majukumu mapya ya kuwa balozi wa chuo hicho na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma kati ya chuo hicho na Tanzania.

Aidha, amemwelekeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, kuangalia namna ya kuanzisha ushirikiano kati ya Tanzania na Chuo Kikuu cha Nasarawa katika maeneo mbalimbali ya elimu.

Ametaja baadhi ya maeneo yanayoweza kuangaliwa kuwa ni pamoja na kubadilishana wanafunzi, kufanya ziara za masomo pamoja na kutumia fursa nyingine za kitaaluma zitakazowanufaisha wananchi wa nchi zote mbili na kufungua milango ya ushirikiano mpana zaidi katika elimu na tafiti kati ya Tanzania na Nigeria.

Kwa kutunukiwa shahada hiyo, Rais Samia sasa anakuwa amepokea jumla ya shahada saba za heshima kutoka vyuo vikuu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Miongoni mwa taasisi zilizomtunuku ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambacho Novemba 30, 2022 kilimtunuku Shahada ya Heshima ya Doctor of Letters (D.Litt) kwa mchango wake katika kuimarisha elimu, demokrasia na maendeleo ya jamii.

Aidha, mwaka 2023, Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha India kilimtunuku Shahada ya Heshima ya Uzamivu (PhD Honoris Causa) kwa kutambua mchango wake katika kukuza diplomasia na ushirikiano wa kimataifa.

Katika mwaka huo huo, Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza) kilimpatia Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Usimamizi na Masoko ya Utalii kwa mchango wake katika kukuza sekta ya utalii.

Aprili 17, 2024, Rais Samia alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Uchumi na Chuo Kikuu cha nchini Uturuki, pamoja na Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Usimamizi wa Usafiri wa Anga kutoka Chuo Kikuu cha Anga cha Korea Kusini (KAU), kwa kutambua mchango wake katika mabadiliko ya sera na uongozi wa kimantiki.

Aidha, Novemba 24, 2024, Chuo Kikuu Mzumbe kilimtunuku Rais Samia Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Uongozi, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuimarisha utawala bora na maendeleo ya taifa.